24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa utaratibu mpya kukabili corona

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WAKATI watu waliothibitika kuwa na virusi vya ugonjwa wa corona nchini wakifikia 88, Waziri Mkuu Mkuu Kasim Majaliwa, amekemea mikusanyiko inayofanyika kwenye nyumba za ibada kwa kigezo cha kutaka watoto wasikae majumbani kwa vile hawaendi shuleni.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza, vituo 24 ambavyo watu watakaojihisi kuwa na joto kali na mafua makali, wataenda kupimwa na ikibidi kuchukuliwa sampuli zao ili zipelekww maabara kuu ya taifa.

Pia wabunge wameshauri wakati Serikali ikiendelea kukabiliana na janga hilo, ni vyema baa zikafungwa.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Tanzania, duniani walioambukizwa virusi hivyo sasa ni takribani milioni mbili, waliofariki dunia 127,000, huku Marekani ikiongozwa kwa kwa na wagonjwa zaidi ya 600,000 na waliopoteza maisha wakiwa 26,000.

Majaliwa

Jana Majaliwa alikemea mikusanyiko inayofanyika  nyumba za ibada kwa kigezo cha kutaka watoto wasikae majumbani kwa vile hawaendi shuleni.

 “Ninazo taarifa  wameanzisha mfumo wa kupeleka watoto kwenye madarasa ya dini. Tumeruhusu ibada tu, na hizo ibada lazima ziangaliwe ziwe za muda mfupi kadri inavyowezekana. “Tumesisitiza kwenye makanisa au misikiti ambako ibada zinafanyika, waumini wakae kwa kuachiana nafasi,”alisema

Alisema changamoto inajitokeza kwenye makanisa makubwa ambayo yana waumini karibu 3,000. 

“Hayo sasa yatakuwa ni makongamano. Tunaaamini maaskofu na Mufti wataliweka vizuri suala hili,” alisema.

Alisema Serikali haitazuia biashara kwenye masoko, maduka au supermarkets, isipokuwa amewataka wenye biashara hizo wahakikishe wanaweka ndoo za maji na sabuni ili wateja wanawe mikono kabla ya kuingia kupata huduma na wakati wanapotoka kupatiwa huduma hizo. Vilevile, alihimiza wananchi wazingatie kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kutoka kwa mtu mwingine.

Kuhusu mikusanyiko mingine, alisema watu wanapaswa wajizuie kwenda kuzagaa kwenye vituo vya mabasi na kama hawana shughuli za lazima za kufanya huko, basi wabakie majumbani kwao.

Wagonjwa 88 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, jana jioni alitoa taarifa kwa vyombo vya habari, ikionyesha wagonjwa wa corona sasa wamefika 88, huku wanne wakiwa wamefariki dunia.

“Wizara inatoa taarifa ya uwapo wa wagonjwa wagonjwa 29 waliothibitika kuwa na ugonjwa wa corona (COVID 19) nchini. Wagonjwa hawa wote ni Watanzania kati yao 26 wapo Dar es Salaam, wawili wapo Mwanza na mmoja yupo yupo Kilimanjaro.

“Kufikia leo (jana), watu 88 wamepata maambukizi ya COVD 19 nchini kutoka 53 tuliotolea taarifa awali. Ongezeko hilo linajumlisha wagonjwa wapya sita waliotolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar mapema leo (jana). Wagonjwa waliopona ni 11 na vifo nchini ni vinne.

“Serikali inapenda kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kama tunavyowapatia taarifa na elimu mara kwa mara. Katika kipindi hiki ni muhimu kwa wananchi kuepuka misongamano na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima,” ilisema taarifa hiyo.

Zanzibar

Jana pia Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed, alitoa taarifa ya wagonjwa wapya sita visiwani humo na sasa wana wagonjwa 18 na kifo kimoja.

Taarifa hiyo, ilieleza wagonjwa wapya watano ni Watanzania mbao kwa siku za karibuni hawana historia ya kusafiri nje ya nchi.

Ilisema mmoja ni raia wa Misri mwenye miaka 33 aliyeingia nchini Machi 15, mwaka huu akitokea nchini mwake kupitia Dudai kwa Shirika la Ndege la Fly Dubai.

Aliyefariki dunia ni mwanamume mwenye miaka 63 mkazi wa Kijichi aliyefariki dunia akiwa nyumbani kwake Aprili 11, mwaka huu na kuzikwa siku hiyo hiyo.

Taarifa hiyo iliongeze wagonjwa wote wamelazwa katika vituo maalumu wakiendelea na matibabu ya ugonjwa huo wa mlipuko ulioikumba dunia tangu mwishoni mwa mwaka jana.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya, inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu zinazitolewa mara kwa mara ikiwamo unawaji wa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni, kuepuka misongamano na kuahirisha safari za nje na ndani zisizo za lazima,” ilisema taarifa hiyo.

MAKONDA 

Katika hatua nyingine,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza vituo 24 vitakavyotumika kuwafanyia vipimo watu wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya irusi vya corona.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa jana kwa njia ya mtandao, Makonda alisema endapo mtu atajisikia ana dalili za corona ikiwamo mafua makali, homa kali na kikohozi, anaweza kufika kwenye vituo hivyo na kupimwa kama anamaradhi ambayo anaona dalili zake na mengine kama malaria.

Alisema endapo utapimwa na kuonekana huna magonjwa hayo, wataalamu kwenye hospitali hizo watakuwa na jukumu la kuwasiliana na maabara ya taifa  ili kuchukua sampuli na kupima kuona kama una corona ama laa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Manispaa ya Kinondoni vituo vilivyoteuliwa ni Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Magomeni kituo cha afya, Mikoroshini Kituo cha Afya, IST Clinic, TMJ hospitali na Rabininsia.

Manispaa ya Ilala, ni Hospitali  ya Rufaa ya Amana, Buguruni Hospitali, Mnazi mmoja hospitali, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hindu Mandal, Agha Khan na Regency.

Katika Wilaya ya Temeke, ni Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Mbagala Rangi Tatu, Yombo HC, TOHS hospitali. Ubungo ni Sinza hospitali, kituo cha Kimara, Mloganzila, Bochi, huku Manispaa ya Kigamboni, ni kituo cha afya Vijibweni, Kigamboni na Agha Khan.

Makonda kupitia taarifa hiyo alisema wahisiwa wa ugonjwa huo, wamekuwa wakipimwa katika maabara kuu ya taifa, lakini changamoto ambayo imekuwa ikijitokeza ni baadhi ya watu wenye dalili za ugonjwa huo kupita vituo kadhaa vya kutolea huduma za afya na kukutana na watu kadhaa kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa hali inayoweza kuchangia kuongezeka kwa visa vya ugonjwa kwa kasi kubwa. 

“Mkoa umejipanga kupunguza ueneaji wa ugonjwa kwa kuainisha vituo maalumu vya wahisiwa wanaokidhi vigezo vya tafsiri ya ugonjwa kuchukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya maabara katika maabara kuu ya taifa.

“Ieleweke  vituo hivi havitatumika kupima samapuli za corona, bali ni vituo vya kukusanyia sampuli za wahisiwa tu. Vituo hivi vitaongeza kasi ya mapambano dhidi ya corona,” ilisema taarifa ya Makonda.

WABUNGE NA BAA

Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema ushauri wa wabunge wa kutaka baa zifungwe kipindi hichi cha ugonjwa wa corona linatakiwa kuangaliwa.

Akizungumza jana wakati wa majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya  Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,George Mkuchika wakati kwa mwaka 2020/21,Ndugai alisema kuna haja ya jambo hilo kuangaliwa.

“Mheshimiwa Jenista (Mhagama) ushauri wa  baa iwe ‘take away’  mtu afungashe aondoke,”alisema Spika Ndugai.

Awali akichangia,Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema anashangaa ni kwa jinsi gani mtu ambaye amelewa kama anaweza kufuata masharti ya ugonjwa wa corona ya kutokumsogelea mtu. 

“Kwa namna gani mtu aliyelewa anafuata masharti ya corona mtu anaambiwa akae mbali na mhudumu hivi mtu hawezikulewa nyumbani wale wahudumu watakuwa na usalama kiasi gani kuna haja gani ya kucheza disco na baa, lazima  kuwekwa utaratibu,” alisema.

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) alisema kipindi hiki kuna haja ya kuangalia makato ambayo amekuwa akikatwa mfanyakazi ili kumpungizia mzigo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles