31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatangaza kufuta Diploma ya ualimu

ndalichakoPatricia Kimelemeta

SERIKALI imefuta diploma maalumu ya ualimu ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kuongeza idadi ya walimu.

Itakumbukwa wakati Serikali inaanzisha diploma hiyo, ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa somo la sayansi.

Diploma hiyo ilianzishwa na Serikali ya awamu ya nne, baada ya kujitokeza upungufu mkubwa kwa walimu wa masomo hayo na kutolewa kwenye vyuo mbalimbali, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na Serikali na kusainiwa na Kaimu Kamishna wa Elimu Tanzania, Nicolas Burreta, ambao umeanza kutumika mwaka wa masomo 2016/17 katika vyuo vya elimu vya Serikali na binafsi, wizara ilihusisha programu za mafunzo ya ualimu mwaka 2014/15 ili kukidhi mahitaji ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.

Waraka huo, unasema hivi sasa wizara inaendelea na maandalizi ya sheria, kanuni na miongozo ya utekelezaji wa sera hii, ikiwamo uendeshaji na usimamizi wa mafunzo ya ualimu nchini.

Sehemu ya waraka huo inasema: “Kwa kuzingatia maandalizi yanaendelea, mwongozo wa utekelezaji wa programu za mafunzo ya ualimu ya mwaka 2016/17 utakuwa wa mafunzo ya ualimu kwa astashahada (cheti) na stashahada.

“Mafunzo hayo yataendeshwa kwa kutumia mtaala wa kitaifa ulioandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) wa mwaka 2009 kwa astashahada na stashahada. Kutokana na hali hiyo, wizara itakuwa inatoa maelekezo ya sifa za kujiunga na mafunzo ya ualimu.”

Pia unasema mafunzo hayo tarajali ya stashahada ya juu ya elimu ya sekondari yaliyokuwa yakitolewa kuanzia mwaka wa masomo 2014/15, yamehitimishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) na kutoa tuzo ya stashahada ya kawaida ya ualimu ya sekondari kwa wahitimu wa programu hiyo baada kukamilisha mwaka wa pili wa masomo.

Aidha, wanachuo wanaoendelea na mafunzo tarajali ya ualimu wa stashahada ya kawaida kwa kutumia mtaala wa Tuzo za Taifa za Elimu ya Ufundi (NTA), wataendelea na mafunzo yao na kuhitimisha kama ilivyopangwa.

“Programu ya mafunzo kazini ya stashahada ya elimu ya msingi iliyokuwa inatumia mtaala wa Tuzo za Taifa za Elimu ya Ufundi (NTA), imesitishwa ili kufanyiwa maboresho.

“Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), litatahini na kutoa tuzo ya mafunzo ya ualimu ya astashahada na stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2016/17 na kuvitaka vyuo vya ualimu kuhusika kutoa mafunzo ya ualimu (astashahada na stashahada) pekee, bila kuchanganya kozi nyingine.

 

WADAU 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema Serikali ya awamu ya nne iliamua kuanzisha programu hiyo kwa ajili ya kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Alisema kitendo cha Serikali ya awamu ya tano kuifuta, ni sawa kwa sababu wenyewe ndio waliamua kuanzisha na wenyewe ndio wameamua kuifuta, hivyo walimu wa masomo hayo watakwenda kutafutwa nje ya nchi.

“Mpaka sasa kuna uhaba wa walimu wa sayansi, jambo ambalo limechangia Serikali ya awamu ya nne kuanzisha programu hii, kitendo cha kufuta ni uamuzi wao wenyewe, labda watakwenda nje ya nchi kutafuta walimu wa sayansi,” alisema Mukoba.

Aliongeza vijana wengi waliosoma masomo ya sayansi na kuhitimu kidato cha sita wanakwenda chuo kikuu kutafuta taaluma nyingine, siyo ya ualimu, hivyo wananchi wategemee tatizo la uhaba wa walimu litaendelea siku hadi siku.

“Kuna vijana wengi wanaohitimu kidato cha sita ambao wamesoma sayansi wanakwenda chuo kikuu kutafuta taaluma nyingine, ikiwamo ya udaktari na si ualimu, kwa mtindo huu tatizo la walimu litaongezeka,” alisema.

Alisema Serikali imeamua kuboresha diploma ya msingi kwa walimu kwa madai ya kujipanga upya, lakini ni imani yao wakimaliza kujipanga watakuja na uamuzi mzuri ambao utasaidia kuboresha sekta ya elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Profesa Innocent Ngalinda,  alisema uamuzi huo ni mzuri kwa sababu umelenga kuboresha sekta hiyo.

Alisema siku hizi digrii ni sawa na elimu ya kidato cha nne, Serikali lazima ihamasishe walimu ili wajiendeleze.

“Kuondolewa programu hii kutasaidia walimu wengi kujiendeleza kielimu, kwa sababu digrii ya sasa ni sawa na elimu ya kidato cha nne, tunapaswa kujifunza siku hadi siku ili twendane na wakati,” alisema Ngalinda.

Alisema ili taifa liweze kupata maendeleo, linahitaji mwalimu bora ambaye amezalishwa katika chuo bora kwa ajili ya kutoa elimu bora zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles