25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Sh bil 12 kudhibiti Ukimwi mipakani

Koku David- Dar es salaam

TANZANIA inatarajia kutumia Sh bilioni 12 katika utekelezaji wa programu ya udhibiti Ukimwi mipakani ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwaka Afrika (SADC Cross-border Initiative).

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mratibu wa Programu za Kikanda na Kimataifa wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Renatus Kihongo, alisema SADC kupitia Tacaids ilisaini makubaliano na Tanzania ili kutekeleza programu hiyo katika mipaka ya Tanzania na Malawi (Kasumulu/Songwe) na ule wa Tanzania na Zambia (Tunduma/Nkonde).

Alisema hadi sasa vituo viwili vimeanza kazi na vinaendelea kutoa huduma za Ukimwi na magonjwa mengine kupitia Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Halmashauri ya Wilaya ya Kyela.

“SADC kupitia Mfuko wa Dunia wa Kifua Kikuu, Ukimwi na Maralia (GFATM), imetekeleza programu ya udhibiti Ukimwi mipakani, imesaidia kutoa miongozo mbalimbali, ikiwamo mwongozo wa utoaji huduma kwenye barabara kuu katika vituo vya magari ya mizigo yanayoingia nchini na yale yanayosafiri kwenda nchi za SADC,” alisema Kihongo.

Alisema mwongozo huo umesaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wasafirishaji wa masafa marefu na jamii zinazoishi kwenye vituo hivyo hatarishi kwa maambukizi ya VVU.

Kihongo alisema jumuiya hiyo imewezesha mafunzo mbalimbali  maeneo ya udhibiti kwa wataalamu na viongozi, ambayo yamesaidia kujenga uwezo maeneo ya utafiti, uandaaji wa miradi pamoja na kupata uzoefu wa nchi nyingine katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, Tanzania inashiriki utekelezaji wa Programu ya Uboreshaji wa Biashara na Usafirishaji Kusini mwa Afrika (SATTFF), ambayo inatekelezwa kuanzia Dar es Salaam hadi Durban nchini Afrika Kusini kupitia Malawi, Zambia na Zimbabwe.

“Katika programu hii, utoaji wa mafunzo kwa watoa huduma imeshafanyika na kwamba Tacaids inashughulikia uratibu wa masuala ya Ukimwi, huku vituo 20 vya afya vinavyotoa huduma za Ukimwi vikiendelea kuboreshwa kwa kujenga maabara na CTC, pia taratibu za ununuzi wa mashine za kupima kiwango cha kinga (CD4 count machine) na kiwango cha virusi vinavyosababisha ugonjwa huu mwilini (Viral Load Machines), zikiendelea ikiwa ni pamoja na ujenzi wa chomea taka ukiendelea,” alisema Kihongo.

Alisema programu hiyo inayogharamiwa na Benki ya Dunia, inalenga kuboresha utoaji wa huduma vituo hatarishi (hotspots) vilivyopo barabara kuu ya kuanzia Dar es Salaam hadi Kasumulu (mpaka wa Tanzania na Malawi) na Tunduma (mpaka wa Tanzania na Zambia).

Kihongo alisema kutokana na Tacaids kuwa mratibu wa Ukimwi sekta mtambuka, programu hiyo katika udhibiti inatekelezwa kwa ubia kamilifu wa sekta za Uwakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), sekta binafsi (wakandarasi na mtaalamu mshauri), Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano na wadau wa maendeleo (Benki ya Dunia).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles