26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sera ya elimu ni mwelekeo mpya wa mafanikio

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru KawambwaNa Markus Mpangala

TANGU kutangazwa kwa mpango mpya wa elimu kumekuwa na maoni tofauti kuhusiana na suala hilo. Baadhi walikuwa wakishangazwa na mpango huo lakini wakakosa hoja za msingi kukosoa zaidi ya malalamiko ya kawaida na yaliyozoeleka.
Wakosoaji hawajatoa njia mbadala wala hawataki kuona mambo mazuri yaliyobuniwa. Binafsi ninadhani ni sahihi kubadili muundo wa elimu ambao kwa namna moja ama nyingine unatusaidia kuendelea kutumia nguvu za ujana kwa kutafuta maarifa zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Natambua changamoto iliyobaki ni suala la watekelezaji, yaani walimu. Rais Jakaya Kikwete ametamka wazi kuwa mradi unaofuata sasa ni ujenzi wa nyumba za walimu vijijini.
Eneo hilo pia limepata wakosoaji kama ilivyoada. Wanasema ujenzi wa maabara haujakamilika hivyo kujiingiza kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu vijijini ni kuongeza mzigo ambao hauwezi kutekelezwa.
Naam, hayo ni madai mepesi kwa kuwa yameegemea kwenye falsafa ya kushindwa. Wanaofikiri muda wote kushindwa ndiyo huamua kuweka kila aina ya vikwazo sababu ya mazoea yao.
Hata hivyo niseme tu, yapo mazuri ya kuzungumziwa zaidi. Mfano hapa nchini kijana wa miaka 15 hawezi kuwa mzalishaji wala mbunifu isipokuwa anakuwa anaendelea kuchezea makopo nyumbani.
Anachukuliwa kama mtoto (sababu ya katiba) lakini ukweli unabaki umri huo si kikwazo cha ubunifu wa jambo lolote. Hivyo basi, nimeona niseme machache kuhusiana na mpango huo mpya ambao naweza kusema umekuwa na mwelekeo mpya na endelevu, utajenga kizazi chenye msingi wa wajibu kungali mapema.
Mosi, naiopongeza kwa Serikali kupunguza umri wa kuanza shule, hii ina maana tutakuwa na wahitimu wa elimu ya juu wenye miaka 20 na wale wa shahada za juu wenye umri wa miaka 22.
Mhitimu huyu atajitambua mapema mno na nguvu ya mahitaji (kwa wasiopata ajira rasmi) itawasukuma kuwaza zaidi na hiyo inachochea ubunifu hatimaye maendeleo ya mmoja mmoja (nchi za Ulaya unakuta mtu ana umri wa miaka 26 lakini ana PhD.
Huyu umri unamruhusu kuendelea kusoma zaidi kitaaluma hivyo maisha hayajaanza kumzonga na hajazeeka. Lakini mfumo uliopo umewafanya wengi wapate ‘Masters’ wakiwa na umri wa miaka 28 na kuendelea).
Pili, sera hii itakamilika kutumika jumla baada ya miaka 10; hii ni nzuri kwa mtu anayetaka kukosoa au kushauri au kuongea lolote aseme ili lipewe nafasi.
Tatu, ni vema serikali ikaamua kutamka wazi kuwa Kiinegereza kitumike kufundisha shuleni (ingawa si jibu la moja kwa moja la maendeleo ya elimu, kwani lugha ya kwanza ya mhusika yaani Kiswahili inaweza kuwa na thamani zaidi ikiboreshwa).
Serikali ya awamu ya tatu na nne zimeboresha uwekezaji na mifumo yote ya mawasiliano (anga na maji bado kidogo) vijana watahitimu wangali wadogo na ajira ni popote duniani.
Wapo watakaokuwa wafanyabiashara wa kimataifa. Wapo watakaobuni na kuuza ujuzi mpya. Wawekezaji watahitaji wasomi wetu na teknolojia nyingi zinakuja kwa lugha ya Kizungu (Kiingereza) hivyo kuna uwezekano mwingine kuiomba serikali itamke tu kwamba lugha ya kufundidhia itakuwa Kiingereza badala ya kusuasua.
Nne, nchi nyingi zilianza na kuiba ujuzi kutoka nje ndio wakaja kuufanya mali yao, ili watu wetu waweze kuiba taaluma nje lazima wawe wanajua lugha hiyo kwanza.
Aidha, watoto wa miaka tatu au nne chekechekea akianza kufundishwa masomo yote kwa Kiingereza ni rahisi mno kushika na kuelewa.
Tano, masomo ya hesabu, uchumi (biashara) kilimo, michezo yapewe kipaumbele maalumu kwa kuwa hakuna serikali duniani iliyoajiri wasomi wake wote.
Hivyo basi, sisi tuwaandalie mfumo wa kujiajiri katika michezo yote, biashara kubwa, kilimo na wakipata elimu hii tangu utotoni itawasaidia hadi wanapomaliza kidato cha nne wanakuwa na umri wa miaka 15.
Kwa umri huo mhitimu atakuwa amepanuka kiakili na kimwili na asipoendelea kusoma atakuwa anajitambua – hapa ndio kuna kundi kubwa la watu hivyo ni vyema wawe na elimu niliyotaja miongoni mwa mengineyo.
Sita, kuwe na shule maalumu moja kila mkoa baadae kila wilaya, za vipaji maalumu yaani michezo.
Mwanafunzi atakayeonekana wa kipekee katika mchezo ahamishiwe shule za aina hiyo. Aidha, kila Umisseta ikifanyika washindi kila mkoa wasome shule za aina hiyo.
Vyama vya michezo vya mikoa vitakuwa karibu kutoa walimu na makocha wa michezo katika shule za aina hii. Pia tukiweza hili, miaka 20 ijayo Afrika na dunia itajua na kuiogopa Tanzania.
Vilevile tutakuwa tumeitangaza nchi yetu. Sisi hatuna taaluma au teknolojia tutakayouza hivyo lazima tuanze kujua lugha za wenzetu kwanza na baadaye ndio tuanze kutumia lugha yetu ya Kiswahili au vyovyote itakavyoonekana inafaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles