*Azawadia wachezaji viwanja Dodoma
*Mtoto wa miaka 7 afariki dunia kwa kukanyagwa Uwanja wa Taifa
SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amekutana na wachezaji, viongozi wa benchi la ufundi na wajumbe wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde na kuwapongeza, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda ‘Cranes’.
Stars ilivuna ushindi huo ulioiwezesha kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, zitakazofanyika kuanzia Juni mwaka huu nchini Misri, katika mchezo wa marudiano uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli, alisema kabla ya ushindi wa juzi wa Taifa Stars, alikuwa amevunjika moyo baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wake dhidi ya Lesotho.
“Niseme wazi, nilikuwa nisiite timu yoyote Ikulu, tulipofungwa na Lesotho nilivunjika moyo maana waziri (Harrison Mwakyembe) aliniambia nisiwe na hofu kila kitu kiko vizuri. Tangu wakati huo sijawahi kuzungumza naye wala naibu waziri, taifa lenye watu milioni 55 linafungwa na taifa lenye watu milioni mbili?” alihoji Magufuli.
“Lakini Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan) na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), walinipa moyo.”
Alisema kama wachezaji wa Taifa Stars watadumisha viwango walivyovionyesha katika mchezo dhidi ya Uganda, ana imani kikosi hicho kitafanya vizuri pia katika fainali za Afcon nchini Misri.
Awamwagia viwanja
Rais Magufuli alitangaza kuwazawadia wachezaji wa Taifa Stars na viongozi wa benchi la ufundi viwanja vya makazi jijini Dodoma kama shukrani zake kwa kufanikisha ushindi huo.
Mbali ya wachezaji hao, Rais Magufuli, pia alimpongeza na kumzawadia kiwanja bondia, Hassan Mwakinyo, ambaye alialikwa katika hafla hiyo.
Mwakinyo alifanikiwa kushinda kwa KO pambano lake dhidi ya bondia raia wa Argentima, Sergio Gonzalez, lililofanyika Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Mikutano wa KICC, Nairobi nchini Kenya.
Wengine waliokutana na bahati hiyo ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga na staa wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino, ambao pia Rais Magufuli alitangaza kuwapatia viwanja.
Tenga na Tino walikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki kwa mara ya kwanza fainali za mataifa ya Afrika zilizofanyika mwaka 1980 nchini Nigeria.
Mbali ya kumpatia kiwanja, Rais Magufuli, alimpa Tino ambaye pia alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde Sh milioni tano.
Aibeba Afcon ya vijana
Rais Magufuli alisema atatoa Sh bilioni moja kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili zitumike kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17 yaliyopangwa kuanzia Aprili 14 hapa nchini.
“Kuna mashindano makubwa ya Afrika yanafanyika hapa na nikaona mwelekeo ni ule ule kuombwa hela, ingawaje mimi sikuuliza na sikutaka kuuliza kama jana mlikata tiketi nyingi uwezo wa uwanja ni watu 63,000 na zaidi ya nusu walikuwa nje nao walikata tiketi zimekusanywa kiasi gani, hilo nalo siulizi.
“Hata ukienda uwanjani kuna mambo mengi hayajafanyika vizuri, ukarabati hauko vizuri, mtu wa kawaida anaweza kujiuliza hizo asilimia zinazokatwa katika matumizi ya uwanja zinatumika kufanya nini, je, wizara inafanya nini, je, viongozi wa wizara huwa hawaendi pale uwanjani kuuona, nao wanataka waundiwe kamati, hayo ni maswali ambayo Watanzania wanaweza kujiuliza.
“Watanzania wanaweza kujiuliza, kama watu wengi walikatiwa tiketi ina maana za Tanzania huwa hazina ukomo, je, suala la ulinzi wameliangaliaje watu wa wizara, je, kama watu laki mbili wangeingia na uwanja uwezo ni watu 63,000, je, kama ungeanguka ni watu wangapi wangekufa?
“Tunaweza tukawa tunashangilia mashindano ya Afcon yanafanyika hapa, lakini je, tumejiandaaje, naipongeza TFF kwa kuanza kupata zile fedha ambazo zilikuwa zimekataliwa kutokana na matumizi mabaya, ni mwelekeo mzuri,” alisema Rais Magufuli.
Wakati huo huo pongezi zimeendelea kumiminika kwa wachezaji na viongozi wa kikosi cha Taifa Stars, baada ya ushindi wao huo.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema ushindi huo ni wa kihistoria na kwamba umeiletea nchi heshima.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jana ilipunguza gharama za vipimo vya ECHO na ECG kutoka Sh 120,000 hadi 25,000 kwa wagonjwa waliokwenda kupatiwa huduma hiyo, kama sehemu ya kusherehekea ushindi wa Stars.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia taarifa yake iliyotolewa na Mkuu wake wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, kimewapongeza wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi la Taifa Stars kwa ushindi huo na kutaka utumike kama kichocheo cha kufanya vizuri katika fainali cha Afcon.
Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alipongeza ushindi huo na kuongeza kuwa na mwendelezo wa utekelezaji wa ilani ya chama hicho.