29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Historia ya makocha timu ya taifa England

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

MWISHONI mwa wiki iliyopita habari ambayo iligonga vichwa mbalimbali vya habari katika soka ulimwenguni ni kuhusu aliyekuwa kocha wa zamani wa klabu ya Newcastle, Sunderland, West Ham na klabu nyingine, Sam Allardyce, kufukuzwa kazi katika timu ya taifa ya England.

Ni siku 67 tangu kocha huyo ateuliwe kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya England, huku akichukua nafasi ya Roy Hodgson ambaye alijiuzulu mara baada ya timu hiyo kutolewa katika michuano ya Euro 2016.

England ilimuamini kocha huyo kuwa ana uwezo wa kubadilisha soka na kurudisha heshima ya taifa hilo, lakini kutokana na tuhuma za kujihusisha na masuala ya uhamisho wa wachezaji kinyume cha sheria na kujipatia kitita cha pauni 400,000, kimemsababishia kufukuzwa kazi.

Mwenyekiti wa chama cha soka nchini England (FA), Greg Clarke na mkurugenzi wa chama hicho walikaa na kujadili tuhuma hizo hivyo kufikia makubaliano ya pande mbili kocha na chama cha soka.

SPOTI KIKI leo hii imekufanyia uchambuzi wa makocha ambao waliwahi kuifundisha England lakini walifukuzwa kazi kutokana na kukumbwa na tuhuma mbalimbali.

Don Revie

Mwaka 1974, Revie alipata nafasi ya kuifundisha timu ya taifa ya England kutokana na mafanikio ambayo aliyapata akiwa anaifundisha Leeds United tangu mwaka 1961 hadi 1974.

Kutokana na mafanikio hayo ambayo aliyapata akiwa na timu hiyo, England ilihakikisha inampa mkataba kocha huyo tangu mwaka 1974 hadi 1977 alipofukuzwa kazi. Miaka mitatu ilitosha kocha huyo kumchoka ndani ya timu hiyo kutokana na kushindwa kuipeleka timu hiyo katika michuano ya Euro, lakini aliweza kuipatia ushindi kwa michezo 14 kati ya 29 akitoa sare michezo nane na kufungwa michezo saba ikiwa ni sawa na asilimia 48.3.

Kwa kushindwa kuipeleka timu hiyo kwenye michuano ya Euro, walianza kumchukia na kumtaka aondoke hivyo alifanikiwa kupata timu United Arab Emirates ambapo alisaini mkataba wa pauni 340,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, hakusema kuwa tayari amejiunga na timu za Uarabuni, ila aliwapa taarifa kuwa anaelekea nchini Brazil kwa ajili ya mazungumzo na Middle East, lakini baadaye England walipata taarifa hiyo kuwa amejiunga na Falme za Kiarabu hivyo wakamfungia kujihusisha na michezo kwa miaka 10 nchini England.

Terry Venables

Huyu ni miongoni mwa makocha ambao walionekana kuwa wanaweza kuleta mafanikio makubwa ndani ya England. Kocha huyo alipewa nafasi ya kufundisha tangu mwaka 1994 hadi 1996, hivyo aliifanya timu hiyo itinge hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Euro 1996 lakini walikuja kutolewa na Ujerumani kwa mkwaju ya penalti.

Baada ya kumalizika kwa michuano hiyo kocha huyo alifanyiwa uchunguzi na kugundulika kwamba alijihusisha na uhamisho wa wachezaji kinyume cha sheria na kujipatia kitita cha pauni 50,000, hivyo alifukuzwa kazi.

Timu hiyo ilicheza michezo 23 na kufanikiwa kushinda mara 11, huku ikitoa sare mara 11 na kufungwa mara moja ikiwa sawa na asilimia 47.8.

Sven Goran Eriksson

Huyu ni kocha ambaye alipewa nafasi ya kukinoa kikosi cha England tangu mwaka 2001 hadi 2006, alitoa mchango mkubwa katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2002, ambapo aliipeleka timu hiyo hadi robo fainali sawa na mwaka 2006.

Lakini kocha huyo alifukuzwa kazi kutokana na tuhuma za kutoka kimapenzi na katibu wa chama cha soka nchini humo, Faria Alam, hivyo ikadaiwa kwamba kocha huyo anashindwa kuisimamia timu vizuri kutokana na uhusiano wake na katibu huyo.

Rekodi ambayo aliiacha ni kuisimamia michezo 67 huku akishinda michezo 40 akitoa sare 17 na kupoteza 10, ikiwa sawa na asilimia 59.7. Hata hivyo kocha huyo baada ya kufukuzwa alieleza sababu za kutoka na katibu wa chama hicho huku akidai kuwa alikuwa mrembo na mtanashati.

Fabio Capello

Aliichukua timu hiyo tangu mwaka 2008 hadi 2012 lakini alikuja kujiuzulu kutokana na tuhuma za mchezaji wake John Terry za madai kwamba mchezaji huyo amembagua nyota wa klabu ya QPR, Anton Ferdinand katika mchezo wa Chelsea dhidi ya QPR, Oktoba 2011.

Kutokana na ubaguzi ambao aliuonesha, Terry ilibidi asimamishwe michezo minne pamoja na kulipa kiasi cha pauni 220,000 kwa chama cha soka, lakini Capello alimtaka mchezaji huyo kuwa katika kikosi chake kwenye Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, ila FA ilikataa kutokana na tuhuma hizo.

Capello aliamua kujiuzulu kwa madai kuwa FA haikutenda haki kwa mchezaji huyo. Rekodi ambazo aliziacha Capello ni michezo 42 ambayo aliisimamia huku akishinda michezo 28, sare michezo 8 na kufungwa michezo 6 sawa na asilimia 66.7.

Baadhi ya makocha ambao wameifundisha England tangu mwaka 1946 ni pamoja na Walter Winterbottom 1946-62, Sir Alf Ramsey 1963-74, Mercer Caretaker, Don Revie 1974-77, Ron Greenwood 1977-82, Sir Bobby Robson 1982-90, Graham Turner 1990-93, Terry Venables 1994-96, Glenn Hoddle 1996-99, Howard Wilkinson 1999.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles