27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

UHASAMA UNAIANGAMIZA FAMILIA YA WATAWALA KOREA KASKAZINI

KIFO cha kaka wa kambo wa Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, anayeitwa Kim Jong-nam kilichotokea siku kumi zilizopita kimezua mkanganyiko wa siasa za ‘kimafia’ za taifa hilo kutokana na sababu ya kuuawa kwake kugubikwa nadharia mbalimbali zenye utata kuhusu sakata hilo lililogeuka habari kubwa katika vyombo vya habari vya kimataifa.

Nam aliyetarajiwa kumrithi baba yake madarakani lakini alimchefua baba yake, Hayati Kim Jong-Il kwa kushirikiana na wapinzani wa taifa hilo ikiwamo Japan aliyoitembelea kinyemela mwaka 2001, figisu zilizosababisha akimbilie ughaibuni alikoishi kwa takribani miaka 14 iliyopita, mdogo wake Kim Jong-un akafanywa mrithi na Kim Jong-nam kugeuka mpinzani wa familia ya watawala akiishutumu kila mara.

Hatimaye mawindo dhidi yake yalitimia kwa kuuawa kwa kuvutishwa kemikali ya sumu katika shambulio lililofanywa na wanawake wawili katika uwanja wa ndege nchini Malaysia, wanaoshukiwa kutumwa na utawala wa Korea Kaskazini.

Aliuawa kabla hajapanda ndege kurudi Macau ingawa iliwawia vigumu polisi kuthibitisha utambulisho wake kwani ili kuepuka mawindo ya Serikali ya mdogo wake, mara nyingi alisafiri kwa kutumia majina bandia hata alipouawa alikuwa akitumia jina la Kim Chol.

Baada ya kifo chake ndipo mkanganyiko mzima ulipoibuka kwa mahasimu wa Korea Kaskazini kutamka kuwa taifa hilo linaendeleza hulka yake ya kuwaua wanaoikosoa Serikali inayofanya mambo yake kwa hali ya kuwatia kihoro wote wanaoipinga.

Korea Kusini imesema wazi kuwa ina uhakika mahasimu wake wa Kaskazini wamemuua kaka huyo wa kiongozi wa DPRK, hususani baada ya Korea Kaskazini kupinga vikali uchunguzi wa mwili wake kuhusiana na kifo hicho.

Hayo ndiyo mazingira yaliyosababisha kifo chake kugeuka habari kubwa ikihusishwa na ujasusi wa kizamani wa Korea Kaskazini. Inawezekana wengi hamkuwahi kumsikia kabla ya kifo chake lakini Kim Jong-nam alizaliwa na hawara wa Kim Jong-il aliyewahi kuzaa na wanawake watatu tofauti, kwa hiyo Nam alilelewa kwa kificho na baba yake kutokana na babu yake (Kim Il-sung) kiongozi wa kwanza wa taifa hilo kukerwa na tabia za wanawe kutumia nafasi ya baba yao kuwa kiongozi kufanya mambo yanayoiharibia sifa familia ya watawala.

Lakini Nam hakuwa akitamka kauli za kuupinga utawala wa mdogo wake wa kambo kwa kuropoka, kwa kuwa alishawahi kuhudumu katika Wizara ya Usalama wa Taifa wakati alipokuwa akiandaliwa kuwa kiongozi afuataye baada ya baba yake, akihusishwa na mambo muhimu ya Serikali ikiwamo mkabala na Taifa la China kabla ya kutengwa kutokana na misimamo yake na kutumia muda mwingi ukimbizini nje ya taifa lake.

Ndipo propaganda za kumchafua zilipoanza ili akose sifa ya kuwa kiongozi mkuu wa taifa hilo, kwa kubuniwa hadi kauli mbiu mahususi kwenye jeshi la taifa hilo: ‘Mama anayeheshimika ndiye mwaminifu kwa kiongozi wetu mkuu’ ili kumsafisha mtoto wa ndoa wa Kim Jong-il, Kim Jong-un, ambaye hatimaye alikabidhiwa uongozi wa taifa hilo baada ya kifo cha baba yake.

Nam alishutumiwa kugeuka ‘kabaila’ baada ya kuhitimu masomo yake nchini Uswiss kutokana na kutaka mabadiliko ya mfumo wa utawala, kwamba baada ya kuzaliwa ndugu zake watatu kwenye ndoa ya baba yake ambao ni Kim Jong-chol, Kim Jong-un na dada mwingine wa kambo Yo-jong ndipo umuhimu wake ulipofifia hata baba yao alipofariki Nam alirudi nyumbani kwa siri na kutoa heshima zake za mwisho lakini hakuhudhuria mazishi kutokana na figisu za kifamilia zilizomzunguka.

Ni kifo cha mtu mmoja tu lakini kimeibua figisu na mkanganyiko kwa kuhatarisha uhusiano baina ya mataifa ya Malaysia na Korea Kaskazini inavyoelekea kila upande unasukumwa na matakwa yasiyoeleweka yanayochezeshwa na wengine walioko katika kila upande husika kutokana na uhasimu wa miaka mingi.

Mamlaka nchini Malaysia iliiwekea Korea Kaskazini masharti magumu kwamba bila kudhihirisha DNA kwamba Nam ni ndugu yao, hawawezi kuukabidhi mwili wake ingawa ni wao wenyewe waliothibitisha kifo chake kwa kumtambua licha ya kusafiri kwa kutumia jina bandia.

Korea Kaskazini imetangaza kutotambua matokeo ya uchunguzi wa kitabibu kuhusiana na kifo hicho kwa kuwa umefanyika bila idhini yake, kwamba ni uvunjaji wa haki za kibinadamu na inataka kuwasilisha suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Sheria (ICJ) inayosimamiwa na UN.

Lakini mauaji hayo yanayovaliwa njuga na mahasimu wa Korea Kaskazini kiasi cha kujadiliwa katika Bunge la Korea Kusini, kwa ripoti ya mkuu wa idara ya upelelezi wa taifa hilo kwamba ni China ndiyo iliyokuwa inamlinda Nam asiuawe na mdogo wake ambaye ni kiongozi wa DPRK (Kim Jon-un) mwenye hulka ya kuwatafutia sababu na kuwaua hadi nduguze wanaoonekana kuwa tishio kwake, kama alivyowahi kuidhinisha kuuawa kwa mjomba wake aliyekuwa kiongozi mwandamizi katika chama kwa kupigwa na kombora la kutungulia ndege.

Hata taarifa za kifo cha Nam hazikutangazwa wazi nchini DPRK katika kujaribu kuthibiti fikra za wananchi zibakie kuzingatia utawala uliopo madarakani, katika nchi ambayo imetawaliwa na ukoo mmoja tangu iwe taifa huru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles