Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakati wadau mbalimbali wa tasnia ya habari wakitamani kuona Bodi ya Idhibati ya Habari huru, Serikali imesema hilo ni miongoni mwa jambo muhimu ambalo inakwenda kulifanyia kazi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Julai 13, 2022 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-(MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kwenye Mkutano wa Wadau wa Maendeleo uliofanyika katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Msigwa amesema kuwa serikali imeonesha dhamira nakwamba inataka kwenda kupitia upya.
“Suala la Bodi ya Ithibati, hayo ni miongoni mwa mambo yanayokwenda kujadiliwa kwenye mchakato mzima wa kupitia upya sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016 ambayo ndio imeunda hiyo Bodi ya Ithibati.
“Ninachotaka kusema ni kwamba, serikali imeonesha dhamira sasa kwamba tunataka kwenda kupitia upya sheria na taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari,” amesema Msigwa.
Lengo la wadau ni kuona Bodi hiyo ya Ithibati inaweka mazingira ya usawa kati ya serikali na vyombo vya habari nchini ambapo Msigwa amesema kuwa wadau wadau wameonesha nia ya kushirikiana na serikali.
“Wadau wameonesha nia ya kushirikiana na serikali, wadau na waandishi wa habari katika kuhakikisha tunaweka vizuri mazingira ya waandishi wa habari na vyombo vya habari,” amesema Msigwa.