24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kiongozi wa Mwenge aagiza Halmashauri zote kurejesha fedha walizopokea kutoka Serikali Kuu

*Ni za uwezeshaji wa Vijana Kiuchumi

*Asema ni kikwazo cha maendeleo ya mfuko huo

Na Clara Matimo, Kwimba

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022, Sahili Geraruma amewaagiza Wakurugenziwa Halmashauri zote nchini ambazo hazijafikiwa na mwenge huo kuhakikisha wanarejesha fedha walizopokea kutoka Serikali Kuu kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi kabla mwenge huo haujawafikia.

Geraruma ametoa agizo hilo Julai 12, 2022 katika kijiji cha Mwamhembo, Kata ya Malya wilayani Kwimba mkoani Mwanza, baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, kuupokea mwenge huo wa Uhuru ukitokea mkoani Simiyu.

Amesema fedha hizo zilitolewa kwa vijana kama mikopo walengwa walizitumia wakazirejesha katika halmashauri lakini cha kusikitisha kuna baadhi ya halmashauri baada ya kuzipokea hazijazirejesha serikali kuu na kuwa moja ya kikwazo cha maendeleo ya mfuko wa kundi hilo.

“Mwenge wa uhuru hautaondoka katika halmashauri zote ambazo zinadaiwa na zimeshindwa kurejesha fedha hizo kwa wakati, hivyo kwa lengo zuri la kurahisisha zoezi la mbio za mwenge wa uhuru ndani ya halmashauri zote ambazo bado hazijarejesha fedha hizo ni vyema zirejeshe kwa wakati ili zoezi liweze kwenda vizuri na kwa ufasaha zaidi, kwa maslahi mapana ya maendeleo ya vijana wa taifa hili:

“Pia, tumekuja kuendeleza mapambano dhidi ya adui maradhi, ujinga na umaskini pamoja na kupiga vita ubadhilifu wa mali za umma, sambamba na hilo tunaomba tukute taarifa za miradi ndani ya magari yetu na nyaraka halisi maeneo ya miradi pamoja na wataalamu waliopewa dhamana ya usimamizi wa miradi hiyo,” amesema Geraruma.

Amesema lengo ni kuendeleza amani, upendo, umoja, mshikamano, kudumisha uzalendo sambamba na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajia kufanyika Agosti 23, 2022.

Kwa upande wake, Mhandisi Gabriel baada ya kuupokea Mwenge wa Uhuru amesema: ”Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kilomita 563 eneo la nchi kavu na Nautical Miles 86.3 eneo la maji Ziwa Victoria,” amesema Mhandisi Gabriel.

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo mkoani humo katika Sekta za Elimu, Afya, Miundombinu, Maji na amebainisha kuwa mwenge wa uhuru utaifikia miradi 52 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 18.7 nakwamba kati ya hiyo 15 itawekewa mawe ya msingi, 29 itazinduliwa, 3 itafunguliwa na 5 itakaguliwa.

“Mwenge wa uhuru utafanya ukaguzi kwenye miradi ya anuani za makazi inayotekelezwa katika Halmashauri zote ambapo hadi kufikia Julai 3, 2022 jumla ya nyumba 653,827 zimewekewa namba sawa na asilimia 118.54, hivyo kuvuka lengo lililowekwa. Jumla ya anuani zilizosajiliwa katika mfumo ni 670,407 ambapo utekelezaji wa mkoa umekamilika kwa asilimia 102,” amefafanua Mhandisi Gabriel. 

Vilevile, amesema zoezi la uwekaji nguzo zinazoonesha majina ya barabara limekua likiendelea vema hadi Juni 30, 2022  jumla ya nguzo zilizotengenezwa ni 31,525 na kufanya utekelezaji kukamilika kwa asilimia 104.7.

Amesema mkoa huo umeendelea kutekeleza kaulimbiu ya mapambano dhidi ya lishe duni, VVU na UKIMWI na amebainisha kuwa yameendelea kupungua kutoka asilimia 15.1 hadi asimilia 8.1 mwaka hadi mwaka na kwamba vijana wameendelea kuwezeshwa kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. 

Aidha, baada ya maelezo hayo, Mhandisi Gabriel alimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Johari Samizi, ambaye alibainisha kwamba utakimbizwa wilayani humo kilomita 124.85 na utapita Kata za Malya, Mwandu, Nyambiti, Bungulwa, Walla, Ngudu, Igongwa, Ng’hundi na Hungumalwa.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 utazindua miradi mitatu ndani ya halmashauri yetu ya Wilaya ya Kwimba, utaweka mawe ya msingi na kukagua miradi mitatu katika sekta ya elimu, ardhi, maji, afya, ujenzi wa barabara na kuwawezesha vijana kiuchumi yenye thamani ya Sh bilioni 3,834,607,889.91,”amesema Johari.

Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 ni ‘Sensa ni Msingi wa Mpango wa Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Malengo ya Taifa’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles