24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

 JPM ateta na Rostam Aziz

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara Rostam Aziz Ikulu, Dar es Salaam jana.

Rostam ambaye pia alipata kuwa mbunge wa Igunga mkoani Tabora, alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi bora na kutengeneza misingi imara ya uchumi unaokua kwa uhakika zaidi.

Alisema Rais Magufuli amejenga miundombinu, ikiwamo barabara, reli na bandari ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira. Mfanyabiashara huyo alisema anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli, huku akisema jukumu la wafanyabiashara ni kutumia fursa nyingi zilizopo katika viwanda, ujenzi na nyinginezo.

“Nimekuja kumwona rais wangu na mwenyekiti wangu wa CCM, nimekuja kumpongeza kwa kazi nzuri anazozifanya, namtakia kila la kheri.

 “Tunamuunga mkono Rais kwa kuhakikisha Watanzania tunawekeza katika nchi yetu, kukuza uchumi wetu, hilo ndilo la msingi kwa sisi wafanyabiashara,” alisema Rostam.

Alishauri wafanyabiashara kuwekeza kwenye viwanda na fursa ambazo zinajitokeza na kwamba si sawa wawekezaji kutoka nje kuja nchini kujenga uchumi wakati Watanzania wapo.

“Mimi nilikuwa kwenye siasa, niling’atuka muda mrefu sana. Sisi kama wafanyabiashara tunaangalia fursa ikiwa ni kuwekeza kwenye viwanda na zingine zitakakojitokeza, huko mbele ni nyingi zaidi.

“Tutaziangalia fursa hizo na kuzitumia kwa sababu Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe, siyo tutegemee wawekezaji waje kujenga uchumi, sisi ndio tunatakiwa kuwekeza na kukuza uchumi wetu, hilo ndilo jambo la msingi kuhakikisha tunamuunga mkono Rais kwenye kuwekeza.

“Kwenye kurekebisha chochote kuna maumivu yanatokea, haya maumivu ni muhimu ili kuwa na uchumi endelevu, watu waliozoea labda mambo laini laini sasa wanapata tabu kidogo, itabidi sasa wajirekebishe kuendana na wakati,” alisema.

Rostam ambaye pia alipata kuwa mwekahazina wa CCM, aliwapongeza viongozi wa chama hicho kwa kuweka utaratibu wa kuchagua viongozi wenye uwezo na si wenye fedha.

“Nakipongeza chama changu na viongozi kwa kuhakiki mali za chama na kuhakikisha zile mali za chama zinafanya kazi ambazo zinastahili kukipa mapato chama, hata kwenye chaguzi hivi sasa kinachofanyika ni uwezo wa mtu unaangaliwa zaidi kuliko fedha, hiyo ya ‘ku-fight corruption’ ndani ya chama nayo inakwenda vizuri na CCM ndiyo maisha ya Mtanzania.

“Sisi wana CCM tunataka kuhakikisha chama chetu kinashinda milele, ni bahati mbaya patatokea wakati soko huria halifanyi kazi ipasavyo, na pale ambapo halifanya kazi ipasavyo Serikali haina budi kuingilia, kwahiyo Serikali imefanya hivyo wakati mwafaka kwa tatizo ambalo limejitokeza kutokana na mfumo wa soko huria kutokuwa kamili kabisa, nadhani Serikali imebidi ifanye hayo iliyoyafanya,” alisema.

Akizungumzia kuhusu sakata la zao la korosho, Rostam alisema anategemea wafanyabiashara watajiandaa zaidi pamoja na wizara husika ili yaliyojitokeza yasitokee tena.

“Tunategemea wafanyabiashara watajiandaa zaidi, wizara zinazohusika zitajiandaa vizuri ili tusirudie haya yaliyojitokeza kwenye zao la korosho.

“Kwakweli unapokuwa kwenye siasa unaonekana zaidi, lakini unapokuwa kwenye biashara unaonekana nyumbani kwako na ofisini kwako, sasa inawezekana huonekani mitaani, hauko kwenye mikutano ya hadhara, tupo tunaendelea na shughuli zetu,” alisema mfanyabiashara huyo.

Mbali na Rostam, Rais Magufuli pia alikutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa John Cheyo (Mwenyekiti wa Chama cha UDP), James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na John Shibuda (Katibu Mkuu wa Ada Tadea).

 

JAMES MBATIA

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), alisema katika kutekeleza malengo 17 ya dunia, Tanzania inafanya vizuri katika lengo la elimu ambalo linazungumzia elimu bora na shirikishi.

Pia mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa Watanzania wote wana kila sababu ya kuendelea kuijenga nchi yao kwa mawazo ya pamoja yanayozingatia ujumbe uliomo katika wimbo wa taifa unaosisitiza hekima, umoja na amani.

 

JOHN SHIBUDA

Kwa upande wake, Shibuda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, alisema amekutana na Rais Magufuli ili kumpongeza kwa uamuzi mzuri alioufanya kutatua tatizo la soko la korosho.

Shibuda alimhakikishia Rais Magufuli kuwa vyama vya siasa vinamuunga mkono kwa uongozi mzuri unaolenga kurekebisha dosari za mmomonyoko wa maadili ndani ya Serikali na taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

“Katika miaka mitatu, Rais Magufuli amerejesha sifa ya utaifa wetu ya kuwa nchi ya kuaminika na kusadikika na ameweka ari ya uhuru na kujitegemea, tulikuwa na hali duni na dumavu ya maendeleo na ustawi wa jamii, tulikuwa na hali ambayo maendeleo yetu hayawiani na maliasili tulizonazo na rasilimali tulizonazo,” alisema Shibuda.

 

JOHN CHEYO

Naye Cheyo alimpongeza Rais Magufuli kwa msimamo na ujasiri aliouonesha katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Aliwataka Watanzania kujivunia kuwa na Rais ambaye ameonesha dhamira njema ya kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Sisi Watanzania ni lazima tujivunie Rais tuliyenaye, ni Rais anayetoa maamuzi, hata kama yatakuwa magumu kiasi gani, akiamua kusema tunakwenda kujenga Stieglers’ Gorge tutakwenda.

“Akiamua kuwa tunakwenda kujenga standard gauge tunakwenda, akiamua watoto watasoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari inafanyika na katika miaka mitatu hii imedhihirika kuwa maamuzi yake yanalisaidia taifa sana,” alisema Cheyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles