26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

CUF wamtega IGP Mangu

Ernest Mangu
Ernest Mangu

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu kumchukulia hatua za kimaadili, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi kwa kauli yake aliyoitoa Juni 28, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Unguja Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa CUF, Salim Bimani, alisema kauli aliyoitoa DDCI Msangi inapigia chapuo ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea visiwani humo.

“DDCI Msangi Juni 28, mwaka huu aliendeleza utekelezaji wa mkakati wa kulihusisha Jeshi la Polisi katika kukandamiza haki za raia kwa kutoa vitisho kwa wale wanaounga mkono upinzani. Kwa kauli yake hiyo, kumekuwa na vitendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar.

“Kwa mfano  Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkoa wa Kusini Pemba na Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo wananchi watano wasiokuwa na hatia walifyatuliwa risasi za moto na kujeruhiwa  sehemu tofauti za miili yao na bado wengine wanakamatwa na kusingiziwa kesi na wananyimwa dhamana,” alisema.

Bimani alisema ndiyo maana CUF inamtaka IGP Mangu na mamlaka zote zinazohusika ndani ya jeshi hilo kuchukua hatua za kimaadili dhidi ya DCI Msangi na wale wote waliopewa dhamana za juu kulinda raia na mali zao na wakashindwa kufanya hivyo.

“Kuendelea kunyamazia unyama wa aina hii si tu kunachochea kuendelea kwa matukio haya, lakini pia yanatoa mwanya kwa watawala waovu kuendelea kuwatumia watendaji wa aina hii kuratibu na kutekeleza mipango itakayokuwa na athari mbaya kwa nchi yetu,” alisema.

Alisema kauli ya vitisho aliyoitoa Msangi, zinamfanya apoteze heshima na uaminifu wa kulitumikia Jeshi hilo kwani ameweka mbali maadili yake na badala yake anafanya kazi kwa ushabiki.

Bimani alisema kauli aliyoitoa Msangi imelenga kuwatisha wananchi wenye mawazo tafauti na misimamo ya CCM na wafuasi wa CUF Zanzibar na wale wanaounga mkono jitihada za wananchi kupinga uonevu na udhalilishaji unaofanywa na Jeshi hilo dhidi ya raia wasio na hatia.

“Inakwenda kinyume pia na sheria mbalimbali za nchi ikiwamo Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai S. 41 ya CPA No. 7/2004. Kwamba kuwazuia mawakili na wadau wengine wa sheria kutekeleza wajibu wao wa kikatiba na kukandamiza sheria maana yake ni kuidhalilisha fani hiyo na kuwakosesha raia hai ya kupata utetezi kwenye kesi zinazowakabili,” alisema.

Bimani alisema kauli hiyo ya Msangi inadhihirisha usahihi wa kauli na matamko mbalimbali ya CUF kuwa watendaji wengi waliopewa dhamana katika jeshi hilo wamekuwa wakiburuzwa na ushawishi binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles