25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Sifa zipi mwanamume huzitafuta kwa mwenzi wake? – 3

o-men-and-women-facebookNa Christian Bwaya,

TUMESHAONA jinsi mwanamume anavyohitaji kujiona kwamba ana mamlaka. Hulka hiyo humfanya atamani kusikilizwa, awe huru kufanya mambo yake bila kuingiliwa sambamba na kuwa na faragha. Tumeona kuwa unapomfanya mwanamume ajione hana mamlaka, haheshimiwi, asiye na sauti wala uhuru, ni rahisi kukuhesabu kama mwanamke asiye na sifa.

Katika makala haya, tunamalizia sifa nyingine tatu anazozihitaji mwanamume kwa mwenzi wake.

Mbinafsi anayevutiwa na mwili

Ingawa binadamu wanao ubinafsi kwa asili, lakini ubinafsi wa mwanamume unazidi ule wa mwanamke. Mwanamume wa kawaida hujifikiria zaidi yeye na mahitaji yake. Wakati mwingine hata katika nyakati ambazo haileti maana kujifikiria mwenyewe, ni rahisi mwanamume kujitanguliza.

Hali hii ya kujitanguliza inayo uhusiano wa karibu na maumbile. Mungu ameweka tamaa ya mwanamume katika macho yake. Tamaa inapotawala ufahamu wa mwanamume, kwa kawaida ubinafsi huzaliwa.

Isipokuwa katika mazingira ambayo mwanamume amebadilishwa nafsi yake, kwa kawaida anaposema anakupenda mara nyingi anafikiria mahitaji yake ya kimwili. Anafikiria sifa zako za kimwili zinazoweza kukidhi tamaa zake. Hali hii ni tofauti kwa wanawake.

Ikiwa unataka kugusa moyo wa mwanamume, hakikisha unaendelea kumvutia kimwili. Fahamu kinachomvutia na jitahidi kujiweka katika namna anayoitarajia.

Kosa kubwa wanalolifanya wanawake wengi ni kujisahau mara wanapoolewa. Unaposahau kuendelea kuwa vile ulivyokuwa kabla ya ndoa, unachochea ubinafsi wa mwanamume na kukaribisha hatari isiyotarajiwa.

Mfanye ajione anahitajika

Wanaume wanakua wakiaminishwa na jamii, marafiki rika na wakati mwingine kupitia matendo ya baba zao wenyewe kwamba wao ndio watatuzi wa matatizo. Na kwa jinsi imani hii ilivyojikita mizizi kwenye akili ya mwanamume, tukisema anaamini ni mtatuzi wa matatizo bado haitoshi… anatamani awe jibu la mambo yote.
Jaribio lolote la kumwonesha mwanaume kuwa hata asipokuwepo, hata asipofanya chochote, hata asipotoa wazo lolote, hakuna kitakachoharibika linaweza kumfanya ‘akahujumu’ uhusiano. Kumfanya ajione hahitajiki, kunaathiri kiburi chake cha uanaume (ego) na inaweza kuwa mwanzo wa matatizo makubwa.
Hata kama ni kweli unamzidi kipato, unamzidi hekima, unamzidi uelewa, jifunze kuwa chini yake na mwaminishe kuwa anahitajika na ndiye mwenye uwezo wa kutatua matatizo yenu. Mwanamume anapojua anahitajika huhamasika kukupenda. Usifanye kosa la kumfanya ajione amekataliwa.

Hapendi kubadilishwa
Kila mwanadamu hapendi kujisikia kuna mtu mahali ana mpango wa kumbadilisha. Mara nyingi tunapohisi tunabadilishwa, tunajisikia kudhalilika. Fedheha ya kubadilishwa hutufanya tujihami kwa kuzorotesha uhusiano na huyo anayejaribu kutubadilisha.

Kwa mwanamume, hali hii ya kujisikia kudhalilika anapohisi mwenzi wake anataka kumbadilisha ni kubwa zaidi. Ni kosa la jinai anapogundua kuna vitabia vyake unakazana kuvibadilisha. Mwanamume anapofahamu unambadilisha, anajiona kama mtu aliyepoteza mamlaka yake. Hawezi kukubali kirahisi.

Ni kweli yapo mambo unayohisi ni muhimu ayabadilishe. Labda ni marafiki wanaompetezea muda wake ambao angeweza kuutumia na familia, labda hana hamasa na mambo ya kidini, labda ni kazi anayofanya au tabia fulani zinazokukera. Usijaribu kuonesha nia ya kumbadilisha.
Ukitaka afuate yale unayotaka ayafanye, mkubali vile alivyo na ajue umempokea bila masharti. Kukubaliwa ni motisha ya kubadilika. Mume wako anapojua pamoja na upungufu alionao bado umemkubali alivyo, kubadilika ni suala la muda tu. Atabadilika.

Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles