27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YATISHIA KUFUTA NGO’s

 WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa

Mwandishi Wetu, Ngorongoro

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali itazifutia usajili Taasisi Zisizokuwa za Serikali (NGO’s) zilizoko kwenye Tarafa ya Loliondo zinazofanya kazi kinyume na katibana sheria za nchi.

Amezipa miezi sita kujitathimini kama zinafanya kazi ya kuhudumia jamii au la.

Pia ameahidi kumpeleka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Tarafa hiyo ya Loliondo  kuzifanyia ukaguzi NGO hizo  kubaini kiasi cha fedha wanazopata kama kinalingana na matokeo ya kazi za jamii inazofanya katika tarafa hiyo.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wakurugenzi wa NGO na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwa katika ziara ya  kazi mkoani Arusha.

Alisema NGO nyingi zimekuwa zikipata bajeti kubwa ya fedha lakini masuala ya maendeleo wanayoyafanya katika eneo hilo hayalingani na bajeti halisi wanayopata.

“Loliondo pekee kuna NGO zaidi ya 30 ila zilizokuwa ‘active’ ni 15 tu kuna nini Loliondo? Na baadhi yake zinafanya kazi ya kuchochea eneo hili lisiwe na amani,”alisema.

Miongoni mwa NGO hizo ni PWC inayopata Sh bilioni 2.5 kwa mwaka, UCRT inayopata Sh bilioni 1.5 kwa mwaka na Oxfarm Tanzania inayopata Sh bilioni 1.7 kwa mwaka.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa: “Watu wote wanaoshirikiana na NGO hizo zinazochafua taswira ya nchi tutawashughulikia. “Mnawavalisha watoto kandambili zilizotoboka na miguu michafu kisha mnawapiga picha mnazituma kwenye mitandao na kusema umasikini wa Tanzania ndiyo huo. Hatutawavumilia watu wa namna hii.

“Nitafuatilia kwa karibu kuona kazi wanazozifanya kwa sababu  zinapata fedha nyingi kwa mwaka. Lazima tujenge nidhamu kwa wote wanaopata fedha kwa lengo la kuisaidia jamii.

“Wote wanaojihusisha na shughuli nje ya mikataba yao wabadilike ndani ya miezi sita. Wafuate kanuni, sheria na taratibu za nchi,” alisema.

Alizitaka NGO hizo kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA)   ziweze kutambulika katika sheria na ofisi zake zijulikane badala ya hivi sasa kuwa na ofisi za mifukoni.

Awali, Waziri Mkuu, alizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ololosokwan ambako alizungumzia  mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Tarafa ya Loliondo   na wawekezaji.

Alisema Serikali itahakikisha mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu unamalizika haraka.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kukutana na uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro na kamati ya wananchi iliyoundwa kwa ajili ya kuboresha uhifadhi ili kumaliza mgogoro huo na  kumpelekea taarifa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wananchi kuingiza ng’ombe holela kutoka nje ya nchi.

Alsema  kitendo hicho kinachangia kuwapo  migogoro ya ardhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles