Derick Milton, Simiyu
Serikali imetaifisha pamba inayodaiwa kuwa ya magendo ikiwa ni siku mbili baada ya kukamatwa kwa gari aina ya scania yenye namba za usajili T917 BCN ikiwa na pamba tani zaidi ya 20.
Pamba hiyo ilikamatwa katika kijiji cha Dutwa Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Agosti 12, mwaka huu saa tano usiku, ikisafirishwa bila kibali maalumu huku ikiwa haijulikani wapi inapelekwa wapi imenunuliwa wapi.
Akitoa uamuzi ya kuitafisha pamba hiyo leo Jumatano agosti 14, Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga amesema uchunguzi umeonyesha kuwa pamba hiyo ilinunuliwa kwa njia za machinga kwa Sh 700 hadi 900 kutoka kwa wakulima.
“Wakati serikali ikipambana na watu wanaonunua pamba kwa njia za kimachinga, bado wako wafanyabishara wanaendelea kupiga vita juhudi hizo kwa kuendeleza biashara hiyo na kuwanyonya wakulima.
“Baada ya wahusika kushindwa kujitokeza, sasa kama Mkuu wa Wilaya nachukua uamuzi wa kuitaifisha pamba hii na tunaenda kuiuza kwenye viwanda vya kuchambua pamba leo hii na fedha zote zitapelekwa kununua vifaa vya kukamilisha ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Simiyu,” amesema Kiswaga.
Amesema Ofisi yake haitalala ili kuhakikisha inapambana na biashara hiyo ili wakulima wa pamba waweze kunufaika na zao hilo.
Aidha, amesema pamba hiyo ina thamani ya zaidi ya Sh milioni 10, na mara baada ya kuuzwa uchunguzi utaendelea kujua nani mhusika mkuu na wakati huo huo gari litaendelea kushikiliwa.