27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaeleza vikwazo katika kudhibiti vifo vya akinamama na watoto

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema imani, mila, na desturi za kitamaduni, ukosefu wa usawa wa kijinsia bado ni miongoni mwa sababu zinazorudisha nyuma udhibiti wa magonjwa na vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini.

Hayo yameelezwa leo Mei 9, jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angellah Kairuki katika hafla ya fupi ya makabidhiano ya majengo, vifaa vya huduma za dharura za afya ya uzazi na mtoto na gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha Dabalo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma msaada uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi(UNFPA) kupitia mradi wa RMNCH unaotekelezwa na TAMISEMI.

Waziri Kairuki amesema kuwa kuna mambo makubwa mawili yanayokwamisha juhudi hizo za kupunguza vifo ambayo ameyataja kuwa ni yale yanayohusus mfumo wa afya na yaliyo nje ya mfumo wa afya.

“Kuna sababu zinazorudisha nyuma udhibiti wa magonjwa na vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini miongoni mwa hizo ni mambo yanayohusu mfumo wa afya ikiwa ni pamoja na kutotekelezwa ipasavyo kwa sera, miundombinu dhaifu ya afya, upatikanaji mdogo wa huduma bora za afya.

“Uhaba wa rasilimali watu, upungufu wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, mifumo dhaifu ya rufaa, ukosefu wa vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi na uratibu duni kati ya sekta za umma na sekta binafsi.

“Sababu nyingine ni mambo yaliyo nje ya mfumo wa afya ikiwa ni pamoja na ushiriki duni wa jamii na ushirikishwaji katika kupanga, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya wa huduma za afya, baadhi ya imani, mila, na desturi za kitamaduni, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na kutokuwa na tabia za kutafuta huduma za afya kwa wakati, pindi changamoto za kiafya zinapoanza kujitokeza.

“Ili kukabiliana na changamoto hizi kunahitajika juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau wengine wa Maendeleo katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingke Mtambuka. Makabidhiano tunayoshuhudia leo ni sehemu ya juhudi hizi za pamoja kati ya UNFPA, Serikali ya Denmark na Serikali ya Tanzania,” amesema Kairuki.

Aidha, Kairuki amesema kuwa anatambua mchango wa UNFPA, Serikali ya Denmark na Serikali ya Tanzania kupitia OR-TAMISEMI, Mkoa wa Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika kuboresha Zahanati ya Dabalo kuwa Kituo cha Afya ili kiweze kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa kina mama wajawazito na Watoto Wachanga, kuimarisha mifumo ya rufaa kwa kutoa gari la kubebea wagonjwa lakini pia kutoa vifaa muhimu vya matibabu kwa kituo cha afya cha Dabalo, na Zahanati  nyengine tatu zaidi (Manda, Itiso & Nhinhi).

“Kupitia msaada huu, Zahanati ya Dabalo imeboreshwa na kuwa Kituo cha afya (ukarabati/ujenzi, vifaa) ili kuweza kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa wajawazito na watoto wachanga. Zahanati tatu za (Manda, Itiso & Nhinhi) zimepatiwa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kutoa huduma za Msingi kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga na gari moja la kubebea wagonjwa limenunuliwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za rufaa kwenye Wilaya hii. Aidha, kituo  cha huduma rafiki kwa vijana kimejengwa na kuanza kutoa huduma katika zahanati ya Nhinhi,” amesema Kairuki.

Ameongeza kuwa gharama za msaada huu ni  jumla ya Sh 615,205,539 ambapo Sh 327,000,000 zimetumika kwa ukarabati na ujenzi na Sh 288,205,539 zimetumika kwa ununuzi wa gari la kubebea wagonjwa na vifaa/vifaa tiba.

Awali, Mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania, Mark Bryan Schreiner alisema kuwa wanatambua dhamira ya pamoja na Serikali ya Tanzania kutoa haki na chaguo kwa wote, na kwamba wanaheshimu kujitolea kwa wahudumu wa afya katika kutoa huduma za afya ya uzazi na jinsia.

“Tunaitambua Serikali ya Denmark kama mtetezi dhabiti wa kimataifa wa afya ya uzazi na haki za uzazi, na Ubalozi wa Kifalme wa Denmark jijini Dar es Salaam kwa kusaidia uimarishaji wa mfumo wa afya ili kupanua uwezo wa huduma za afya ya uzazi nchini Tanzania.

“Tunaishukuru Serikali ya Denmark kwa ufadhili wa dola za Marekani milioni 2.3, ambazo zilisaidia mradi wa Kutambua Upatikanaji wa Haki za Afya na Haki za Ujinsia na Uzazi Vijijini hapa Tanzania. Shughuli nyingi za mradi zilifanywa kutoka 2019 hadi 2021,”amesema Schreiner.

Mradi huo unaofadhiliwa na Denmark pia ulianzisha kituo rafiki kwa vijana kwa huduma za afya ya uzazi na uzazi katika zahanati ya Nhinhi wilayani Chamwino. Katika kupongeza juhudi hizo, vijana 50 mjini Dodoma walipatiwa mafunzo ya Afya ya Ujinsia na Uzazi kwa Vijana, na kuzuia na kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia. Vijana hawa sasa wanafanya kazi kama waelimishaji rika, na wamechangia katika mradi huo kuwafikia vijana na vijana wapatao 50,000 wenye taarifa na huduma za Afya ya Ujinsia na Uzazi.

Balozi wa Denmark nchini, Mette Norgaard amesema: “Kupitia utoaji wa huduma za afya ya uzazi na taarifa, mradi unaofadhiliwa na Denmark umeleta mabadiliko katika maisha ya makumi ya maelfu ya wanawake, wanaume na vijana,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles