25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

DC Muleba asisitiza utunzaji vyanzo vya maji

Renatha Kipaka, Muleba

Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila, amesisitiza juu ya utunzaji wa vyanzo vya Maji ili kuondoa uhaba wa huduma ya Maji wilayani humo.

Nguvila ametoa kauli hiyo juzi katika ziara ya ukaguzi wa vyanzo vya maji ambapo aliungana na wataalamu wa mamlaka ya maji MLUWASA.

Aidha, Nguvila ametoa maagizo kwa mamlaka kusimamia ipasavyo na kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kupanda miti rafiki, kufanya usafi wa mazingira wa mara kwa mara.

Pia Nguvila amekagua chanzo cha maji cha Kaigara, chemichemi ya Ihako na chemichemi ya Nyamwala matenki ya kuhifadhia maji ambayo ni tanki la Buyango, tanki la Kaigara na tanki la Bomani (Kibonwangoma).

“Tupande miti aina ya mibuyu na parachichi ambayo ni rafiki kutunza maji na wakati mwingine tuache vichaka viwe vingi ambavyo vitasaidia kutunza asili ya maji. iti ambayo sio rafiki kwa vyanzo vya maji ikatwe na ipandwe miti ambayo ni rafiki kwa maji wakati huu wa mvua miti ikipandwa ya kutosha kutunza vyanzo hivi vya maji hatutakuwa na ukosefu wa huduma ya maji,” ameeleza Nguvila.

Aidha, ameagiza wataalam wa idara ya maji kwa kushirikiana na wataalam wa Ardhi na Maliasili kuhakikisha wanawaondoa wananchi wanaofanya shughuli za kilimo pamoja na ujenzi wa nyumba karibu na vyanzo vya maji hususan katika chanzo cha maji cha Kaigara.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji Muleba Mjini, Mhandisi Augustino Kasindi amesema mgao wa maji unasababishwa na upungufu wa uzalishaji wa huduma ya maji unaosababishwa na wananchi wanaofanya shughuli za binadamu kama kilimo na ujenzi kwenye vyanzo vya maji ambapo ametolea mfano wa chanzo cha maji cha Kaigara kilichovamiwa kwa asilimia kubwa na kusababisha kupungua kwa maji katika chanzo hicho.

Amesema kutokana na shughuli hizo za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mita sitini mwanzoni walikuwa na uwezo wa kuzalisha lita 265 lakini kwa sasa maji yanazaliswa lita 120 mpaka 130 kwa siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles