22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Siku 14 za kuvuna fursa

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

KUFANYIKA kwa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ni fursa nyingine kwa Tanzania.

Kuanzia kesho, wananchi wataanza kuvuna fursa zitokanazo na mkutano huo unaotarajiwa kukutanisha watu zaidi ya 1,000 kutoka nchi 16.

Mkutano huo unafanyika nchini baada ya miaka 16 tangu ulipofanyika mara ya mwisho mwaka 2003, huku Rais mstaafu, Benjamin Mkapa akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

Shughuli za mkutano huo zitaanza kesho kwa Maonyesho ya Wiki ya Viwanda ya SADC yenye kaulimbiu ‘Mazingira wezeshi ya kibiashara kwa maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda’.

Maonyesho hayo yatafanyika viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Karimjee na Gymkhana, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, hadi sasa zaidi ya wafanyabiashara 800 wamejiandikisha kushiriki maonyesho hayo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema umuhimu wa Wiki ya Viwanda kwa Tanzania ni kutangaza bidhaa inazozalisha, kupata ujuzi na uzoefu toka nchi nyingine.

Pia kuingia ubia, kupata oda ya kuuza bidhaa, kuhamasisha uzalishaji, kutambua fursa zilizopo katika nchi za SADC na kushirikiana kudhibiti bidhaa zisizofaa.

Wiki ya Viwanda itafunguliwa na Rais Dk. John Magufuli na kufungwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Matukio mengine yatakayofanyika kabla ya Agosti 17 ambayo Rais Magufuli atakabidhiwa rasmi uenyekiti, ni pamoja na vikao vya mawaziri na kufunguliwa jukwaa la kibiashara (SADC Business Forum).

Pia kutakuwa na mjadala utakaofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao utaongozwa na Rais mstaafu, Mkapa.

FURSA TARAJIWA

Kufanyika kwa mkutano huo ni fursa kwa wadau mbalimbali, hasa sekta binafsi kama vile wasafirishaji, wenye hoteli, taasisi za fedha, watoa huduma za utalii na wengine.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Faraji Mnyepe, hivi karibuni alikutana na watoa huduma za utalii na taasisi za fedha na kuwataka wajiandae kwa mkutano huo.

Baadhi ya watoa huduma za utalii na usafirishaji waliozungumza na MTANZANIA Jumapili, walisema wamejipanga vyema na wana matumanini mkutano huo utainua biashara zao.

Mkurugenzi wa kampuni inayojishughulisha na masuala ya utalii na usafirishaji ya Walpha, Richard Kashaija, alisema amejipanga vyema na tayari ametangaza huduma anazotoa kupitia tovuti ya SADC.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema mbali ya mkutano huo, bado Tanzania itakuwa mwenyekiti kwa mwaka mzima, hivyo matukio mengi ya jumuiya hiyo yatakuwa yakifanyika nchini.

“Tuna mwaka mzima wa kuwa mwenyeji, na kwa mwaka mzima nchi zote za SADC watakuwa wanakutana hapa (Tanzania), kwa hiyo kiuchumi ni fursa kubwa,” alisema Balozi Kijazi.

Wabobezi katika masuala ya SADC, wanasema mkutano huo ni fursa kwa sekta binafsi kutengeneza mtandao wa kibiashara, hasa ikizingatiwa kwamba idadi ya watu katika nchi wanachama ni karibu milioni 450, hivyo kuna soko kubwa.

Takwimu za Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonyesha mauzo ya Tanzania kwa SADC mwaka jana yalikuwa Dola za Marekani milioni 999.34 ikilinganishwa na dola milioni 877.8 za mwaka juzi.

Hata hivyo mtazamo wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) kuhusu soko hilo, ni kwamba licha ya fursa kubwa iliyopo, lakini bado Tanzania haijaweza kulitumia ipasavyo.

Bidhaa nyingi za Tanzania ambazo zimekuwa zikiuzwa katika soko la SADC ni za mazao ya kilimo, kama vile ngano, mafuta ya kula na bidhaa za nguo.

Ofisa wa Sera na Biashara wa CTI, Frank Dafa alisema; “Hatujaweza kulitumia ipasavyo soko la SADC kwa sababu kuna changamoto mbalimbali.

“Lakini fursa bado ipo, na tunachofanya ni kuzidi kuwahimiza wafanyabiashara na wazalishaji waende kwenye nchi husika kuuza bidhaa zao na kushindana.

“Changamoto kubwa tunashindana na Afrika Kusini ambayo imeendelea kiviwanda zaidi, lakini pia ni fursa kwa sababu inawapa nafasi watakaokwenda kule kuongeza ubora wa bidhaa zao ili waweze kuuza.”

Dafa alisema wamewashawishi wanachama wao kujisajili kwa wingi kwenye maonyesho ya Wiki ya Viwanda ili kuonyesha bidhaa zao.

“Tumewashawishi wanachama wetu wajisajili waweze kushiriki kwenye maonyesho, pia tumeshiriki kuchagua majina ya baadhi ya viwanda ambavyo vitatembelewa.

“Hata kama ni mzalishaji mdogo, kutakuwa na fursa ya kukutana na wafanyabiashara zaidi ya 1,000 kutoka nchi 16, hivyo tunawashawishi watu waje kuonyesha bidhaa zao ambazo ni za kipekee,” alisema Dafa.

Kwa mujibu wa Dafa, baadhi ya sekta ambazo zimepewa kipaumbele katika maonyesho hayo ni dawa za binadamu, saruji, vinywaji, nguo na Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA).

Mathalani katika sekta ya dawa, itakumbukwa kwamba Tanzania imeteuliwa kuwa mnunuzi mkuu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa nchi wanachama wa SADC, hivyo maonyesho hayo ni fursa kwa wenye viwanda vya kuzalisha dawa kuonyesha bidhaa zao.

Vitu vingine vinavyotarajiwa kuuzwa katika maonyesho hayo ni bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, wanyama, chuma, madini, bahari na nyingine.

MAANDALIZI

Maandalizi ya mkutano huo yanaendelea sambamba na shughuli mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha unafanyika kwa mafanikio na kukidhi matarajio ya nchi wanachama.

Kumbi zinazotarajiwa kutumika wakati wa mkutano huo tayari zimeandaliwa na mwanzoni mwa wiki hii, makatibu wakuu viongozi, Balozi Kijazi na Dk. Abdulhamid Yahya Mzee wa Zanzibar walizikagua na kusema kuwa wamejiridhisha na maandalizi yaliyofanyika. 

Pia maeneo mbalimbali ya jiji yamesafishwa na tayari vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 wamesambazwa kusimamia usafi wa mazingira.

Sambamba na hayo, kwa siku kadhaa sasa makundi mbalimbali yanayotarajiwa kushiriki mkutano huo wakiwemo viongozi, wafanyabiashara na waandishi wa habari yamekuwa katika jitihada za kujisajili kupata uhalali wa kushiriki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles