24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Kata za Nkuyu, Nkoma zaongoza ukatili wa kijinsi

Mwandishi Wetu -Itilima

IMEELEZWA kata za Nkuyu na Nkoma, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, zinaongoza kuwa na matukio makubwa ya ukatili wa kijinsia.

Chanzo kikubwa kinatajwa kuwa ni baadhi ya viongozi wa siasa na wakazi wa kata hizo, kuwaficha wahusika wa matukio ya ukatili.

Hayo yalisemwa jana na baadhi ya maofisa watendaji wa kata hizo, wakati wa warsha ya siku moja iliyoratibiwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Kawiye Social Development Foundation (KASODEFO).

Warsha hiyo ilikuwa na lengo la kuwakutanisha wadau wanaohusika na udhibiti wa ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake.

Watendaji hao, walisema baadhi ya madiwani na wananchi wenyewe wamekuwa chanzo cha ongezeko la vitendo vya ukatili wa wanawake na watoto kutokana na wao kuwaficha watuhumiwa kwa hofu ya kupoteza kura zao pamoja na kuvunja undugu baina yao.

 “Wazawa waishio huko wengi wana mfumo dume, sambamba na baadhi ya viongozi wa siasa ambao tuliwategemea  wawe mstari wa mbele kutusaidia dhidi ya ukatili huu, hali ipo tofauti, baadhi yao wamekuwa wanasababisha kuongezeka mambo hayo kwa kuyakumbatia.

“Kata yetu ipo pembezoni kabisa na mji na tumepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, watu wanashindwa kujichanganya, wengi hawana elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia, hata vyombo vya habari kufika kule ni ngumu,” alisema Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ikindilo, Alphoncina Rusasa.

Mwanasheria wa Wilaya ya Itilima, Joshua Shayo, alisema vitendo vya ukatili kwa wanawake  na unyanyasaji wa watoto wa kike, haviruhusiwi na atakayebainika atashtakiwa kwa mujibu wa sheria.

“Jamii zetu zimekuwa zikifumbia macho matatizo haya, yanatokea, kibaya wanayachukulia kama fursa ya kujipatia fedha au mali,” alisema.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, John Chale, alisema awali matukio yalikuwa mengi, lakini kadiri siku zinavyokwenda yanapungua.

Alisema jamii  ina mila na desturi ambazo wamezigeuza kama imani ambazo zinakinzana na sheria za nchi.

Mkurugenzi wa taasisi ya Kasodefo, Ezekiel Kasanga, alisema tayari wameunda kamati ya ulinzi na usalama ya mtoto na mwanamke, lengo likiwa ni  kuwakutanisha wadau wanaohusika na udhibiti wa ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Elizabeth Gumbo, alisema  mwaka 2019/20, wametenga Sh milioni 2.4 kwa kamati mbalimbali za kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles