Mwandishi Wetu, Geita
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi kwenye kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Mbugani iliyopo katika Halmashauri ya Mji Geita.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam Ole Nasha amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara hiyo mkoani Geita jana Alhamisi Agosti Mosi.
Amesema fedha hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu nchini ambapo amesema serikali inatambua umuhimu wa kuwajengea fursa na mazingira mazuri ya kusoma watoto wenye mahitaji maalumu na ndiyo maana imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba kunapatikana walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vitabu ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo kutokana na changamoto zao za kimaumbile.
“Kwa miaka mingi jamii nyingi zimekuwa zikiwatenga watoto wenye mahitaji maalim, lakini kwa sasa nashukuru tumeendelea kuwawezesha kupata haki yao ya elimu kama walivyo watoto wengine na kwamba wanaweza kuwa na changamoto za kimaumbile lakini ubinadamu wao upo pale pale,” amesema Waziri Ole Nasha.
Aidha, amewataka wanafunzi hao kutokatishwa tamaa na changamoto walizonazo za kimaumbile kwani serikali imewawekea mazingira ya kuwawezesha kufika mbali zaidi katika elimu na kuwataka kuendelea kutumia fursa hizo za kielimu ili kutengeneza maisha yao ya baadaye.
“Wanafunzi, mtu hawezi kujua kipaji chako ni kipi lakini serikali inakupa fursa ya kuonyesha kipaji chako, Rais ametambua uwezo mkubwa wa watu wenye mahitaji maalumu na ndioyomaana siku hizi tunaye Naibu Waziri anayeshughulika na watu wenye mahitaji maalumu ambaye naye ana changamoto ya ulemavu,” amesema Naibu Waziri.