Ramadhan Hassan – DODOMA
WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani, amewatoa hofu Watanzania kwa kusema kuna mafuta ya kutosha licha ya changamoto ya wa corona ambapo amedai pia wameagiza mafuta ya kutosha kwa zaidi ya miezi miwili.
Akijibu hoja za wabunge juzi wakati akihitimisha hotuba yake ya bajeti ya 2020/21, Dk Kalemani alisema licha ya changamoto za corona nchini kuna nishati ya mafuta ya kutosha kutumiwa kwa zaidi ya miezi mwili.
“Tumeagiza mafuta ya kutosha miezi miwili ijayo na tunaziada ya lita milioni 368, niwaondoe wasiwasi Watanzania mafuta yataendelea kupatikana,”alisema.
Dk Kalemani alisema pia nchini kwa sasa kuna ziada ya megawati 312 za umeme hivyo anashangaa kusikia kuna maeneo umeme huwa unakatika.
“Naomba kutoa maelekezo kwa mameneja wa mikoa wasikate umeme labda kuwe ni dharura,”alisema.
Alisema kuanzia Julai mosi wizara itaanza kusambaza vifaa vya kuunganishia umeme ambavyo vitakuwa vikizalishwa hapa nchini.
“Pia umeme wa kuendesha treni kwa nchi za Afrika Mashariki sisi tumekuwa wa kwanza asilimia 82.2 umekamilika. Umeme vijijini umefika katika maeneo mengi.
“Leo pembe nne za nchi zetu zinang’aa umeme hata ukienda Uvinza kuna umeme, Mwasi, Masasi kuna umeme hakuna ambako haujafika,”alisema.
Kalemani alisema hadi Julai mwaka huu vijiji 1,822 vitakuwa vitapeleewa umeme.
“Vitongoji na maeneo ya mitaani hasa pembezoni mwa majiji yote tuna mkakati na tumetenga Sh bilioni 103.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Subira Mgalu, alisema wizara itaendelea kuchapa kazi kwa kuhakikisha kila eneo linakuwa na umeme na kutatua changamoto ya kukatikakatika kwa umeme.
Wabunge
Wakichangia mjadala wa bajeti hiyo, baadhi ya wabunge waliomba wizara hiyo kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi majumbani.
Mbunge Nanyamba Abdallah Chikota (CCM) alisema miradi mingine ya umeme imesimamiwa kikamilifu lakini usambazaji gesi majumbani ndiyo kasi yake bado hairidhishi.
“Nataka kuzungumzia usambazaji wa gesi majumbani, pamoja na uzuri wa wizara hii, usambazaji wake bado haukidhi mahitaji licha ya kuwa mmepeleka vijiji vingi lakini kwa muda ulioanzia kwa shughuli zake naona bado mnahitaji kuongeza kasi,” alisema Chikota.
Kuhusu umeme alisema hadi sasa malalamiko katika jimbo lake yamepungua na kwamba usambazaji wa umeme umetia matumaini kwa kufika katika maeneo mengi kwa wakati huu jambo ambalo ni faraja kwa wananchi.
Pia alitaka kasi ya ya ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ambayo itasaidia kuongeza umeme wa megawati 8 kwa wananchi wa Lindi.
Naye, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma, (CCM) alihoji kuhusiana na tatizo la kukatika kwa umeme katika mikoa ya kusini.
“Tatizo ni nini umeme kukatika mara kwa mara kule Kusini wakati mwingine wanasema mvua zikinyesha nguzo zinaanguka, basi tuwekewe nguzo za chuma ili mambo yaende sawa,”alisema.
Mbunge wa Chemba Juma Nkamia (CCM) alisema nguzo zimekuwa zikichimbiwa na kukaa kwa muda mrefu bila wahusika kusema kitu chochote.
Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema) aliitaka wizara hiyo kulipa madeni ya wakandarasi kwani wengi wamekuwa wakigoma kufanya kazi kutokana na kulipwa fedha zao.
“Madeni ya wakandarasi imekuwa ni changamoto hasa suala la kuwalipa hata kamati ilipoagiza wakandarasi waitwe kwanini kazi haziendelei wengi wanalalamika hawalipwi hivyo hawaaminiwi na wafanyakazi wao na Mabenki,”alisema.
Mbunge wa Tanga Mjini Musa Mbarouk (CUF) alisema kuna haja ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuangalia mita za luku ambazo wamekuwa wakizifunga kwani zimekuwa zikiwapa shida.
“Luku ni umeme ambao umesaidia sana lakini kuna kero lazima tuzizungumze unapowekewa mita ya luku unalazimishwa kukopeswa unit 50 na kwa bahati mbaya zikiisha lazima ukanunue Tanesco. Naomba jambo hili lirekebishwe huo sio utaratibu mzuri.
“Nitoe wito madeni ambayo yalikuwa na mita za zamani wafanye kwamba hayalipiki na wawasamehe. Suala zima la Rea kuna awamu tatu lakini awamu ya pili bado haijafika kwetu nipongeze Wizara ya Nishati kazi ni nzuri kule kwetu Mianjani wanakushukuru,”alisema.
Wizara ya Nishati imeidhinishiwa na Bunge bajeti ya Sh trilioni 2.197 kwa mwaka wa fedha 2020/21, kati yake Sh trilioni 1.44 zikiwa zimetengwa kwajaili ya utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Nyerere.
Mradi ho unaotarajiwa kutumia dola za Marekani bilioni 2.9 sawa na (Sh trilioni 6.5) hadi kukamilika kwake, ulitarajiwa kukamilika Juni 2022.
Akisoma bajeti yake bungeni, Dk Kalemani alisema Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi huo ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa bwawa, ujenzi wa njia kuu za kupitisha maji, ujenzi wa eneo la kufunga mitambo ya kufua umeme na ujenzi wa kituo cha kusafirisha umeme.
Alisema katika bajeti hiyo Sh trilioni 1.44 zimetengwa kwa mwaka 2020/21 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Alisema wafanyakazi 3,897 wameajiriwa tangu utekelezaji wa mradi uanze ambapo watanzania ni 3,422 sawa na asilimia 87.81 na kutoka nje ya nchi ni 475 sawa na asilimia 12.19.
Alisema hadi kukamilika kwa mradi Watanzania 6,000 wataajiriwa.
Bajeti ya Sh trilioni 2.19 iliyopitishwa jana na Bunge imeongezeka kutoka Shi trilioni 2.14 kwa mwaka 2019/20.