32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SHULE YA MSINGI MAWENI KUJENGWA UPYA

Na Amina Omari– Tanga


 

dscn0265SERIKALI ya Awamu ya Tano imejikita katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kutolea elimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu.

Licha ya jitihada hizo bado sekta ya elimu nchini inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo uchakavu wa majengo hali inayodumaza juhudi za kutoa elimu bora.

Shule ya Msingi Maweni iliyopo Jijini Tanga, ni miongoni mwa shule ambazo zinakabiliwa na changamoto za miundombinu hali inayoathiri utoaji wa elimu.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1975 na waliokuwa wafanyakazi wa mamlaka ya mkonge wakati huo kwa ajili ya watoto wao kupata elimu ya msingi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Debora Mzava, anasema shule hiyo ilikuwa na vyumba nane vya madarasa ambavyo vilikuwa vinatosheleza mahitaji.

“Shule ilikuwa na mkondo mmoja pekee na madarasa yaliweza kutosheleza bila wasiwasi kwa sababu ilikuwa ni shule maalumu kwa watoto wa wakulima wa mkonge,”amesema Mwalimu Mzava.

Hata hivyo kukua kwa mji pamoja kulisababisha shule hiyo kuanza kuchukua wanafunzi ambao wazazi wao si wakulima.

Hivyo walianza kupokea wanafunzi wanaoishi maeneo ya karibu na shule kwa lengo la kuwapunguzia umbali mrefu wa kutembea ili kupata elimu.

Mwalimu Mzava anasema shule hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa majengo pamoja na miundombinu mengine.

Anasema majengo ya shule hiyo ni ya muda mrefu yanahitaji ukarabati na mengine kujengwa upya ili kusaidia kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

“Shule ina madarasa nane na mpaka sasa ina mkondo mmoja huku wanafunzi wengine wakilazimika kusoma hadi 120 katika darasa mmoja,”anasema.

Mwalimu Mkuu huyo anasema kutokana na uchakavu wa majengo wakati wa mvua au upepo mkali hulazimika kusitisha masomo ili kuepuka wanafunzi kupata madhara.

“Kuna madarasa matatu yana nyufa wakati wa mvua huwa tunarudisha wanafunzi nyumbani ili kuepuka madhara,”anasema Mwalimu Mzava.

Anasema pia kuna upungufu wa matundu ya vyoo kwani kuna wanafunzi wa kiume 447 ambao wanatumia matundu matatu, huku wasichana 228 wakitumia matundu matatu,” anasema.

Licha ya changamoto ya miundombinu shule hiyo pia imelazimika kuchukua wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutokana na Jiji la Tanga kuwa na shule mmoja pekee.

Mwalimu Mzava anasema wanalazimika kuwachanga pamoja na wanafunzi wazima.

“Tuna wanafunzi 23 wenye mahitaji maalumu kutoka darasa la awali hadi la sita, kutokana na shule kukosa walimu wa kuwafundisha tumelazimika kuwachanganya na wengine,”anasema.

Kutokana na changamoto hizo hivi karibuni waliweza kupata msamaria mwema ambaye aliwapunguzia adha hiyo.

Kiwanda cha Saruji cha Simba (Simba Cement), kilichopo jijini hapa kimefanikiwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, matundu mawili ya vyoo na kutengeneza madawati 50.

Meneja Raslimali watu wa kiwanda hicho, Diana Malambugi, anasema Sh milioni 76.8 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo.

“Tunathamini sana elimu kwa sababu tunajua haina mbadala wake ndiyo maana siku zote tumekuwa tukijikita kusaidia sekta hii,” anasema Malambugi.

Anasema kila mwaka huwa wanatenga asilimia moja ya faida wanayoipata na kurudisha kwa jamii katika maeneo mbalimbali kama ya elimu, afya, mazingira na huduma zingine za kijamii.

Anasema kwa mwaka huu zaidi ya asilimia 30 ya mchango huo kwa jamii  imekwenda kusaidia sekta ya elimu.

Anasema wanahitaji wanafunzi waweze kupata elimu sahihi itakayotolewa katika mazingira mazuri ambayo yanawawezesha kuongeza kiwango cha ufaulu.

Naye Mkurungenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji, anasema kutokana na uchakavu wa shule hiyo wamelazimika kuiweka katika mpango wa maboresho makubwa.

Anasema kwa kushirikina na wafadhili wa Jeshi la Marekani wameingia mkataba wa kuijenga upya shule hiyo ili iwe na mwonekanao wa kisasa.

“Wataalamu wa ardhi wamesema kuwa eneo la shule tetemeko la ardhi huwa linapita hivyo kusababisha uharibifu wa majengo, lakini wenzetu wa Jeshi la Marekani walifanya utafiti na kuainisha namna ujenzi utakavyokuwa,”anasema Mayeji.

Anasema msaada wa Tanga Cement ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo na utakapokamilika vitajengwa vyumba vya madarasa 10 na vyoo 42.

Ofisa Elimu Msingi, Khalifa Shemahonge, anasema katika bajeti ya mwaka 2017/18 wanatarajia kutenga Sh milioni 800 kujenga madarasa mapya pamoja na kukarabati yaliyopo katika shule mbalimbali za mkoa huo.

Anasema hatua hiyo imelenga kuhakikisha shule zote za msingi zinaboreshwa kwa kuwa na mazingira mazuri ili kumaliza changamoto ya uchakavu wa majengo.

“Pia tumetenga Sh milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vipya katika shule zote za msingi na kuondoka na tatizo la uhaba wa vyoo,”anasema Shemahonge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles