23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Shikamoo Lowassa

MMGL1424Fredy Azzah na Pendo Fundisha, Mbeya

WATOTO wa mjini wangesema Shikamoo Lowassa. Tunasema hivyo kwani amri ya Jeshi la Polisi nchini inayopiga marufuku maandamano nchi nzima hadi baada ya Uchaguzi Mkuu, haikuweza kufua dafu wakati mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, alipoliteka Jiji la Mbeya kwa saa kadhaa jana.

Yalikuwa ni maandamano makubwa yasiyo rasmi pale wananchi walipojitokeza kumpokea Waziri Mkuu huyo wa zamani, wakati alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Songwe saa 8:20 mchana na kumsindikiza hadi katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe maarufu kama Uwanja wa Dk. Slaa ambako alifanya mkutano wa utambulisho na kushukuru wakazi wa Mbeya waliojitokeza kumdhamini katika harakati zake za kuwania urais.

Polisi walijaribu kuuzuia msafara huo mara tatu bila mafanikio, kwani mbali na waliokuwa wakiusindikiza karibu kila mahali alikokuwa akipita mamia ya wananchi walikuwa wamesimama pembeni mwa barabara wakimshangilia kiongozi huyo.

Utitiri wa polisi ulianza kuonekana nje ya Uwanja wa Ndege wa Songwe, ambako walikuwa wamekaa katika eneo hilo, wengine wakiwa kwenye magari huku wakiwa wamebeba mabomu ya machozi.

Licha ya wananchi waliokuwa wamesimama eneo hilo la uwanja, wengine wakiwa kwenye pikipiki, bajaji na magari kuzuiwa na askari kutoongoza msafara wa Lowassa kama ilivyozoeleka kwenye misafara mingi ya wanasiasa, hata hivyo hilo lilishindikana.

Jaribio hilo la kuzuia wafuasi hao wa Lowassa aliyekuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mgombea Mwenza, Juma Haji Duni, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa NLD, Emanuel Makaidi, lilionekana kutozaa matunda kwani wale wenye pikipiki waliufuata nyuma msafara huo mara baada tu ya kuingia katika barabara ya Mbeya –Tunduma.

Awali ndani ya uwanja wa ndege, yaliruhusiwa kuingia takribani magari 20, ambayo yalipangwa kuwa kwenye msafara huo ili utembee haraka na kufika Mbeya mjini mapema.

Baada ya pikipiki na magari yaliyokuwa nje ya uwanja huo kufuata nyuma msafara huo na kufanya uwe na takribani magari 100 na pikipiki zaidi ya 100, ulipofika eneo la Ifisi, polisi waliruhusu magari ya viongozi kupita na kisha kufunga barabara kwa magari mawili yaliyokatisha katikati ya barabara hivyo kufanya wafuasi wengi kubaki nyuma.

Magari yaliyofunga barabara hiyo yaliyokuwa yamebeba askari wenye mabomu ya machozi na bunduki, yalionekana kushindwa kudhibiti umati huo kwani waliokuwa na pikipiki walianza kupenya na kufanikiwa kupita katika mashamba na kuufuata msafara.

Baada ya muda magari yaliyozuiwa pia nayo yalifuata na msafara ukaendelea kuwa na msururu mrefu wa magari, pikipiki, baiskeli na bajaji huku watu wengine wakitembea kwa miguu.

Msafara huo ulipofika Mbalizi, wananchi waliuzuia tena wakitaka awasalimie na baada ya kufanya hivyo walishangilia kwa nguvu huku wengine wakiimba, ‘Rais, Rais.’

Kutokana na kusimamishwa kila mara, msafara ulifika Iyunga saa 9:36 ambapo pia ulisimamishwa na mamia ya wananchi ambao walijipanga barabarani. Hali hiyo ilijitokeza karibu njia yote hasa maeneo yenye shughuli za kibiashara.

Wakati wote tangu msafara ulipotoka Uwanja wa Songwe mpaka Uwanja wa Ruandanzovwe ulipofanyika mkutano ambako wananchi walilazimika kumsubiri Lowassa kwa takribani saa nane huku wengine wakizimia kwa kukosa hewa kutokana na uwingi wa watu, askari polisi walikuwa wakiufuata wakiwa na magari matatu ambayo yalikuwa yakitumika kutawanya wananchi ili utembee haraka.

Mbali na magari hayo, kulikuwa na vijana wa kikosi cha ulinzi cha Chadema maarufu kama Red Brigade waliojikinga na mavazi maalumu kwenye viwiko na magoti ambao baadhi walikuwa kwenye magari mawili ya wazi huku wengine wakitembea kwa miguu kujaribu kuwatawanya wananchi ili msafara huo utembee.

Licha ya juhudi zote hizo, msafara huo uliwasili uwanjani hapo saa 10:15, zikiwa zimetumika takribani saa tatu  badala ya nusu saa kutembea umbali wa kilomita 21.

Baada ya mkutano mamia ya wananchi walimsindikiza pia Lowassa, huku magari ya polisi yakiwa yanamfuata kwa nyuma.

Leo kiongozi huyo anatarajiwa kufanya mkutano mwingine jijini Arusha.

 

LOWASSA

Baada ya kukaribishwa na mgombea mwenza, Duni Haji, Lowassa alisema amefarijika kwa mapokezi makubwa na kuwashukuru wadhamini waliomdhamini katika safari yake ya kuusaka urais.

Alisema mara ya mwisho kwenda Mbeya alikuwa CCM akiomba wadhamini na kulikuwa na umati mkubwa wa wananchi uliojitokeza.

Alisema kutokana na umati huo, mahasimu wake wa kisiasa walisema amehonga watu hao.

“Sasa niulize hapa, kuna mtu amepewa hela?” Alihoji Lowassa huku baadhi ya wananchi wakiitika “haongwi mtu hapa.”

Baada ya kauli hiyo, Lowassa alisema: “Asanteni sana, walie tu, hawatuwezi.”

Lowassa alisema akipata ridhaa ya kuwa rais, ahadi yake kwa wananchi wa Mbeya ni kuufanya mkoa huo kuwa wa kibiashara.

“Nina ndoto na Mbeya, nataka kuugeuza Mbeya uwe mji wa kimataifa, uwe kama Nairobi. Nitaanza na Uwanja wa Songwe, ndege kutoka nchi jirani za Zambia na DRC zije kuanzia safari zao hapa,” alisema.

Kadhalika, alisema kutokana na idadi kubwa ya vijana aliyoiona; ataunda Serikali rafiki kwa masikini hasa waendesha bodaboda, mama ntilie na wamachinga.

Kuhusu walimu, wakulima alisema ataunda Serikali rafiki na kwamba mtu atakayefanya uzembe atamuweka pembeni.

Alisema anataka watu wafanye kazi saa 24 ili kuhakikisha uchumi unakuwa na maendeleo yanapatikana kwa haraka.

Alisema lengo lake la kuwania nafasi hiyo ni kufanyakazi na sio kufanya mchezo.

Hata hivyo, alisema wananchi wote wenye sifa za kupigakura wanapaswa kwenda kupigakura na kuzilinda ili wahakikishe ushindi.

Wananchi walipomtaka kuzungumzia suala la polisi kuzuia msafara na kuzonga wananchi, alisema wapo wengi wanataka mabadiliko lakini baadhi yao wanawarudisha nyuma.

 

MBOWE

Mbowe alisema wanatarajia kuwa na uchaguzi huru na wa haki, lakini akasema wanataka daftari la kudumu la wapiga kura lifanyiwe uhakiki kwa uwazi.

Alisema anataka iundwe tume shirikishi itakayojumuisha vyama vya upinzani ili kuona mchakato mzima wa kuhakiki daftari hilo.

Alisema tume ya uchaguzi inaundwa na maofisa wa Serikali ya CCM hivyo ni vyema kukawa na ushirikishwaji kuliko ilivyo sasa ambapo habari za tume wanazipata kwenye vyombo vya habari.

Alisema pia, anataka vituo vya kufanya uhakiki wa daftari hilo viwe vingi na kuwe na muda wa kutosha ili wananchi waweze kuhakiki majina yao.

“Sasa hivi wanataka mambo yaende haraka ili watu wengi wasiweze kupiga kura, kama walichelewa kuandikisha watu ni makosa yao,” alisema.

 

SUGU

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Chadema Nyanda za Juu Kusini, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alisema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kumlaki Lowassa ni gharika na kusema yeyote atakayejaribu kufunga goli la mkono Oktoba 25, atakiona cha moto.

Alisema wamepata taarifa kuwa kuna kadi zaidi ya 3,000 za wapigakura ambazo zimeingia jijini Mbeya kinyemela.

 

MAKADA CCM WAHAMIA CHADEMA

Katika hatua nyingine, waliowahi kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, walitumia mkutano huo wa Lowassa kutangaza kujiunga na Chadema.

Wabunge hao ni pamoja na yule wa Mbarali, Modestus Kilufi, Luckson Mwanjale (Mbeya Vijijini) na mbunge wa Lupa ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa na waziri kwa nyakati tofauti, Njela Kasika.

Wakizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Mbeya, makada hao walisema CCM ni chama cha wala rushwa, wezi na wasiopenda haki na ndiyo maana wameamua kuhamia Chadema.

“CCM ni gari bovu, limechakaa hakuna sababu ya kuendelea na safari. Tumeshuka ili tuendelee na gari la uhakika,” alisema Kilufi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles