25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

SHEIKH PONDA AIBWAGA JAMHURI MAHAKAMANI

Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetupilia mbali maombi ya rufaa yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda.

Katika kesi hiyo, Jamhuri ilikata rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro ya kumwachia huru sheikh huyo katika kesi iliyokuwa inamkabili ya kutoa matamshi ya uchochezi.

Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo jana, Jaji wa Mahakama Kuu, Edson Mkasimongwa, alisema kuwa mahakama imemwachia huru Sheikh Ponda kwa sababu hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morogoro haikukosea.

Alisema anaunga mkono uamuzi huo na kumwachia huru Sheikh Ponda kwa sababu hawajakosea katika uamuzi wao katika kesi ya kutoa matamshi ya uchochezi.

“Ninakubaliana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morogoro, kwa sababu hawajakosea katika uamuzi wake, hivyo basi na mimi natupilia mbali rufaa iliyotolewa na upande wa Jamhuri katika kesi ya kutoa matamshi ya uchochezi,” alisema Mkasomongwa.

Jaji Mkasimongwa alisema kuwa upande wa Jamhuri haukupaswa kumshtaki Sheikh Ponda kwa kosa lile lile la kuvunja amri ya Mahakama ya Kisutu, bali walitakiwa kumrudisha katika mahakama hiyo ili imchukulie hatua zaidi.

Sheikh Ponda akiwa katika Mahakama ya Morogoro alipandishwa kizimbani na kudaiwa kuwa Agosti 10, 2013 katika eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, aliwaambia Waislamu wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwa madai kuwa zimeundwa na Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.

Mbali na hili, alidaiwa kuwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao watajitokeza kwao na kujitambulisha kwamba ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.

Anadaiwa kuwa kauli aliyoitoa ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, 2010, ambayo ilimtaka Ponda ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani na kuwa raia mwema.

Shtaka lingine ni kwamba alidaiwa kuwa Agosti 10, 2013 katika eneo la Uwanja wa Ndege, Morogoro, aliwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi hao ni Waislamu.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Juma Nasoro ambaye ni wakili wa Sheikh Ponda, aliunga mkono hukumu hiyo na kudai kuwa mahakama imetenda haki kwa mteja wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles