Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA
SERIKALI imepiga marufuku mwalimu kumchapa mwanafunzi na kutembea na kiboko katika eneo la shule.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve (CCM).
Katika swali lake, Tweve aliitaka Serikali itoe tamko kuhusu walimu kufofuata sheria ya uchapaji viboko kwa wanafunzi.
“Kuna changamto katika uekelezaji wa utoaji wa adhabu mashuleni, kwa mfano sheria inamtaka kabla mwalimu hajatoa adhabu, lazima apate kibali kutoka kwa mkuu wa shule, lakini pia na idadi ya viboko anayotakiwa kuchapwa mwanafunzi ni viboko vinne.
“Lakini kuna baadhi ya walimu wachache hawafuati taratibu hizo, naiomba Serikali itoe tamko rasmi kwa walimu wote nchini juu ya wao kufuata sheria za utoaji adhabu kwa wanafunzi,” aliuliza Tweve.
Akijibu, Ole Nasha alisema utaratibu wa viboko umeainishwa vizuri katika Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002, uliotengenezwa chini ya kifungu cha 66 cha sheria ya elimu.
“Mwongozo huo pamoja na mambo mengine umeeleza dhahiri kwamba kuna makosa ambayo viboko vitatakiwa vitumike na siyo kwa kila kosa, bali kwa makosa makubwa ya kinidhamu na yenye sura ya kijinai,” alisema Ole Nasha.
Kuhusu viboko, alisema waraka huo unaeleza wazi kwa wakati mmoja mwanafunzi hatakiwi kuchapwa viboko vinavyozidi vinne.
“Lakini pia anayeruhusiwa kuchapa siyo mwalimu yeyote, bali ni mkuu wa shule au makamu wake au mwingine yeyote aliyepewa ruhusa hiyo kwa maandishi.
“Kitu kingine kinachoelezwa katika waraka huo ni kuchapa viboko lazima kibali, na kitolewe na mkuu wa shule kwa maandishi maana waraka unasema waziwazi kwamba ni marafuku mwalimu yeyote kutembea na kiboko kwa ajili ya kumchapa mwanafunzi,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaagiza maofisa elimu wote kuhakikisha wanagawa waraka huo kwa walimu ili wausome na wautekeleze.
Awali katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa Serikali kudhibiti au kukomesha adhabu shuleni ambazo wakati mwingine husababisha vifo.
Akijibu, Ole Nasha alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa wanaobainika kujihusisha na vitendo vya kikatili au unyanyasaji dhidi ya watoto kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi na sheria za nchi.
“Mfano walimu waliohusika kumpiga mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kibeta iliyopo Manispaa ya Bukoba na kusababisha kifo chake walisimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani na kesi inaendelea, na ofisa elimu kata, mwalimu mkuu na msadizi wake wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi,” alisema.