24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi zinazomkabili Lema ni pasua kichwa

lemaa*Jopo la mawakili watano wajitosa kumtetea

Na JANETH MUSHI – ARUSHA

KESI zinazomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ni pasua kichwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mbunge huyo kufikisha nusu mwezi akiwa mahabusu bila kupewa dhamana.

Wakati hali ikiwa hivyo, hatima ya kupata dhamana inatarajiwa kujulikana leo mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi.

Akizungumza mahakamani hapo jana, Wakili  wa Lema, Sheck Mfinanga, alidai wamepokea barua kutoka Mahakama Kuu ikiwataka kufika mahakamani hapo Novemba 17, mwaka huu  ili maombi yao waliyoyawasilisha yaweze kusikilizwa.

Wakili Mfinanga, alitaja maombi hayo kuwa wanaiomba Mahakama Kuu ipitie mwenendo na uamuzi wa kuzuia dhamana kwa mteja wao uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, mwishoni mwa wiki.

Alisema maombi hayo, yamepangwa kusikilizwa na Kaimu Jaji Mfawidhi Moshi ambaye tayari alikwishatoa barua ya wito kwa mawakili wa Serikali na magereza waliopewa hati ya kumpeleka Lema mahakamani.

Mfinanga alisema katika maombi hayo, upande wa utetezi unatarajiwa kuwasilishwa na jopo la mawakili wane ambao ni Tundu Lissu, Peter Kibatala, John Mallya na Charles Adiel.

“Maombi ya barua tuliyawasilisha juzi kwa Msajili wa Mahakama Kuu tukiiomba ifanye mapitio ya majalada ya kesi za jinai namba 440 na 441 ya mwaka huu.

“Miongoni mwa maombi tunayotaka, mahakama ipitie uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi Desderi Kamugisha wiki iliyopita na madai ya mawakili wa Serikali kukata rufaa kabla hakimu hajamaliza kutoa uamuzi.

“Kwenye uamuzi Hakimu Kamugisha alitupa pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa Serikali, wakitaka mteja wetu asipewe dhamana. Na mpaka sasa bado tunahoji mawakili hao kukata rufaa kabla ya hakimu hajamaliza uamuzi wake,” alisema Mfinanga.

Alisema katika mwenendo na uamuzi huo uliokuwa na kurasa 22, hakimu mkazi alikuwa amefikia ukurasa wa 21 akiendelea kutoa uamuzi.

“Hakimu alisema mahakama inamwachia kwa dhamana, ikiwamo masharti atakayopangiwa mahakamani hapo. Lakini kabla hajaanza kutoa masharti ya dhamana, mawakili wa Serikali walikata rufaa, wakati walipaswa kusubiri uamuzi wa mahakama ukamilike na uamuzi huo utekelezwe ndipo wakate rufaa,” alidai.

Hakimu Mkazi Kamugisha hivi karibuni akisikiliza kesi ya Lema anayetuhumiwa kufanya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli alitoa uamuzi na kumwachia kwa dhamana mtuhumiwa Lema.

Kabla ya kuandika masharti ya dhamana, Wakili wa Serikali, Kadushi, alidai mahakamani kuwa wameshasajili kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi huo. Hatua hiyo ilimlazimu hakimu kufuta dhamana aliyokuwa ameiandika.

 

WAANDISHI WATISHWA

Katika hatua nyingine, usalama wa waandishi wa habari wanaoripoti kesi mbalimbali, zikiwamo zinazomkabili Lema, uko shakani baada ya jana kutishwa na askari magereza waliokuwa wamebeba silaha za moto.

Waandishi hao walifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kufuatilia kesi zinazomkabili mbunge huyo anayeshikiliwa Gereza la Kisogo mjini hapa baada ya kukosa dhamana kwenye kesi ya uchochezi dhidi ya Rais Magufuli.

Jana Lema na mkewe Neema, walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi ya kudaiwa kumtumia ujumbe wa kumwita shoga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Pia kesi nyingine, inamkabili Lema pekee yake anayodaiwa kuhamasisha maandamano.

Waandishi walioonja adha ya askari jana ni Janeth Mushi (MTANZANIA) na Lilian Joel (Uhuru).

Walijikuta wakikumbwa na mkasa huo saa 2:28 asubuhi wakati Lema alipokuwa akishushwa kwenye gari la magereza lenye namba za usajili MT 0040.

Licha ya kujitetea na kuonyesha kibali cha kupiga picha kilichotolewa na mtendaji wa mahakama na kujitambulisha, bado askari hao zaidi ya sita waliwafuata na kuwatisha kwa bunduki wakitaka wapotee eneo hilo.

Ili kujinusuru, waandishi hao walikimbia moja kwa moja hadi kwa Hakimu Mkazi, Nestory Baro aliyekuwa anaingia eneo hilo.

Baada ya askari hao kumuona hakimu huyo, walirudi kwenye gari lao.

Pia kelele za kuwaondoa waandishi eneo hilo, zilisababisha Hakimu Mkazi Mfawidhi, Augustine Rwizile kutoka ofisini kwake na kwenda kusimama nje ya mlango ili kushuhudia tukio hilo.

Hakimu Baro aliyekuwa tayari amewanusuru wanahabari, alilazimika kuongozana nao hadi kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi kuwasikiliza.

 

HAKIMU AKERWA

Akizungumzia malalamiko hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Rwizile alisema ataandika barua kwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha na Kamanda wa Polisi (RPC), kuwaelezea tabia za baadhi ya askari wanaowabughudhi waandishi wa habari na kuwafanya washindwe kutimiza wajibu wao.

“Nilikuwa hapa ofisini nikasikia kelele za askari magereza, nikasema ngoja nitoke niangalie kinaendelea nini nje. Nimeshuhudia kitendo walichowafanyia na ndiyo maana mmekuta nazungumza na kiongozi wao ili awaeleze vijana wake taratibu za kufanya kazi hapa mahakamani.

“Hapa si polisi wala magereza, huu ni mhimili unaojitegemea. Kama kuna sababu za kiusalama walipaswa kuleta taarifa kwa uongozi wa mahakama. Sasa kiongozi wao anadai baadhi ya askari ni wale wanaoleta watuhumiwa wa kesi za mabomu, kwahiyo wamezoea ku-treat watu vibaya,” alisema.

Tangu kufikishwa mahakamani kwa Lema, uhusiano wa waandishi wa habari, askari magereza na polisi umeyumba, hususani wanapokuwa wakipiga picha au kuingia ndani ya chumba cha mahakama.

 

KESI ZA LEMA

Katika hatua nyingine, upande wa Jamhuri, unatarajia kuwa na mashahidi watano katika kesi namba 352 ya mwaka 2016 ya uchochezi kwa kuhusisha watu kukusanyika na kufanya maandamano kinyume cha sheria inayomkabili Lema.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Hakimu Agustino Rwizile, Wakili wa Serikali, Fortunatus Mhalila, aliwataja mashahidi hao kuwa ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO), George Katabazi, ASP Damas Masawe (OC- CID), Adam Nyamiti, WP 6826 Ester Yohana na Ezekiel Kwayu kutoka Kitengo cha Upelelezi cha Makosa ya Jinai makao makuu Dar ss Salaam na kuwasilisha vielelezo kadhaa mahakamani hapo ambavyo wakili hakuvitaja.

Awali akimsomea hoja za awali za kesi hiyo, Wakili Mhalila alidai tarehe isiyojulikana kati ya Agosti mosi hadi 26, mwaka huu, Lema akiwa mbunge na kiongozi wa Chadema, alirekodi na kusambaza ujumbe mfupi ‘audio’, kupitia mitandao ya kijamii ‘whatsapp’, kuhamasisha watu kukusanyika na kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia Septemba mosi, mwaka huu.

Alidai kuwa Lema alihamasisha watu kutenda kosa hilo la jinai na baada ya taarifa hizo kumfikia RCO, aliamuru kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.

Lema alikana kutenda kosa hilo na kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 2, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa kwa mawakili wa Serikali kuleta mashahidi mahakamani hapo.

 

KUMKASHIFU GAMBO

Wakati huo huo, kesi namba 351 ya uchochezi kwa kutoa kauli za kukashifu dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, inayomkabili Lema na mke wake Neema Lema, imeshindwa kuendelea jana baada ya Neema kushindwa kufika mahakamani.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa hao walikuwa wasomewe hoja za awali za shtaka linalowakabili.

Mdhamini wa Neema, Happiness Charles, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa yuko Dar es Salaam katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Ilala akitarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya jinai namba 219.

Wakili Mallya, aliiomba mahakama hiyo kupokea nakala ya hati ya wito kutoka katika mahakama hiyo.

Kutokana na hali hiyo, aliiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo hadi atakapokuwapo mshtakiwa huyo ili asomewe hoja za awali.

Kesi hiyo ilihirishwa hadi Desemba 21, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles