31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAMLAKA FUKWE KUANZISHWA TANZANIA KUIMARISHA UTALII  

Na LEONARD MANG’OHA


KATIKA mwaka wa fedha 2016/2017, sekta ya utalii ilichangia asilimia 17.5 ya pato la Taifa huku ikiliingizia asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Pia sekta hiyo ilitoa takribani ajira 500,000 za moja kwa moja huku zaidi ya watu wengine milioni moja wakijiajiri katika sekta hii kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii.

Kwa kiasi kikubwa utalii ambao umelipatia Taifa umaarufu ni ule unaohusisha wanyama na baadhi ya vivutio vichache kama vile milima ambayo imejikusanyia umaarufu mkubwa kutokana na uwapo wa Mlima Kilimanjaro ambao ni miongoni mwa milima mitatu mirefu duniani.

Kwa kipindi kirefu shughuli za utalii zimeegemea zaidi ukanda wa Kaskazini mwa nchi ambako zinapatikana mbuga za wanyama za Arusha, Ngorongoro, Manyara, Tarangire na Serengeti ambayo ni ya kwanza kwa ukubwa duniani, pia Mlima Kilimanjaro upo ukanda huo.

Hili limefanya hata watalii wengi wanaotoka nje ya nchi wanapokuja hapa nchini hupenda kwenda huko hivyo kuiaminisha dunia kuwa utalii na  maeneo ya utalii hapa nchini hupatikana huko tu.

Historia inaonesha kuwa siku za nyuma maeneo ya Mkoa wa Iringa yalikuwa kitovu cha shughuli za kitalii ambapo hata wageni mbalimbali walielekea huko kwa mapumziko, lakini sasa hali ni tofauti si wengi wanaovutiwa kwenda ilipoachwa kutangazwa.

Kwa kuiona hatari hiyo katika mwaka huu wa fedha, Serikali ina mpango wa kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini ambako kuna vivutio vingi vya utalii lakini pamekuwapo idadi ndogo ya watalii wanaotembelea ukanda huo ukilinganisha na ukanda wa Kaskazini. Iringa ndio mji ulioteuliwa kuwa makao makuu ya utalii Kusini mwa nchi.

Katika jitihada za kutekeleza hilo, Serikali imepokea Dola za Marekani milioni 150, kupitia mradi unaofahamika kama Resilient Natural Resource for Tourism and Growth (REGROW), unaoanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Lengo la mradi huu ni kuongeza ubora wa vivutio vya utalii kwa kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi, usimamizi wa maliasili na kuongeza faida kiuchumi kwa jamii zinazoishi kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi hizo.

Vile vile mpango huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi na pato la Taifa.

Katika hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akiahirisha Bunge Novemba mwaka huu, anasema Serikali inaimarisha matangazo ya vivutio kwa kuwaruhusu wakuu wa mamlaka za mapori kuanza kutangaza vivutio vilivyopo katika mamlaka zao kazi watakayoifanya kwa ushirikiano na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ambayo ndiyo wenye jukumu la kutangaza utalii nchini.

Jambo la kufurahisha katika hotuba ya Waziri Mkuu ni kuukumbuka utalii wa fukwe ambao haujachangia kwenye pato la Taifa licha ya kuwa na eneo kubwa la ufukwe kote Bara na Visiwani, ikilinganishwa na nchi nyingi duniani.

Majaliwa alimwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuanzisha mamlaka ya fukwe za bahari na maziwa ili kutangaza utalii na kuendeleza fukwe zote ambazo hazina shughuli za kitalii.

“Fukwe za bahari ni eneo mojawapo ambalo likiendelezwa vizuri, linaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi,” anasema Majaliwa.

Uamuzi huu wa Serikali unastahili kupongezwa japo umekuja kwa kuchelewa kwa sababu ulipaswa kutazamwa mapema zaidi ili kulinufaisha Taifa tofauti na sasa ambapo ni watu wachache tu wanaofaidika na uwepo wa eneo hilo ambalo nchi nyingi Afrika na duniani kwa ujumla zinalikosa.

Baadhi ya nchi kama vile Brazil, Ufilipino na Uturuki zimekuwa zikijikusanyia mabilioni ya Dola za Marekani kila mwaka kupitia utalii wa fukwe.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zinaonesha kuwa sekta ya utalii nchini Ufiilipino ilichangia asilimia 8.6 katika pato la taifa (GDP) mwaka 2016 huku ikitoa ajira zaidi ya milioni tano.

Sekta hiyo pekee imevutia uwekezaji wa kigeni kiasi cha Dola za Marekani bilioni 3.7 (zaidi ya Sh trilioni 8.2) zilizotokana na ujenzi wa mahoteli na sehemu za mapumziko (resorts).

Mwezi Mei mwaka huu pekee sekta hiyo iliwezesha kuvutia watalii wa kigeni wapatao 532,757, sawa na ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na watalii 445,449 mwaka 2016.

Lakini inaelezwa kuwa watalii wengi wanaotembelea nchi hiyo huvutiwa zaidi na utalii wa fukwe ambazo ndizo zinazovutia watalii wengi.

Fukwe hizo ni pamoja na ule unaopatikana katika kisiwa cha Boracay (Aklan) kinachopatikana Kusini mwa mji wa Manila kikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 315.

Kisiwa hiki ni kituo maarufu cha utalii nchini Ufilipino kikiwa na resorts zaidi ya hoteli 350 za kifahari na zile za watalii wa kipato cha kati.

Kisiwa hiki kimeweka mazingira mazuri yanayolenga kumvutia kila mmoja anayetembelea eneo hilo ikiwa ni pamoja na maeneo ya michezo ya majini, kuogelea, kumbi za burudani na disco, bar na migahawa.

Maeneo mengine yenye visiwa fukwe za kuvutia ni pamoja na kisiwa cha El Nido (Pawalan),  Puerto Galera (Oriental Mindoro)  Samal, (Davao Cit)  Panglao (Bohol).

Fukwe kama vile Patara, Bodrum Peninsula, Ölüdeniz lagoon, Kalkan na Antalya zimekuwa chanzo kikuu cha mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini Uturuki, nchi ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa ikivutia idadi kubwa ya watalii kabla ya kuathiriwa na tishio la mapinduzi kutoka kwa kundi la PKK linalopinga utawala wa Rais Recep Tayyp Edorgan.

Patara ndio ufukwe mrefu zaidi nchini Uturuki na umekuwa ukifahamika zaidi kwa mchanga wake mweupe huku ukiwa ndio ufukwe mzuri zaidi nchini,  vile vile umekuwa kivutio kwa watoto kutokana na joto lake.

Ufukwe wa Kalkan ulikuwa kijiji maarufu cha uvuvi hadi kufikia miaka ya 1920 Chini ya taifa la Ugiriki, huku ufukwe wa Antalya ukijikusanyia sifa ya kuvutia watu wengi ambao hufika katika eneo hilo kufurahia mandhari asilia ya fukwe za bahari ya Mediterranean na burudani nyingine.

Mwaka 2014 taifa hilo lilivutia watalii wapatao milioni 42 ambapo lilikuwa la sita kwa kuvutia watalii wengi duniani, idadi hiyo ilishuka hadi milioni 36 mwaka uliofuata na iliendelea kushuka zaidi hadi milioni 25 mwaka jana.

Nchi nyingine ambayo imejipatia umaarufu mkubwa kwa utalii wa fukwe ni Brazil ikijivunia kuwa na fukwe nzuri na ndefu duniani  ambazo zinapatikana katika miji ya Rio de Janeiro, El Salvador, Natal, Recife na Fortaleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles