26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Nape awapongeza Dk. Slaa, Lipumba

napeNA EVANS MAGEGE

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye, amewafananisha viongozi waliokihama chama hicho na oili chafu.

Pia aliwapongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu ‘aliyepumzishwa’ wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, kuwa wamejitambua kisiasa kwa kujitenga na oili hiyo inayomiminwa ndani ya injini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo za CCM zilizopo Lumumba, Dar es Salaam jana, alisema uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, ni sawa na oili chafu iliyomwagwa kutoka katika injini ya gari ili kuiepusha isiharibike.

Alisema uamuzi wa makada hao kujiondoa ndani ya CCM unatokana na sababu binafsi na kubwa ni kumfuata swahiba wao, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekatwa jina lake katika mchakato wa kuomba ridhaa ya kugombea urais.

Akizungumzia sababu nyingine iliyomsukuma Mgeja kujiunga na Chadema, Nape alisema inatokana na hasira, baada ya binti yake kushindwa katika kura ya maoni ya kumpata mbunge wa viti maalumu kupitia Mkoa wa Shinyanga.

“Huyu Mgeja alikuwa na binti yake aliyekuwa anawania nafasi za ubunge wa viti maalumu mkoani Shinyanga, kwa bahati mbaya binti huyo kura zake hazikutosha katika matokeo ya kura za maoni.

“Baada ya matokeo hayo, Mgeja alitumia nafasi yake ya uenyekiti kumshawishi katibu mkuu abadili matokeo, lakini ombi lake likakataliwa, hivyo akaamua kuondoka ndani ya CCM,” alisema Nape.

Mbali na Mgeja, pia alizungumzia uamuzi kama huo uliofanywa na Guninita kuwa alishindwa vibaya katika kura za maoni za kupata mgombea ubunge wa Jimbo la Kilombero.

“Huyu Guninita naye aliangushwa vibaya na kijana wa miaka 32 tu katika kura za maoni za kupata mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Kilombero, alianzia CCM, akaenda Chadema, akarudi CCM, amekwenda Chadema.

“Injini ya CCM inaendelea kujisafisha, hawa akina Mgeja na Guninita ni sehemu ya oili chafu tunayoendelea kuimwaga ndani ya CCM, walitoka, wanaendelea kutoka, lakini bado ni wachache sana, CCM ina wanachama wanaokaribia milioni nane, kwa hiyo wao si lolote kwa ushindi wa CCM mwaka huu,” alisema Nape.

 Katika hatua nyingine, alisema CCM haijahusika na mpango wowote wa kumshawishi Profesa Lipumba na Dk. Slaa kujiondoa ndani ya umoja huo.

“Profesa Lipumba na Dk. Slaa ni watu wanaojitambua, wanastahili pongezi kwa hilo kwa sababu hawakukubali kuchafuliwa na oili chafu, haiwezekani mtu anunue chama kama ananunua suruali dukani na wakati kulikuwa na watu waliojiandaa siku  nyingi kwa mbio za urais,” alisema Nape.

Alisema mambo yaliyotokea Ukawa hayahitaji kutafuta mchawi kutoka nje kwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, ndiye aliyekiuza chama chake na Ukawa kwa ujumla kwa Lowassa.

Profesa Lipumba na Dk. Slaa kila mmoja alijitenga na harakati za kisiasa za Ukawa siku chache baada ya Lowassa kujiunga na  Chadema, ikiwa ni hatua ya kumteua moja kwa moja kuwa mgombea urais wa umoja huo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Dk. Slaa alitangulia kujitenga na harakati hizo kwa kususia kazi yake ndani ya Chadema, ikiwamo kutofika ofisini tangu chama chake kimpokee Lowassa na Mbowe alikaririwa akisema yupo mapumzikoni.

Kwa upande wake, Profesa Lipumba alijiondoa siku chache baada ya Lowassa kupitishwa kuwa mgombea kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari Agosti 6, mwaka huu na kuwaeleza dhamira yake ya kung’atuka inatokana na nafsi yake kumsuta kwamba mgombea urais aliyepitishwa na Ukawa haendani na misingi ya umoja huo.

 

LAPTOP ZA MAGUFULI

Katika hatua nyingine, Nape alikanusha  uvumi unaoenezwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, ametoa ahadi ya kugawa kompyuta mpakato (laptop) kwa walimu nchi nzima.

Alisema taarifa hizo ni uzushi mkubwa unaoenezwa ili kuaminisha wananchi kuwa CCM imeanza kampeni kinyume cha sheria.

“Hizi taarifa si za kweli na kwamba Ilani ya chama tumeipitisha jana jioni na itazinduliwa Agosti 23, wamezusha mambo wasiyoyajua wala kuyafahamu, wasubiri Ilani izinduliwe ili wapate hoja za kuongea,” alisema Nape.

Katikati ya wiki hii, gazeti moja (si MTANZANIA) lilichapisha habari iliyodai kuwa Dk. Magufuli ana mpango wa kuwagawia walimu nchini kote kompyuta hizo.

Hoja hiyo ilizua mitazamo tofauti, huku malimbikizo ya madai ya walimu, nishati ya umeme na mazingira mabovu ya ufundishaji zikiibuliwa na wadau wa elimu kuwa mpango huo si sahihi.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles