20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Shisha yapigwa marufuku nchi nzima

Uvutaji wa shisha

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amepiga marufuku uvutaji wa shisha nchini na kulitaka Jeshi la Polisi kufuatilia na kutokomeza matumizi ya sigara hiyo ili kuokoa makundi ya vijana ambao wanajihusisha na ulevi huo.

Waziri mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo juzi jijini Dar es Salaam katika futari iliyoandaliwa na waumini wa dini ya kiislamu wa madhehebu ya Shia.

“Shisha ni aina ya tumbaku inayokuwa na mchanganyiko mwingi wa vilevi mbalimbali kama gongo na viroba… na mtumiaji anayetumia kilevi hicho asipokipata na kukitumia hukosa nguvu, hivyo huhitaji kutumia kila siku kwa kukifuata  popote,” alisema.

Alisema shisha ina mchanganyiko mwingi na kwamba  wanaweza kutia maji lakini wakati mwingine maji hayo  yakawa yamewekwa gongo na vilevi vingine mbalimbali.

“Si maji ya kawaida wanakuwa na viroba vimechunwa chunwa vimejazwa humo (kwenye shisha) na mvutaji anapata harufu zote za tumbaku lenyewe, maji yale na hilo gongo lenyewe halafu anapata kilevi mchanganyiko,” alisema.

Waziri mkuu Majaliwa alisema mtu anapotumia kilevi hicho anakuwa anashawishika kila siku kukitumia na kwamba pale anapokikosa husikia mwili unasisimka na hivyo kulazimika kuifuata popote pale ilipo.

“Narudia tena kwa kauli ya Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda-Dar es Salaam) kuipiga marufuku shisha popote inakotumika,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuunga mkono michango inayotolewa na taasisi za dini nchini katika kuhakikisha amani na utulivu nchini vinaimarishwa pamoja na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Naye Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, aliwataka waumini wa dini zote kuishi kwa upendo na mshikamano bila kujali itikadi za dini kwani hilo ndilo agizo la Mwenyezimungu.

Juzi akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani, pamoja na matumizi ya sigara ya shisha mkoani humo kwa kuwa inachanganywa na vilevi vinavyoharibu vijana.

Makonda, alikuwa akihutubia uwanja wa Taifa katika tamasha la vijana lililokuwa limeandaliwa na Upendo Media Group ambapo aliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wavuta shisha hadharani, sigara na mashoga ndani ya siku saba baada ya tamko lake hilo.

Agizo hilo alilisisitiza tena jana kwa wakuu wa wilaya za mkoa huo, ambapo aliwataka wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanazuia na kukomesha matumizi ya shisha.

“Ni marufuku biashara ya shisha kwenye mkoa wangu. Wanaofanya biashara hiyo wote nitawakamata. Mimi ndiye mbabe wa vita…Nina imani watakuwa wamefungasha virago vyao iwe ni kwenye klabu au baa maana humo wanachanganya vitu vingi; bangi na vilevi ambavyo vina madhara. Baada ya siku saba tutakutana (Gereza la Segerea),” alisema.

Alisema utafiti alioufanya chini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), shisha ina madhara makubwa kwa wanaoivuta na wasiovuta kwa kusababisha saratani ya mapafu na koo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha shisha inayovutwa kwa saa moja, ni sawa na kuvuta sigara kati ya 100 na 200.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles