NAIROBI, KENYA
MKE wa Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini hapa, Raila Odinga, Ida Odinga amesema hakupenda kuolewa na mwanasiasa tangu akiwa chuoni na kwamba alipokutana na mumewe huyo hakuwa mwanasiasa.
Ida alisema hayo juzi wakati wa mazishi ya Profesa Rok Ajulu, ambaye alimuelezea kuwa alisababisha awachukie wanasheria, wanasayansi za siasa na wanasiasa wakati akisoma Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alisema Ajulu alisababisha asome kwa miaka mitano badala ya minne ya kawaida.
“Nilikuwa nachukua shahada ya kwanza ya elimu ambayo huchukua miaka minne lakini wakati Ajulu na rafiki yake James Orengo walipoongoza vuguvugu la wana msimamo mkali, nililazimika kukaa kwa mwaka mwingine wa tano,” alisema Ida.
Mke huyo wa Raila alisema ni kwa sababu hiyo yeye na marafiki zake waliapa kutoolewa na wanasheria, wanasiasa na wanasayansi wa siasa.
“Kwa sababu hiyo wakati nilipoonana na Raila hakuwa mwanasiasa na aliniambia kwamba yeye ni mhandisi, nilijua alikuwa mtu maalumu kwangu,” alisema.
Ajulu, mmoja wa wasomi, ambaye aliikimbia nchi mapema miaka ya 1980 wakati wa kilele cha kuwashughulikia walioitwa waasi, alifariki dunia Desemba 27 mwaka jana baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Alifundisha nchini Uingereza na Kenya kabla ya kuweka makazi ya kudumu nchini Afrika Kusini.
Ida aliwaambia waombolezaji kwamba wakati wa siku yake ya harusi alibaini Ajulu alikuwa na ndugu yake.
“Nilishtushwa nilipomuona mtu ambaye nilidhani sitaonana naye tena baada ya chuo kikuu akiwa ameambatana na wifi yangu. Ni hapo nilibaini Ajulu alikuwa ndugu yetu,” alisema.
Anasema tangu hapo taratibu akazoea mazingira ya kisiasa, ambayo mumewe alikuja ingia baadaye.
Aidha alimsifu Ajulu kuwa alikuwa mwepesi wa akili katika kufanya maamuzi yenye kuhamasisha demokrasia.