31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Sikieni mapya Bodi ya Mikopo

bodi-ya-mikopo-ya-elimu-ya-juu-heslbNa LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WINGU zito limeghubika suala   la waliowahi kuchukua mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na hata ambao hawakuwahi kunufaika, kwa kupelekewa madai, huku waliolipa madeni yao wakitakiwa kulipa tena.

Hali hiyo imejitokeza katika baadhi ya vyuo vikuu hususan vya Serikali kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako baadhi ya watumishi ambao hawakuwahi kusoma kwa mkopo, wamepelekewa madai hayo na kutakiwa kulipa madeni ya mkopo ambao hawaijui.

Baadhi ya waathirika wa kadhia hiyo walilieleza MTANZANIA kuwa wameshtushwa na hali hiyo na sasa wanajiandaa kwenda mahakamani.

Baadhi ya waathirika waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kuyotajwa majina yao kwa sababu ya kulinda ajira zao, walisema wameshtushwa na hali hiyo kwa sababu baadhi yao hawana elimu ya chuo kikuu na wengine walishamaliza mkopo wao.

Katika orodha hiyo wapo pia madereva ambao wanadai hawajawahi kusoma elimu ya juu lakini kwa kuwa wanafanyakazi UDSM wamepelekewa wito wa kutakiwa kulipa mkopo.

“Mimi hapa ni dereva, cheti changu nimekipata Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na sijawahi kuomba mkopo wowote zaidi ya benki kwa ajili ya kujenga nyumba.

Mmoja wa wafanyakazi wa idara ya Utawala UDSM (jina tunalo) alisema  wapo watu wanaodaiwa licha ya kuwa hawakunufaika na mkopo wakati wa masomo yao.

Chanzo chetu cha habari cha uhakika chuoni hapo kimelieleza MTANZANIA kuwa kutokana na mfumo mbovu uliokuwapo  HESLB, baadhi ya wafanyakazi wasiokuwa waaminifu walitumia mwanya huo kuandikisha wanafunzi hewa kwa kutumia majina ya baadhi ya wafanyakazi wa UDSM.

Chanzo hicho kimesema huenda pia baadhi ya wafanyakazi walihusishwa katika mpango huo wa kujipatia fedha ambazo hawakustahili, jambo ambalo linadaiwa kuanza kuwagharimu sasa.

MTANZANIA lilimtafuta Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Profesa David Mfinanga  kuzungumzia hali hiyo na akakiri kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi.

“Sisi tunachokifanya ni kuwasaidia kupata taarifa zao na kuwapa watu wa Bodi ya Mikopo, hilo ndilo jukumu letu, hayo mengine ni makubaliano binafsi kati ya mkopeshwaji na mtoa mkopo,” alisema Profesa Mfinanga na kuongeza:

“Kama chuo tumekuwa tukitekeleza wajibu wetu vizuri kwa kuhakikisha tunamkata kila mwajiriwa aliyenufaika na mkopo huo na kuipelekea bodi ya mikopo.

“Hakuna shida yoyote iliyowahi kujitokeza isipokuwa mara moja iliwahi kutokea hatukupeleka makato mwezi mmoja kwa bahati mbaya ingawa tuliwakata lakini bodi ilipotoa taarifa tulipeleka makato yao”.

Licha ya kukiri kuwapo   malalamiko, Profesa Mfinanga alisema si rahisi kufahamu idadi ya watu waliofika kwenye idara yake kulalamika au kuomba msaada kuhusu jambo hilo.

Alisema mbali na wale waliosoma chuoni hapo, pia baadhi ya wafanyakazi wa chuo hicho wanalalamikia kudaiwa mkopo huo na Bodi ingawa hawakuwahi kuuomba.

Profesa Mfinanga alisema awali walijaribu kuzungumza na HESLB na iliwajibu kwamba matatizo hayo yamekuwapo kwa muda mrefu kutokana na mifumo mibovu ya kupata waombaji (wanafunzi) wa mikopo.

“Matatizo haya hayajaanza leo yapo muda mrefu kwa hiyo haya yanayojitokeza yana uhusiano na yale ya nyuma ambako kulikuwa na matatizo mengi katika kuwapata wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Abdul-Razaq Badru alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema hajawahi kupata taarifa za watumishi kuwapa mikopo watumishi wa taasisi nyingine kwa lengo la kujinufaisha.

“Suala hili lazima lithibitishwe, binafsi sijawahi kusikia, labda ututhibitishie kwa sababu hiyo ni jinai si tena suala la Bodi.

“Na ikiwa wanaolalamika wana uhakika watuletee taarifa au kama hawatuamini wapeleke taarifa kwenye vyombo vingine kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili lishughulikiwe.

“Sheria inaelekeza kuwa mwajiri alete ripoti ya wafanyakazi aliowaajiri na vyuo walivyosoma.

“Sisi kama bodi tunakwenda katika vyuo walivyosoma kufuatilia ili kuwatambua na kwa kuwa tunapata taarifa kutoka sehemu tofauti uwezekano wa kupata taarifa zenye makosa upo,” alisema Badru.

Alisema kwa wale walionufaika na mikopo hiyo na wakalipa madeni yao kisha wakapelekewa tena madai wawasiliane  na Bodi hiyo warekebishiwe taarifa zao.

Bodi ya Mikopo imetoa siku 30 pamoja na orodha ya wadaiwa sugu huku ikitishia kuwaburuza mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles