* Aagiza waajiri, wakurugenzi na wakuu wa Idara kuusimamia
Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amezindua Mfumo wa Kielektroniki wa tathmini ya hali ya rasilimali watu katika utumishi wa umma huku akiwaagiza Waajiri, Wakurugenzi na wakuu wa Idara kuusimamia mfumo huo.
Ameagiza Wakuu hao wakamilishe zoezi hilo ifikapo Machi 31, mwaka huu ambapo taasisi ambazo hazitakamilisha zitakuwa zimekiuka maelekezo ya Serikali na hatua stahiki zitachuliwa.
Akizungumza leo Machi 24, 2022 wakati wa uzinduzi wa mfumo huo,Waziri Jenista ameagiza Wakuu hao wakamilishe zoezi hilo ifikapo Machi 31, mwaka huu.
Waziri huyo amesema taasisi ambazo hazitakamilisha zoezi hili zitakuwa zimekiuka maelekezo ya serikali na hatua stahiki zitachuliwa.
Amesema Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina majukumu mengi ya Kisera na kiutendaji yanayotekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayolenga kuimarisha usimamizi wa Rasilimaliwatu tangu mtumishi anapoajiriwa mpaka atakapostaafu.
“Nimekuwa nikisisitiza suala hili mara kadhaa kwamba bila kuisimamia vizuri rasilimaliwatu basi hizo rasilimali nyingine zote tulizonazo haziwezi kutuletea maendeleo tunayokusudia.
“Niseme mapema na kwa dhati kabisa kuwa wote tunaona juhudi anazozifanya mama yetu Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwenye Sekta mbalimbali katika kuiletea maendeleo nchi yetu na watu wake.
“Ni jukumu letu sisi Viongozi na Watumishi wote wa Umma kuchapa kazi kwa utalaamu, ubunifu na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa na maono na azma ya Kiongozi Mkuu wa Nchi yetu yanatimia,” amesema Mhagama.
Pia, amewashukuru wataalamu pamoja na wote waliosimamia mpaka mfumo huo kukamilika hivyo jukumu kubwa linabaki katika kutunza, kusimamia na kuulinda mfumo huu ili uweze kufanya kazi iliyokusudiwa ipasavyo.
Waziri Mhagama amesema mara baada ya kusanifiwa na kujengwa kwa Mfumo huo, Ofisi yake iliupeleka kwa Waajiri wote waliopo kwenye Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) ili kuingiza taarifa na takwimu sahihi kuhusu idadi na mgawanyo wa watumishi kulingana na huduma zinazotolewa na taasisi za Umma.
Amesema kwa taasisi zilizo nje ya Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) zilipelekewa nyenzo ya kukusanya taarifa ambazo zitaingizwa kwenye Mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kuchakatwa zaidi.
Amesema mfumo uliozinduliwa utawezesha ukusanyaji, uchakataji na uchambuzi wa taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma.
Aidha, matarajio ya zoezi hili ni kuweka msawazisho wa Watumishi wa Umma katika taasisi za Umma,kwa tathmini iliyopo inabainisha kuwa utoshelevu wa mahitaji ya watumishi kwa taasisi za Umma upo kati ya asilimia 52 hadi 90,hata hivyo, zipo baadhi ya taasisi ambazo zina watumishi wa ziada katika baadhi ya kada.
Katika hatua nyingine,Waziri Mhagama amebainisha Taasisi zilizofanya vizuri na ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye Mfumo.
“Kwa mfano, Taasisi 10 bora zilizofanya vizuri ni pamoja na Shule ya Sheria Tanzania (97%); Tume ya Ushindani (97%); Chuo cha Ardhi Morogoro (97%); Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala (96%).
“Ofisi ya Rais Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (95%); Sekretariet ya Mkoa wa Iringa (95%); Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (95%); Mamlaka ya Serikali Mtandao (95%); Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (95%); na Wakala ya Mafunzo ya Menejimenti ya Elimu (94%),”amesema.
Waziri huyo amesema Mfumo umebainisha Taasisi takribani 94 ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye Mfumo kwa sababu bado zipo chini ya asilimia 50 ya utekelezaji wa zoezi hilo.