*Rais Dk. Samia amegawa eneo hilo kwa wananachi kwa ajili ya matumizi ya vijiji
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeridhia kugawa eneo la kilomita za mraba 194 la pori tengefu la mto Umba kwa wananchi wa vijiji vinne vya Mkota, Mwakijembe, Mbuta na Pelani vilivyopo wilayani Mkinga mkoani Tanga.
Hayo yamebainishwa leo Februari 28, 2024 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa katika mkutano wa wananchi uliofanyika katika kijiji cha Mwakijembe wilayani Mkinga.
Silaa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri Nane wa Kisekta wanaosimamia maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ya vijiji 975 nchini amesema Rais Dk. Samia amegawa eneo hilo kwa wananachi kwa ajili ya matumizi ya vijiji, ili wanaoishi katika maeneo hayo waweze kunufaika kupitia shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Viongozi katika ngazi za msingi kwenye vijiji na kata husika, wasithubutu kuihujumu ardhi inayopaswa kugawiwa kwa wananchi na badala yake kujinufaisha binafsi.
“Dk; Samia ameridhia kugawa eneo la pori tengefu la Mto Umba lenye kilomita za mraba 194 kwa wananchi wa vijiji vinne, sio jambo dogo hivyo tuhakikishe wananchi wananufaika na mgawo huu,” amesema Silaa.
Aidha? Silaa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe Kanali Maulid Surumbu kuhakikisha wanafanya mikutano na wananchi na kuwashurikisha kuunda kamati zitakazosaidia ugawaji wa maeneo hayo, ili kila mwenye uhitaji aweze kupata.
Pia, Silaa amezungumzia changamoto ya eneo la mgodi ambalo watu wanafanya shughuli za uchimbaji na limeangukia katika hifadhi ya taifa Mkomazi, kwamba wizara zinazohusika za kisekta ikiwemo Maliasili na Utalii, Madini na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zitakaa ili kujadili hatma ya wananchi ambao wamewekeza katika shughuli hizo.
Silaa amewahkikishia wananchi hao kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa maamuzi yatakayotolewa hayatazua taharuki, bali yataangalia maslahi ya wananchi wanaoguswa.
“Niwathibitishie maslahi ya wananchi wote wanaofanya shughuli za uchimbaji katika eneo hili yatazingatiwa” amesema Silaa.