30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bodi kutathmini elimu Afrika Mashariki yaanzishwa

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MABARAZA na Bodi za Mitihani za Afrika Mashariki zimekubaliana kuanzishwa kwa umoja katika tathimini ya elimu, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuweka urahisi wa wanafunzi wa nchi za ukanda huo kwenda kusoma eneo jingine.

Kabla ya mfumo huo, baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakitoka nchi moja kwenda nyingine kusoma elimu ya sekondari walikuwa wanapata vikwazo kujiunga na elimu ya juu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk. Charles Msonde, alisema umoja huo uliopewa jina la EAAEA ulizinduliwa Dar es Salaam.

Dk. Msonde aliyechaguliwa kuwa Rais wa EAAEA na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Uganda, Dan Odongo akiwa Katibu Mkuu, alisema wazo la kuanzishwa umoja huo lilijadiliwa na kuridhiwa katika mkutano wa wakuu wa mabaraza/bodi za mitihani za nchi husika uliofanyika Dar es Salaam Machi mwaka jana.

“Kutokana na uamuzi huo, timu ya wataalamu kutoka nchi hizo iliundwa na kupewa jukumu la kuandaa rasimu ya katiba ambayo itatumika katika uendeshwaji wa umoja huo,” alisema Dk. Msonde.

Alisema kumekuwepo changamoto za wanafunzi wa nchi tofauti kwenda kusoma nchi nyingine, lakini sasa watazijadili na kuziweka sawa.

“Sasa kunakuwa na urahisi wa watoto kwenda kusoma eneo jingine na taarifa zao zinajulikana katika nchi ambazo watakwenda kusoma,” alisema.

Alisema sababu za kuanzishwa umoja huo ni pamoja na kuwapatia uelewa na ujuzi wanachama wake kupitia mafunzo mbalimbali yatakayoandaliwa kwa nchi wanachama, na hivyo kuwaongezea utaalamu katika masuala ya tathmini na utahini.

“Pia kuimarisha umoja na mshikamano baina ya nchi wanachama katika masuala ya tathmini ya mitihani ya taifa kwa kushiriki mikutano.

“Vilevile kupata fursa ya kufanya tafiti na kufanya machapisho ya matokeo ya tafiti mbalimbali kuhusu masuala ya elimu kwa nchi wanachama ambayo yatatumika kibara na dunia kwa ujumla.

“Sababu nyingine kubadilishana uzoefu katika kudhibiti udanganyifu na mianya inayotumika katika ukiukwaji wa uendeshaji mitihani ya taifa.

“Kuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu na ujuzi wa namna bora ya kufanya tathmini ya elimu katika nchi za Afrika Mashariki, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa viongozi wa nchi wanachama kuhusiana na masuala ya tathmini na utahini katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Dk. Msonde.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa umoja huo, Odongo, alisema wanaamini kuanzishwa kwa umoja huo kutaziweka nchi wanachama kuwa karibu na kuweza kusonga mbele katika masuala ya tathmini na utahini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles