26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaangushwa mahakamani Sheria ya Huduma za Habari

Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA

 JOPO la Majaji watano wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), limesema vifungu vya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 vinakiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kauli hiyo imo ndani ya hukumu ya shauri namba 2 la mwaka 2017 lililofunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

 Akisoma hukumu hiyo   mjini hapa jana, Jaji Charles Nyachae, alisema mahakama hiyo imejiridhisha kwa maelezo na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na waleta maombi dhidi ya Serikali ya Tanzania.

 Alisema ni kweli kwamba vifungu vilivyopo kwenye sheria hiyo ukiondoa kifungu cha 14 na 18, vinakiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ni wajibu wa Serikali husika kuvifanyia marekebisho au kutunga sheria upya.

 “Sheria ya Huduma za Habari inapaswa kuendana na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kuhusu gharama za shauri hili zitabebwa na kila mtu,” alisema Jaji Nyachae.

  Wakili Jebra Kambore alisema miongoni mwa vifungu vilivyoonekana vina kasoro mbele ya Mahakama ni cha 7(2) kilichotoa maelekezo ya aina gani ya habari inayotakiwa kurushwa.

 “Vifungu namba 19, 20 21, 35, 36 37,38,30,40 vinavyohusiana na kujinaisha au kusema kashfa ni kosa la jinai vimefutwa, imeonekana kashfa haiwezi kuwa kosa la jina bali ni kosa la madai.

 “Vingine vilivyofutwa ni kifungu cha 52 na 53, vinavyohusiana na uchochezi ambako imeonekana vinakiuka haki za msingi za binadamu na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

 “Kifungu kingine ni 58 na 59 ambavyo vimetoa mamlaka kwa Waziri wa Habari kufungia aina fulani ya habari au baadhi ya magazeti yanayotoka nje kuja nchini, naavyo vimeonekana havipo sawa,” alisema Wakili Jebra.

   Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, alisema kutolewa kwa hukumu hiyo kumeifanya demokrasia kupata ushindi mkubwa mbele ya vyombo vya sheria.

 “Leo haki ya uhuru wa kupata habari imethibitishwa na Mahakama, haki ya waandshi wa habari kufanya kazi zao bila kuingiliwa isivyo halali imethibitishwa leo.

 “Hili ni jambo muhimu sana, huu ni ushindi wa  historia na ni ushindi kwa kila mtu kwa wananchi, wanahabari na serikali ya Tanzania kwa sababu imepewa wasaa wa kwenda kubadilisha sheria yake.

 “Vifungu vingi vya sheria hii vimeonekana kukiuka mkataba wa EAC kwa sababu  vinatoa masharti yanayokinzana na demokrasia ambayo imetamkwa kwenye Mkataba wa EAC.

“Kwa hiyo sheria hii inapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa kama ilivyoagiza Mahakama,” alisema Mukajanga.

   Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Fulgence Massawe alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa na kuanza kutumika kuliibuka malumbano mengi ya kuionyesha haifai kutumika kwa Watanzania.

 “Unapoingia kwenye mikataba ya kimataifa kama EAC lazima uheshimu na uufuate, sisi tuliona sehemu nzuri ya kuleta suala hili ni kwenye Mahakama hii ambayo leo majaji wametamka kwamba sheria hii inakiuka misingi ya haki za binadamu.

 “Tanzania ni sehemu ya Mkataba huu wa EAC na mahakama hii ina mamlaka ya kusikiliza mashauri   inapoona kuna mkataba umekiukwa pia uamuzi wake umeifunga nchi.

 “Kwa hiyo nchi kama Tanzania ina jukumu la kutekeleza maagizo ya yaliyotolewa na Mahakama hii na kama Serikali ya Tanzania haitatekeleza uamuzi uliotolewa sisi mawakili tutarudi tena hapa kuikumbusha,” alisema Wakili Massawe.

Mwaka 2017, waleta maombi watano walifungua shauri hilo kupinga Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 iliyoonekana kuminya uhuru wa habari kinyume na Katiba ya Tanzania pamoja kuikuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 Walidai Sheria hiyo inakiuka kifungu cha 6(d), 7(2) na 8 (1) (c) cha Mkataba wa EAC kwa kuwa haiendani na misingi ya utawala bora, uwazi, demokrasia na utawala wa sheria na binadamu.

 Asasi hizo tano ziliiomba Mahakama itamke kuwa vifungu vya 7 (3) (a) (b) (c) (f) (g) (h) (i) na (j) 13, 14, 18, 19, 20, 21, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 54, 52, 53, 58, na 59 vya sheria hiyo vifutwe kwa kuwa vinaminya uhuru wa habari.

 Shauri hilo lilisikilizwa na Jopo la Majaji watano ambao ni Jaji Kiongozi Monica Mugenyi, Naibu Jaji Kiongozi Jaji Faustine Ntezilyayo, Jaji  Fakihi Jundu, Jaji Audace Ngiye na Jaji Nyachae aliyesoma hukumu hiyo.

 Upande wa mawakili wa waleta maombi walikuwa ni   Donald Deya, Fulgence Massawe, Jenerali Ulimwengu na    Jebra Kambore, wakati upande wa Jamhuri waliwakilishwa na mawakili Mark Mulwambo na Sylvia Matiku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles