23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAKULIMA WAZINGATIE USALAMA CHAKULA, SUMU KUVU

Na JANETH MUSHI-ARUSHA


SUMU kuvu maarufu kama aflatoxin, ni aina ya sumu ambayo inatengenezwa na ukungu katika mazao ya  nafaka kama mahindi au karanga  ambayo haijahifadhiwa katika sehemu ambayo kitaalamu haijakidhi vigezo au masharti ya kuhifadhi nafaka.

Sumu kuvu pia inaweza kujitengeneza katika nafaka ambazo hazijavunwa  shambani ikiwemo mahindi ambayo hayatavunwa baada ya kukauka halafu mvua au unyevu  mkubwa kutanda shambani unaweza kusababisha baadhi ya mahindi kuoza na kutengeneza ukungu ambao unakuwa na sumu kuvu.

Sababu nyingine zinazoweza kusababisha sumu kuvu kwenye mazao ya nafaka ni pamoja na kuhifadhiwa kwa nafaka sehemu yenye unyevunyevu na joto katika stoo au maghala au kuweka nafaka moja kwa moja katika sakafu au ardhini ambapo kunaweza kusababisha unyevu kuanza kujijenga na kutengeneza ukungu ambao baadaye huzalisha sumu kuvu katika mazao.

Mratibu wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) chini ya mradi wa Ubia wa Kilimo Tanzania (TAP), Hendry Mziray, anawataka wakulima kuzingatia usalama wa chakula ikiwa ni pamoja na kununua pembejeo kwa mawakala ili kuepuka dawa zisizokuwa na uhakika.

Akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Lokisale, wilayani Monduli hivi karibuni anasema wakulima wanapaswa kuhakikisha wananunua pembejeo kwa mawakala waliosajiliwa ili kuepuka dawa zisizokuwa na uhakika ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ikiwemo sumu kuvu inayosababishwa na mazao kutokukauka sawasawa.

“Nunueni pembejeo kwa mawakala waliosajiliwa kwani baadhi ya mawakala wanauza dawa ambazo hazifanyi kazi ikiwemo unga wa muhogo na kudanganya wakulima kuwa hiyo ni dawa ya kuulia wadudu na  zingatieni njia
salama za kuhifadhi mazao ili kuzuia wadudu pamoja na magonjwa ikiwemo sumu kuvu,” anasema na kuongeza:

“Utafiti uliowahi kufanywa umeonesha kati ya asilimia 20 hadi 30 ya mavuno ya mkulima hupotea kutokana na uhifadhi ambao huchangia sumu kuvu katika nafaka baraza tunahimiza wakulima mzingatie kanuni bora
za kilimo kuanzia kutafuta mbegu, kuandaa shamba, viuatilifu na kuhifadhi mazao kwani usalama wa chakula ni muhimu.”

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Kaskazini, Didas Mutabingwa, anasema wameanza kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa za chakula hasa wazalishaji wadogo namna ya kuzalisha bidhaa zao kuhakikisha  ziko salama kwa watumiaji  na zina ubora.

Anasema katika mafunzo hayo makundi mbalimbali ya wajasiriamali hupatiwa  mafunzo hayo ambapo hushirikiana na Shirika la viwanda vidogo  vidogo nchini (SIDO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika
kutoa elimu hiyo.

“Tunawasaidia kuwaelekeza namna ya kuzalisha katika viwanda vidogo vidogo na kuvikagua kama vinakidhi ubora na usalama wa watumiaji,” anasema Mutabingwa.

Meneja huyo anasema katika kuisaidia Serikali kutekeleza azma ya uchumi wa viwanda, TFDA wamekuja na mkakati wa kuhakikisha wajasiriamali wadogo bidhaa zao zinasajiliwa ambapo  Mamlaka hiyo imeingia makubaliano na TBS.

Anafafanua kuwa wajasiriamali hao wataenda SIDO ambapo watatambuliwa  na kusajiliwa kabla ya kwenda TBS kwa ajili ya kupimiwa bure  bidhaa zao  wanazozalisha na majibu ya maabara yakishatoka wakionekana kukidhi vigezo bidhaa zao zitasajiliwa na Mamlaka hiyo.

“Huu utaratibu ni tofauti na wa zamani, ambapo walikuwa wanakuja kwetu wanasajili na kupima, wakienda TBS wanapima tena na usajili wa zamani ulikuwa Dola za Marekani 300 ila sasa hivi ni Sh 50,000 kwa bidhaa,” anasema na kuongeza:

“Utaratibu huu utawaondolea usumbufu wajasiriamali na tutaweza kusajili bidhaa nyingi zenye ubora ambazo zitaweza  kutambulika katika masoko ya nje. Tutakuwa tunawasimamia na kukagua bidhaa zao mara kwa
mara ili wazalishe bidhaa salama na bora kwa matumizi ya binadamu.”

Akizungumzia tatizo la sumu kuvu katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Mutabingwa anasema tatizo hilo lipo katika Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara ambapo tatizo limejitokeza na walaji kuathirika na sumu hiyo hususani katika mahindi.
Anasema TFDA wanatoa elimu kwa wakulima na wananchi waelewe madhara ya sumu kuvu na namna ya kutambua mahindi au mazao mengine ya nafaka yaliyoathirika ikiwemo karanga na kuwa hushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kutoa elimu na Wizara ya Afya katika kusimamia.

Kuhusu udhibiti wa sumukuvu katika mazao ya nafaka anasema wamekuwa wakiwashauri wakulima kutumia mbegu kinzani dhidi ya fangasi wanaotoa sumu kuvu, kuzingatia mbinu bora za uhifadhi wa mazao kulingana na  ushauri wa wataalamu.

“Tunawashauri wakulima kuepuka kuhifadhi vyakula vilivyoharibika kwa mfano kutobolewa na  wadudu, kuhakikisha mazao yaliyovunwa  hayanyeshewi na mvua au kumwagikiwa na maji, kuzuia wadudu na wanyama waharibifu wakati wa uanikaji na uhifadhi wa mazao,” anasema.
Mutabingwa anawatahadharisha wakulima kuwa wasitumie mazao yaliyoathirika na sumu kuvu kwani sumu hiyo haiwezi kuisha hata kama nafaka hiyo itapikwa kwa muda mrefu.
“Wakati wa mlipuko ni vema wakakoboa mahindi ili kupunguza uwezekano wa sumu kuvu katika mahindi ambayo hayajaathirika, licha ya kupunguza virutubisho lakini yanakuwa salama zaidi. Walaji wa ugali wa dona wako kwenye hatari iwapo mahindi hayajachambuliwa vizuri na yaliathirika na sumu kuvu, hivyo wakulima wanapaswa kuzingatia usalama wa chakula kwa ajili ya afya za walaji,” anafafanua  na kuongeza:

“Wakulima wanapaswa kujenga maghala yanayoruhusu mzunguko wa hewa ili kusitokee uvundo au unyevu, kunyunyuzia dawa kwa kuzingatia ushauri wa watalaamu, kutumia dawa zinazodhibiti sumu kuvu wakati wa usindikaji wa vyakula.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles