SERIKALI wilayani Mbozi mkoani Songwe, imetoa tahadhari kwa baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaoza watoto wenye umri chini ya miaka 18 na atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kazi za kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), ambaye alisema ndoa za utotoni zimekithiri nchini, hali inayochangia mimba za utotoni na watoto kukatishwa ndoto za kupata elimu.
Kutokana na hali hiyo, alisema hivi sasa Serikali imeamua ukomesha hali hiyo kwa kutunga sheria mpya ambazo watu watakaobainika kufanya makosa hayo watafungwa jela miaka 30 au faini ya Sh milioni tano au vyote kwa pamoja.
“Serikali imeamua kila mtoto atakayehitimu elimu ya msingi anatakiwa kwenda sekondari, ili kufanikisha hilo imetungwa sheria hiyo kuwabana waharibifu wote wanaoharibu maisha ya watoto,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo, alisema ni muhimu wananchi hasa wazazi kuzingatia suala hilo kwa kuwa Serikali ina mpango mzuri wa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.