33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Sido kufanya mabadiliko kusaidia viwanda

profesa-sylvester-mpandujiNa Hadia Khamis, Dar es Salaam

SHIRIKA la kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), limetangaza kufanya mabadiliko yenye lengo la kuleta ufanisi hasa katika utoaji wa huduma za kiteknolojia, mafunzo na fedha kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Profesa Sylvester Mpanduji, alisema hatua hiyo inafanyika kama moja ya njia za kusaidia utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.

“Tunatakiwa kuwa na uwezo wa kusaidia wajasiriamali wetu ili waweze kuwa na nguvu ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi,” alisema Prof. Mpanduji.

Alisema katika mageuzi hayo, Sido itazibadilisha idara zake za teknolojia, mafunzo na fedha kuwa vitengo vinavyojitegemea ili kuleta ufanisi wa huduma kwa wadau wake.

“Tunatarajia kuwa baada ya mageuzi haya, wadau wetu watapata kila aina ya msaada wanaohitaji kama mikopo ili kukuza mitaji yao na kuimarisha teknolojia na maarifa wanayotumia katika shughuli zao za kijasiriamali,” alisema.

Akifafanua zaidi, alisema Sido inataka kuona viwanda vidogo vikiwa na uwezo wa kuajiri Watanzania wengi na kuchangia zaidi maendeleo ya uchumi.

“Nina imani kwamba kama wajasiriamali wakipata msaada na mwongozo unaotakiwa kama teknolojia na mitaji, wataleta mapinduzi makubwa katika uchumi wetu na maendeleo katika viwanda,” alisema.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2015, viwanda 900 vilikuwa vipya kati ya viwanda 5,300 vilivyokuwapo kwa mwaka huo vilivyozalisha ajira 70,000.

Sido inalenga kupambana na umasikini na kuimarisha uchumi kwa kuendeleza viwanda.

“Tunataka kuwa taasisi kiongozi inayosaidia wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuendeleza uchumi na ushindani,” alisisitiza Prof. Mpanduji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles