28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

SERIKALI YAPIGA ‘STOP’ LUKU ZA NJE

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


SERIKALI imesema kuanzia Julai mosi mwaka huu, itasitisha rasmi uagizaji wa mita za Luku ya umeme kutoka nje ya nchi ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Merdad Kalemani, wakati akizindua Kiwanda cha kutengeneza mita za Luku cha Baobab Energy System Tanzania (BEST) kilichopo maeneo ya Mbezi, jijini humo.

Alisema uwekezaji huo utasaidia kupunguza na kuokoa gharama za kuagiza mita za Luku kutoka nje ya nchi kama ambavyo wamekuwa wakifanya.

Dk. Kalemani alisema usitishwaji huo ulitanguliwa na ule wa awali wa uingizaji wa nguzo za umeme kutoka Afrika Kusini na transfoma kutoka India ambao ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya kuinua wawekezaji wa ndani.

“Hii ni awamu ya pili kwani awali tulisitisha uagizaji wa nguzo kutoka Afrika Kusini ambao ulikuwa unatumia fedha nyingi pia.

“Hadi kufikia mwaka jana, mapato ya Tanesco yalikuwa ni Sh bilioni 29 kwa wiki na mwaka huu yamefikia Sh bilioni 32.1 na hiyo imechangiwa na kuzuiwa bidhaa za nje,” alisema Dk. Kalemani.

Waziri huyo alisema upotevu wa umeme kwa mwaka juzi ulifikia asilimia 18 na moja ya sababu ya upotevu huo ni mita mbovu, hivyo kwa kutumia mita za kisasa kutapunguza upotevu huo na hatimaye kuumaliza kabisa.

“Upotevu wa sasa umefikia asilimia 13 na kufikia mwakani tunataka uwe chini ya asilimia 10. Kwa hiyo, natoa wito kwa Tanesco kuhakikisha wateja wote wanatumia mita za kisasa ili kuliondoa tatizo hilo,” alisema.

Aliongeza kwamba, Aprili 24, mwaka huu, walianza matumizi ya gesi katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo ana imani watu wengi watanufaika na mradi huo, huku akibainisha kuwa asilimia 90 ya wakazi wa Dar es Salaam wanatumia mkaa.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Hashimu Ibrahimu, alisema uamuzi wa kuanzisha kiwanda hicho ulilenga kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli wa kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Alisema walikubaliana na wabia wa EDMI kujenga kiwanda hicho nchini ili kuhudumia kwa ukaribu na ufanisi soko la Afrika Mashariki, nchi za SADC pamoja na maeneo yanayopakana nayo.

“Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha mita 500,000 kwa mwaka, hivyo kwa kiasi kikubwa tutatosheleza soko la ndani na hata kuuza nje ya nchi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles