21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yataka kasi utoaji elimu ya mazingira shuleni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande, ameagiza kuongezwa kasi ya utoaji elimu ya utunzaji mazingira shuleni kunusuru uharibifu unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande, akipanda mti wakati wa tamasha la vipaji vya kutunza mazingira na harambee iliyoandaliwa na Shule ya Awali na Msingi ya Bright African iliyopo Kata ya Kivule, Dar es Salaam.

Ametoa agizo hilo wakati wa tamasha la vipaji vya kutunza mazingira na harambee iliyoandaliwa na Shule ya Awali na Msingi ya Bright African iliyopo Kata ya Kivule.

Amesema maendeleo yanayofanyika hivi sasa kama hayatahusisha utunzaji wa mazingira taifa litalazimika kutumia gharama kubwa kuyarejesha katika hali yake ya kawaida.

“Tusipotunza mazingira hatutaishi kwa amani na furaha, tutakuwa na taharuki tu na matokeo ya kutotunza mazingira na uharibifu wa mazingira ni makubwa hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwa balozi wa mazingira,” amesema Chande.

Naibu Waziri huyo pia ameahidi kuchangia Sh milioni 2 na mifuko 30 ya saruji ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo.

Naye Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, ameahidi kuchangia Sh milioni 1 kuboresha mazingira ya shule hiyo wakati Diwani wa Kata ya Mzinga, Bob Isaack akiahidi kuchangia Sh 150,000 na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kivule, Amos Hangaya, akiahidi kuchangia Sh 100,000.

Amesema pia ujenzi wa vyumba vya madarasa 195 vinavyogharimu Sh bilioni 2.5 unaendelea kwa kasi na kwamba mengine yamefikia katika hatua ya kupauliwa.

Aidha amewahakikishia wakazi wa jimbo hilo kuwa barabara za Kivule Msongola, Kivule Mkolemba na Moshi Bar Bomba Mbili tayari wakandarasi wamepatikana huku akisema kiu yao kubwa ni kupata barabara za uhakika hasa za lami.

Awali Kaimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi ya Bright African, amesema wameanzisha taasisi ya mazingira ya Bright African Environment Development Group kwa lengo la kusimamia mazingira kwa vitendo ambapo pia watakuwa wakiotesha vitalu vya miti na matunda na kugawa kwa jamii ili kuhifadhi mazingira.

“Tumekuwa tukifanya vizuri kitaaluma hasa katika mitihani ya taifa ya kuhitimu elimu ya msingi, lakini tuna changamoto kadhaa ndiyo maana tuliamua kuandaa harambee ili kupata fedha zitakazosaidia kuboresha mazingira ya shule yetu,” amesema.

Shule hiyo yenye wanafunzi 870 kati yao wasichana ni 509 na wavulana 361 na katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba 2020 imeshika nafasi ya 34 kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles