NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu kuhusiana na ugonjwa unaomsumbua.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Eligaesha alisema Shigella alifikishwa hospitalini hapo jana jioni akiwa katika hali mbaya.
“Siwezi kueleza anasumbuliwa na ugonjwa gani, hiyo ni siri ya mgonjwa na daktari wake lakini ni kweli tumempokea mkuu huyo wa mkoa na amelazwa katika moja ya wodi ya Sewahaji namba 18 hapa Muhimbili.
“Tulimpokea jana jioni akiwa katika hali mbaya, madaktari wetu wamejitahidi kumpatia matibabu na sasa anaendelea vizuri,” alisema.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa mkuu huyo wa mkoa, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alilieleza MTANZANIA kuwa Shigella alianza kujisikia vibaya akiwa katika ziara ya kazi wilayani Korogwe akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama.
“Shigella akiwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama wilayani Korogwe alianza kusikia hali tofauti baada ya kumaliza kula chakula, ghafla alijikia mwili kuishiwa nguvu na aliamua kunywa maji mengi akidhani ni hali ya kawaida.
“Akiwa nyumbani alimpigia simu daktari wake simu ambaye alifika na kumpatia dawa za kuzuia kutapika na kuharisha. Hata hivyo ilipofika jana (juzi) aliishiwa nguvu hivyo kulazimika kumpeleka Muhimbili kwa sababu ni Hospitali kubwa. Tunashukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema.