Na Sheila Katikula, Mwanza
Wazazi na Walezi ambao ni waamini na wasio waamini wa dini ya kiislamu Mkoani Mwanza wameshauriwa kuwapeleka watoto wao kwenye vyuo vya dini( MADRASA)ili waweze kujifunza maadili ya kidini na kupunguza mmomonyoko wa maadili ndani ya Jamii.
Wito huo umetolewa na Shehe wa msikiti wa Ibaadh, Nuhu Mousa kwenye mashindano ya kusoma Qur’an yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Istiqaama yalikutanisha vyuo mbalimbali vya madrasa jijini hapa.
Mousa alisema ni vema walezi na wazazi kuona umuhimu wa kuwasomesha watoto wao masomo ya dini na ya dunia ili waweze kumtambua Mwenyezi Mungu kwani kuishi bila dini ni sawa na mnyama.
Alisema kila mzazi anawajibu wa kulea watoto wao kwa kuwafundisha maadili ya dini sanjari na kuwahamasisha kupenda kusoma vitabu vya mwenyezi mungu pindi wanapotoka shuleni.
“Inasikitisha kuona mtu anaishi kama mnyama, kuna baadhi ya familia hawaoni umuhimu wa kuwapeleka watoto wao kusoma mambo ya dini, kufanya hivyo ni kosa, kila mzazi anawajibu wa kujitambua yeye ni nani na kwa nini yupo duniani, ukujiuliza hivyo lazima utampeleka akajifunze dini yake,” alihimiza Mousa.
Kwa upande wake mwalimu wa madrasa ya Ilemela, Ibrahim Ramadhani alisema kuwa mtoto anapopata maadili ya dini anakuwa katika misingi bora wa kupata mwelekeo wa familia yenye nidhamu kwenye jamii.
“Mashindano haya yamekutanisha watoto 52 kutoka kwenye vyuo vya dini (madrasa), nane vya jijini hapa kwani lengo letu ni kuhakikisha watoto wanatambua dini yao kwa undani zaidi kwa kuwa tunaimani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo,”alisema Ramadhani.