Patricia Kimelemeta na Christina Gauluhanga
SERIKALI imesimamisha malipo kwa wakandarasi waliojenga jengo la ofisi ya Makamu wa Rais, baada ya kubainika kujengwa chini ya kiwango.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mohammed Mchengerwa alisema jengo hilo lilijengwa kwa gharama ya Sh bilioni 8 lakini tayari lina nyufa.
“Kamati ilitoa ushauri kwa serikali kusimamisha malipo ya wakandarasi baada ya kubaini jengo la ofisi ya Makamu wa Rais limejengwa chini ya kiwango,”alisema Mchengerwa.
Alisema udhaifu huo wameuona, baada ya kamati kutembelea jengo hilo ambalo lilikuwa na matatizo mengi.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imeishauri Serikali kusimamisha malipo yote na kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kufanya ukaguzi maalumu kwenye jengo hilo na kuwasilisha ripoti kwenye kamati hiyo.
Alisema ripoti ya awali, inaonyesha wakandarasi wanaidai Serikali Sh milioni 230.
Alisema pia kamati imeitaka Serikali kuwachukulia hatua Wakala wa Majengo Tanzania(TBA) ambao walihusika kutoa ushauri wa ujenzi wa jengo hilo.
Alisema jengo hilo limejengwa na wakandarasi wa ndani kutoka Kampuni ya Mecco na Kampuni ya ujenzi kutoka China.
Alisema kamati yake imeishauri Serikali kuwafikisha mahakamani watendaji watakaobainika kujenga jengo hilo chini ya kiwango.