HIVI karibuni kumeibuka vita dhidi ya dawa za kulevya ambayo kwa mtazamo wangu ilivyoanza ilianza kwa sura ya siasa za umaarufu jambo ambalo linaweza kupoteza mwelekeo wa mapambano halisi.
Katika msingi huu ndio Rais alitahadharisha kuwa mzaha usitumike katikati ya mapambano haya. Mzaha unapotumika maana nzima ya mapambano inapotea. Kama Taifa hatupaswi kuvumilia na kuacha Taifa liangamie kwa sababu ya dawa za kulevya.
Dawa za kulevya ni vita inayotakiwa kupiganwa na kila Mtanzania mwenye nia njema na Taifa letu huku akiheshimu misingi ya utu, haki na sheria katika utaratibu wa kushughulikia masuala hayo.
Msingi mmoja wa haki za asili unasimama kwenye kigezo kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, kila mtu ana haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa na kuwa mtu hatakuwa na hatia mpaka atakapothibitishwa na Mahakama.
Huwezi kutumia njia zisizo za haki kupambania jambo la haki na kutweza utu wa watu wengine ndani ya vita hii.
Hivyo ninaunga mkono juhudi za Kitaifa na za Rais za kupambana na janga la dawa za kulevya isipokuwa kwa sababu ya kuwa mtu ninayependa utawala wa sheria na usimamizi wa haki katika Taifa letu siungi mkono siasa chafu za dawa za kulevya zinazolenga kutaja au kuchafua majina ya watu wenye heshima katika jamii kwa namna ambayo haifuati misingi ya haki za watu na weledi wa taaluma ya intelijensia ya kubaini nani ni mtuhumiwa na nani si mtuhumiwa.
Ni muhimu ili misingi ya haki na utawala wa sheria ifuatwe basi wale wenzetu miongoni mwetu waliopewa dhamana ya kutuongoza wawe majasiri na wenye uthubutu wa kufika kule wasikoweza kufika wengine ambao hawana dhamana hiyo.
Ujasiri na uthubutu huo usiwe wenye nia ya kuchafua taswira za wale wasiowapenda isipokuwa ujasiri na uthubutu wao wautumie kuhakikisha haki inatendeka katika mchakato mzima wa mapambano.
Vita ya siasa za dawa za kulevya ipiganwe sio kwa lengo la umaarufu wa kisiasa bali nia iwe ya dhati ya kupambana na adui halisi. Juhudi zozote zinazozingatia sheria katika mapambano haya zinapaswa kuungwa mkono.
Isipokuwa ni vema juhudi za mapambano haya zisijikite katika kuchafua watu na majina yao na heshima zao ambazo wamezijenga katika jamii kwa jasho na gharama kubwa.
Vita ya dawa za kulevya sharti ipambanwe kukiwa na dhamira safi ya kiuongozi na ipiganwe katika uwanja mahususi kwa kufuata sheria na taratibu zinazohusisha mapambano hayo.
Umevuka takribani mwaka mmoja tangu sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kupambana na dawa za kulevya hapa nchini ipitishwe na haikuwa imeanza kutekelezwa mpaka Rais alipoamua kuanza kuitekeleza rasmi kwa kuteua Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia dawa za Kulevya.
Rais ameonesha dhamira safi ya kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kufanya uteuzi huo ili kuepusha vita hivyo kupiganwa bila ya kuwa na kamanda wa vita.
Vita hii iwe endelevu isiishie hapa. Hivyo ni muhimu kutopoteza mwelekeo wa vita katika hili. Kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa namna ambayo inalipatia Taifa manufaa atakuwa ameingia katika rekodi za historia kuwa aliitumia nafasi yake vizuri.