32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yajipanga kutokomeza mauaji ya albino

Bahame NyandugaNA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeahidi kuandaa kanuni zitakazosimamia waganga wa tiba mbadala ili kupunguza vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye ualbino.

Pamoja na hali hiyo, imeahidi kuandaa mashtaka kwa ubora zaidi dhidi ya kesi za mauaji ya maalbino pamoja na kuimarisha kampeni maalumu na endelevu za ufahamu kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akielezea kuhusu Mpango wa Kihistoria wa Utekelezaji kwa Albino Barani Afrika, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga,  alisema mauaji dhidi ya albino yamekuwa yakitokea kila kukicha kwa sababu ya mambo mbalimbali ikiwemo ushirikina.

Alisema Serikali inatakiwa kuongeza  bajeti yake ili watu wenye ulemavu wapate haki sawa katika masuala ya matibabu.

“Albino wengi wanaendelea kuathirika afya zao kwa sababu ya kukosa matibabu yanayotakiwa na hiyo inatokana na ukosefu wa fedha,” alisema Nyanduga.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Haki za Binadamu, alisema Serikali itahakikisha kuwa vifaa vya kuimarisha uwezo wa kuona vinapatikana kwa ajili ya watu  wenye ulemavu wa ngozi anapokuwa darasani na kutoa vizuia jua nafuu kama tiba muhimu ili kuzuia saratani ya ngozi ambayo inawaathiri wengi wao na kupoteza  maisha kila kukicha.

Akizungumzia kongamano lililofanyika hapa nchini hivi karibuni na kuhusisha nchi 29 Kanda ya Afrika, mtaalamu Huru wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero, alisema  lililenga kujadili mbinu za kuzuia mauaji ya watu wenye ualbino yanayoendelea kutokea barani Afrika.

“Washiriki wa kongamano lile waliitikia wito na kutoa mapendekezo ikiwa ni pamoja na kuandaa hatua maalumu, rahisi na madhubuti ambazo zinaweza kutekelezwa na wadau wote ili kupunguza vifo na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la The Under  The Same Sun (TUS), Vicky Ntetema, alisema kwa pamoja wataendelea kupambana na unyanyapaa na mauaji dhidi ya watu wenye ualbino.

Alisema polisi wa kimataifa na watu wa Uhamiaji washirikiane kwa pamoja na wananchi ili kulinda watu wanaopitisha maalbino katika mipaka ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles