26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Shule ya Msingi Mailimoja taabani, yahitaji msaada wa haraka

DSCN1027NA GUSTAPHU HAULE, PWANI

SHULE ya Msingi Mailimoja iliyopo Kibaha mkoani Pwani ni miongoni mwa shule ambazo zinapoteza umaarufu wa Mji wa Kibaha kutokana na miundombinu yake kuwa chakavu.

Shule hiyo ilianza mwaka 1975 ikiwa na madarasa manne ya udongo lakini baadae ilizaa madarasa mengine saba ambayo yalijengwa kwa jitihada za aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Profesa Phillemon Sarungi.

Kutokana na umaarufu na umuhimu wa shule hiyo lakini hali yake kwa sasa ni mbaya kwani majengo yake yamekuwa yakihatarisha maisha ya wanafunzi wake kwani madarasa yanabomoka na paa kuezuliwa.

Shule hiyo imewafanya wanafunzi wake kusomea nje chini ya miti kwa kuwa majengo yake ni chakavu na hayajafanyiwa ukarabati tangu kuanzishwa kwake jambo ambalo linahatarisha maisha ya wanafunzi hao .

Hakika, shule imetelekezwa na inatia huruma kwa kuiangalia na unaweza kusema Serikali au halmashauri haipo na hii ni aibu kubwa ya Mkoa wa Pwani ,kwani haiwezekani kuacha wanafunzi hawa wakiteseka huku viongozi wakifumba macho.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Leornad Fanuel, anasema kuwa hivi sasa shule yake ina madarasa manne tu yanayotumika na kwamba inalazimika wanafunzi wengine kuwafundishia chini ya miti.

Fanuel anasema kutokana na uchakavu wa shule hiyo mvua zinapokuja pamoja na upepo mkali zinasababisha ongezeko la shule hiyo kubomoka na hivyo kufanya wanafunzi kukosa madarasa na walimu kukosa ofisi.

Anasema, hali hiyo imewafanya walimu kwa kushirikiana na kamati ya shule na wazazi kuanza kufanya mipango jinsi ya kujadili namna ya kutatua changamoto ya shule hiyo.

Mwalimu huyo, anasema katika vikao vyao wamependekeza kuwa hatua ya kwanza watafute Sh. milioni 4.5 huku wakipendekeza kila mwanafunzi achangie Sh. 5000 ili iweze kuwa sehemu ya kusaidia katika ujenzi wa madarasa mapya.

Anasema pamoja na hilo lakini pia mwalimu huyo alikwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Jenipher Omolo kumueleza hali ya shule hiyo ikiwa pamoja na kutaka wapate msaada juu ya ujenzi wa madarasa mapya ya shule hiyo.

Fanuel anasema mkurugenzi amelipokea lakini ameahidi kuwa atajipanga ili kuona jinsi ya kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo lakini kwasasa bajeti kubwa imeingia katika ujenzi wa maabara.

Anasema pamoja na kuwepo kwa hali hiyo lakini jitihada za walimu kufanyakazi bado zinaendelea ili wanafunzi waendelee kupata elimu kwani kamwe hawataweza kuacha kufundisha kutokana na changamoto hiyo.

“Hali ya shule hii ni mbaya kama mnavyoona hapa majengo yamebomoka na paa kuanguka hali ambayo imetufanya kuwaweka wanafunzi hapa nje na kuwafundishia lakini haya mapaa yange anguka mchana wanafunzi wangepoteza maisha, tunashukuru yalianguka usiku,”anasema mwalimu huyo.

Anasema, madarasa yaliyopo yanatumika kwa awamu huku darasa la kwanza wakiingia asubuhi wanatoka saa tano ambapo muda huo darasa la pili wanaingia na kutoka jioni.

Aidha anasema, darasa la tatu wanatumia chumba kimoja na darasa la nne kwani darasa la nne wanaingia asubuhi mpaka saa sita mchana huku yakitumika na wanafunzi wengine mpaka jioni.

Anasema, wameamua kufanya hivyo ili kuwapa fursa wanafunzi hao kusoma kwa kuzingatia muda halali wa kiserikali ili wanafunzi wasikatishe masomo kwani hii itasaidia kuepusha wanafunzi kuyumba kitaaluma.

“Pamoja na kuwepo kwa upungufu wa madarasa hayo lakini bado walimu hatujakata tamaa tunatumia madarasa kufundisha kwa zamu ili kila mwanafunzi aweze kushiriki masomo yote,”anasema Fanuel.

Anasema, mbali na wanafunzi lakini hata walimu wapo katika mazingira magumu pia kwani hawana ofisi huku wakisema wanafundisha katika mazingira ambayo ni hatarishi kwako na kwamba hawataweza kuacha kufundisha kwa kuwa shule mbovu.

Shule ina wanafunzi 962 wakiwemo wanaume 402 na wanawake 560 huku kukiwa na walimu 29 wakiwemo wakike 25 na wakiume wanne hivyo anasema wanahitaji msaada mkubwa ili waweze kusaidiwa.

Pamoja na changamoto hizo lakini Fanuel anamtaja Rugemalira Rutatina ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Wilaya ya Kibaha Mjini kuwa ni kiongozi wa kuigwa kwani tayari ameonyesha jitihada za kusaidia shule hiyo.

Anasema awali aliwasaidia katika ujenzi wa vyoo vya kisasa ambavyo vinatumika kwa walimu na wanafunzi wao huku akisema awali vyoo vya shule hiyo vilikuwa na hali mbaya ya kuhatarisha maisha yao.

Anamtaka kiongozi huyo kuendelea na jitihada zake katika ukombozi wa sekta ya elimu hususani Kibaha Mjini, mkoa na hata nchi kiujumla huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza zaidi.

Jenipher Juma, mwanafunzi wa darasa la nne katika shule hiyo anaelezwa kusikitishwa na kitendo cha kusomea chini kwenye vumbi huku akisema hali hiyo itasababisha wanafunzi kufeli mitihani yao.

Jenipher ameiomba Serikali kufanya jitihada za kuwajengea shule yao ili waondokane na adha ya kukaa chini ya miti na kukaa kwenye vumbi kwani wanaweza kupata magonjwa mbalimbali.

“Siwezi kuvumilia hali hii mbaya iliyopo katika shule hii, nitajitahidi kwa kila jambo kuhakikisha nashirikiana na uongozi wa shule ,wazazi na hata wanafunzi ili tuweze kuijenga upya shule hii na iwe kwa kiwango kinachokubalika ,”anasema Rutatina.

Kutokana na hali hiyo Rutatina alilazimika kuanzisha harambee ili kupata mchango wa kuanzisha ujenzi huo ambapo katika harambee hiyo jumla ya mifuko ya saruji 190 ilipatikana na ujenzi utaanza maramoja.

Pamoja na harambee hiyo lakini Rutatina, alihaidi kuendelea kushirikiana kwa hatua moja hadi nyingine ili kukamilisha ujenzi huo lakini aliwaomba wadau wengine kujitokeza ili kuwasaidia watoto hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles