28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Samia: Wanaume washirikishwe mabadiliko

samia-suluhuNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, ameyataka mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini (NGOs) hasa yale  yanayoshughulikia masuala ya wanawake na watoto kujenga utamaduni wa kushirikisha wanaume katika kampeni za kumwinua mtoto wa kike kwa lengo la kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.

Kauli hiyo aliitoa juzi jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya uzinduzi wa Binti Klabu iliyofanyika sambamba na harambee ya fadhili mtoto asome ya kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto 500 wa Wilaya ya Kinondoni iliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Binti Foundation.

Alisema wanaume kama wakala wa mabadiliko wanapaswa kushirikishwa na wajue ajenda ili wawe mabalozi wazuri katika kuzungumzia umuhimu wa kumwinua mtoto wa kike kielimu, kiafya na kwenye masuala ya ujasiriamali.

“Tuwaingize wanaume kama wakala wa mabadiliko, tuwashirikishe, wajue ajenda zetu katika mapambano hayo, wanaume wanashikilia sehemu nyingi, watumie nafasi hizo tulete mabadiliko,” alisema Makamu wa Rais na kuongeza:

“Penye mkusanyiko wa watu 100, ukiingiza wanaume 20 na wakajua madhumuni ya mkusanyiko wetu, wataenda kushawishi wenzao 20,000 huko nje,” alisema.

Aliwataka wazazi kuwatunza watoto wao kwani ni zawadi kutoka kwa Mungu na kuhakikisha wanapata elimu zote za dini na za dunia ili kuwajenga kimaadili waweze kuwa raia wema.

Awali akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Mtendaji Mkuu wa Binti Foundation, Johari Sadik, alisema shirika hilo liliamua kuunga mkono jitihada za Serikali ili kuwawezesha watoto kumudu masomo yao na hatimaye kufikia malengo yao.

“Kwa hiyo ukiwa na fedha taslimu, ama vifaa kama vile kalamu, madaftari, pedi, vyote tunapokea kwa ajili ya kusaidia watoto ambao malengo yao yanaweza yasitimie kutokana na changamoto hizo,” alisema.

Kampeni hiyo ya fadhili mtoto asome imeanzia kwa watoto 500 wanaoishi kwenye mazingira magumu wa shule za msingi Mwananyamala, Hananasif, Kumbukumbu na Msasani zilizoko katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles