21.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Kigogo Wizara ya Mifugo kortini kwa rushwa

CLARA MATIMO- MWANZA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, imewafikisha mahakamani watuhumiwa watano akiwamo Ofisa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Judith Mgaya (48)  kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni tano.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Emmanuel Stenga,  ilieleza kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kwa nyakati na maeneo tofauti Februari mwaka huu.

Stenga alisema Mgaya ambaye pia ni Mkuu wa Oparesheni ya Uvuvi haramu Wilaya ya Ukerewe mkoani hapa, alifikishwa mahakamani hapo Machi 12 na kufunguliwa kesi namba 1 ya mwaka 2019, kujibu tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 5.1 kutoka kwa mfanyabiashara Thobias Kaswahili.

Inaelezwa Februari 2, boti tatu za mfanyabiashara Kaswahili zilikamatwa katika operesheni ya uvuvi haramu kwa kosa la kukutwa na nyavu chini ya nchi sita ambapo mfanyabiashara huyo alitozwa faini ya Sh 900,000 na kupatiwa stakabadhi,  lakini Februari 3 alifika ofisini kwa mtuhumiwa ili ampatie injini zake kama alivyoelekezwa na maofisa uvuvi baada ya kulipa faini.

“Baada ya mfanyabiashara huyo kufika ofisini hapo alimkuta mtuhumiwa ambaye alimtaka ampe Sh milioni 5.1 ndipo amrudishie nyavu hizo, ambapo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa  namba  11 ya mwaka 2007….Februari 7, mwaka huu mfanyabiashara huyo alimpelekea mtuhumiwa fedha hizo lakini hakupewa risiti,” ilisema taarifa hiyo.

Baada ya kuona hali haileweki, mfanyabiashara huyo alienda kutoa taarifa Takukuru na baada ya uchunguzi kukamilika mtuhumiwa alifikishwa mahakamani Februari 12, na kusomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Maximillian Kyabona, mbele ya Hakimu Veronica Selemani.

Mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Aprili 2, kesi hiyo itakapotajwa tena kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali.

Katika tukio lingine Stenga alisema Takukuru imewafungulia mashtaka maofisa Afya Sebastian Mazigo (57) na Benjamin Munanga (48) wa wilaya ya Ukerewe  kwa kosa la kuomba na kupokea Rushwa ya Sh 440,000  kutoka kwa wafanyabiashara 13 tofauti.

Katika upande mwingine, Takukuru Wilaya ya Kwimba iliwafungulia mashtaka katika Mahakama ya Wilaya hiyo, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Izizima B, Lucas Katwiga na Claud Vicent ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa kijiji hicho kwa tuhuma za kushawishi na  kuomba rushwa ya Sh 600,000 ambapo walipokea Sh 400, 000 kutoka kwa Kabula Kabadi.

Alisema viongozi hao walitenda kosa hilo Februari 22, mwaka huu, ambapo Kabadi ana mtoto mtoro shuleni hivyo watuhumiwa hao walimfuata na kumtaka awape kiasi hicho cha fedha ili wasichukue hatua dhidi yake.

Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Jovin Majura, mbele ya Hakimu, Janeth Msaloche na kukana makosa yao na kesi kuhairishwa hadi itakapotajwa tena Machi 27, mwaka huu, pia mtuhumiwa wa kwanza Katwiga yuko nje kwa dhamana na Vicent yuko mahabusu baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,590FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles