24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

SIDO yanoa Wajasiriamali 20 Kilimanjaro

Na Safina Sarwatt,Moshi

Wajasiriamali wadogo 20 wamepatiwa mafunzo na Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) mkoani Kilimanjaro lengo likiwa ni kuwaandaa ili waweze kuzalisha kwa ubora sanjari na kuleta ushindani sokoni.

Mafunzo hayo yametajwa kuwa ni kichocheo katika kuhakikisha wajasiriamali wazawa wanazalisha katika mazingira ambayo yataenda kukubalika kimataifa na hivyo kuleta ufanisi tofauti na ilivyo sasa.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Makao Makuu ya SIDO, Ahemed Kitala amesema ili wajasiriamali wazawa waweze kufanya vizuri ni lazima wawe wanjaengewa uwezo mara kwa mara ili kuhakikisha wanaenda kukidhi soko la walaji.

Amesema uzalishaji kwa sasa una ushindani mkubwa hivyo katika kuhakikisha mjasiriamali anafanya vizuri sokoni ni vyema akaandaliwa ikiwa ni pamoja na kupewa darasa ili kutumia njia bora katika uzalishaji.

Kwa upande wake Meneja wa Kitengo cha kuendeleza teknlojia SIDO Kilimanjaro, Arthur Ndedya amesema katika mafunzo hayo walikuwa wamelenga kuwawezesha wazalishaji wa sabuni zote yaani za mche, unga, pamoja na za maji.

Amesema changamoto kubwa inayoighubika sekta hiyo kwa sasa ni uhaba wa vifungashio jambo ambalo linawapelekea wazalishaji hao kushindwa kuendana na kasi ya kiushindani

Kwa mujibu wa Ndedya ni kuwa baada ya mafunzo hayo Sido inaenda kuwa kama daraja yaani kuwaunganisha wajasiriamali hao ambao ni wazalishaji wa sabuni lakini kwa upande wa pili kwa wale ambao ni wazalishaji wa vifungashio

Amesema kuwa kutokana na wazalishaji hao kuwa na uhitaji wa vitu vingi wataenda kuunganishwa na mamlaka nyingine za kiserikali ili kuweza kuwarahisishi majukumu yao katika uzalishaji

Amezitaja baadhi ya mamlaka ambazo Sido itaenda kuwaunganisha na wajasiriamali hao kuwa ni pamoja na ile ya mkemia mkuu wa Serikali kwani wanatumia kemikali katika uzalishaji lakini pia shirika la viwango nchini(TBS).

Kwa upande wake, Loretta Kimath ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa mafunzo hayo amesema tayari yamemsaidia na kuwa yamemjengea uelewa namna ya kuzalisha kwa ubora zaidi lakini pia kuondokana na dhana ya kuzalisha kimazoea.

Amewataka vijana na wanawake kutambua umuhimu wa mafunzo hayo ambayo hutolewa mara kwa mara ili waweze kuzalisha kwa tija lakini pia bidhaa zao ziweze kuuzika katika masoko ya nje badala ya kubaki na dhana ya kuangalia soko la ndani pekee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles