24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awa mbogo

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amegeuka mbogo kutokana na kuendelea kwa vitendo vya rushwa nchini, huku akitolea mfano yaliyofanywa na maofisa wa Serikali baada ya kuagiza ndege ya Serikali iliyokuwa ikibeba viongozi ipelekwe Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kubeba abiria.

Pia amegusia madudu yaliyokuwa yakifanywa na maduka ya kubadilishia fedha na baadhi ya mabalozi akisema kuna wajuaji wengi nchini.

Kutokana na hali hiyo, aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutomwogopa mtu hata kama ni mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) au jeshi na badala yake kuwachukulia hatua wote.

Akizungumza jana wakati wa kumwapisha Balozi Valentino Mlowola anayeenda Cuba, na kupokea taarifa ya Takukuru ya mwaka 2017/2018, Rais Magufuli alisema pia wapo wawekezaji ambao wameshindwa kuwekeza kwa sababu ya rushwa.

MAGARI 194

Alisema hivi karibuni mtu mmoja aliingiza magari 194 bila kulipia kodi inayofikia zaidi ya Sh bilioni 8, lakini akashangaa namna anavyotetewa na kukingiwa kifua.

“Nilikuweka wewe kamishna wa polisi (Mkurugenzi Takukuru, Kamishna Diwani Athuman) kwa sababu unaweza kumshika mtu wakati wowote, ukishindwa kutumia sheria za Takukuru tumia za polisi.

“Huyu pia (yaani mkurugenzi huyo) ni mtumishi wa TISS, kwahiyo hata kama mtumishi wa TISS amefanya kosa la rushwa unamshika.

“Brigedia Jenerali (Naibu Mkurugenzi Mkuu Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo) hata kama ni mwanajeshi atamshika na kumuweka ndani,” alisema.

KIGOGO TAKUKURU

Rais Magufuli alisema kuna mkurugenzi mmoja wa makao makuu Takukuru aliwauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake, lakini anashangaa hajapelekwa mahakamani hadi sasa.

“Wala sijapata taarifa kwamba hizo fedha amezirudisha kwa wafanyakazi aliowadhulumu. Wafanyakazi wanaumia, wanalalamika pembeni.

“Amewadanganya kwamba ana viwanja Bagamoyo, lakini mpaka leo hawajapewa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kashfa hiyo iliibuliwa tangu Balozi Mlowola alipokuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Suala hili lilianza tangu wakati wa Balozi Valentino, nikamuuliza huyu mbona harudishi fedha au hapelekwi mahakamani, akawa na kigugumizi, sasa na wewe usiwe na kigugumizi kwa sababu nafasi za ubalozi zimeisha.

 “Ndiyo maana huwa najiuliza hawa Takukuru huwa ni kwa ajili ya watu wengine, wao ‘hawaji-takukuru’ humo humo ndani?” alihoji.

UFISADI ATCL

Ufisadi mwingine ulioibuliwa na Rais Magufuli ni ule unaoihusu ATCL wa zaidi ya Sh milioni 200.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ufisadi huo unahusisha kubadilisha maneno kutoka katika ndege iliyokuwa ya Serikali na kuchora twiga ili iweze kutumika kibiashara.

“Nilizungumza ndege ya Serikali ipelekwe ATCL iwe inatumika kubeba abiria na viongozi tutapanda hiyo hiyo.

“Sasa ikawa suala la kubadilisha maneno (Air Tanzania) na kuchora yule twiga. Wakasema kumchora twiga na kuandika maneno haviwezi kufanyika Tanzania.

“Zikachaguliwa nchi tatu sitaki kuzitaja, nikasema jamani hapana, tafuteni wataalamu wenu wanajua kuchora, mbona kila mahali ukienda kuna michoro mingi tu hata ya Tingatinga watashindwa kumchora twiga.

“Mbona wanachora simba na hata kuchonga, wakawa wameshatafuta nchi fulani, nikanyamaza,” alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo alisema licha ya kutoa ushauri huo, alishangaa kusikia tayari wameandaliwa watu watakaoisindikiza ndege hiyo ambao wameshalipwa Dola za Marekani 28,000 (Sh milioni 60) na mkandarasi husika alishalipwa asilimia 60 (Sh milioni 200).

“Sasa ndege inapelekwa gereji wanasindikiza kwenda kufanya nini, wanakwenda kumuhudumia nani kule na inakwenda kupakwa rangi. Na siku zimeshapangwa nafikiri 15 au mwezi mzima, wakakae wanaisubiri inapakwa.

“Baadaye Jumapili moja nikaambiwa ndege inaondoka kesho asubuhi, nikasema hii ndege ikiondoka hao watakaokuwa wamehusika nao wanaondoka saa hiyo hiyo.

“Ndege haikuondoka na imepakwa kwa Sh milioni tano na inawezekana leo au kesho itatoka,” alisema Rais Magufuli.

VIONGOZI WA CCM

Rais Magufuli alisema rushwa haina chama, hivyo aliiagiza Takukuru hata kama ndani ya CCM, Chadema kuna walarushwa washughulikiwe.

“Nilipigiwa na raia fulani kwamba wanaombwa rushwa ya Sh milioni tano na viongozi wa CCM ili wawapangishe kwenye majengo yaliyoko Ilala.

“Nikamtafuta mkurugenzi mmoja Takukuru, nikamwambia shughulika na hii na baada ya masaa mawili wakashikwa.

“Ndani ya CCM kuna rushwa, muendelee hivyo hivyo kama ukimkuta mwana-CCM, Chadema anakula rushwa shika hata yeyote ambaye hana chama,” alisema.

Alisema pia kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Takukuru kuokoa Sh bilioni 70.3 watatafuta fedha kuhakikisha ofisi za taasisi hiyo zinafuguliwa katika wilaya 21.

MADUKA YA KUBADILISHIA FEDHA

Rais Magufuli alisema walibaini maduka mengi ya kubadilishia fedha yalikuwa ni uchochoro wa kuchukua fedha na kupeleka nje.

“Watu wanachukua fedha BoT (Benki Kuu ya Tanzania) kwa ajili ya kuuza kwenye maduka ya fedha, lakini ukiwafuata wameuza kiasi gani hawakuelezi na wala hakuna ripoti.

“Wanatumia ‘exchange’ Euro moja wanamuuzia mtu kwa Sh 1,400 kisha wanaichukua hiyo ‘cotation’ kwamba sasa ‘exchange ya T-Sh’ imepanda juu. Kule ni kuharibu uchumi wa nchi, ilikuwa utapeli tu,” alisema Rais Magufuli.

MABALOZI

Alimtaka Balozi wa Cuba, Mlolowa, kuripoti haraka katika kituo chake cha kazi na akawatahadharisha wateule wake ambao wamekuwa wakichelewa kwenye vituo vyao kwa kigezo cha kuaga.

“Sasa ninakushauri balozi (Mlowola), wewe ni askari tumeshamalizana hapa, kapange kazi nenda Cuba. Mke wako kama ni mfanyakazi wa Serikali, waziri ampangie kazi huko huko, ndiye atakuwa msaidizi wako, utatafuta wafanyakazi wengine wachache basi.

“Nimeshawaona hawa mabalozi nikiwateua kila siku wako kwenye ofisi wanakwenda kuaga, nimemteua Balozi wa Zambia sifahamu kama ameshaondoka.

“Kila siku unamuona yuko kwa makamu wa rais, waziri mkuu, mara yuko Zanzibar… sasa nimeshakuteua bado unazunguka tu huko kila siku eti anaaga, kwani hayajui ya Tanzania?

“Nikishakuteua wala uhitaji kuja kuniaga, nenda tu kwenye kituo chako. Sasa huyu wa Zambia bado amebakiza nani… ataenda kwa wakuu wa mikoa akawaage, siku atakapomaliza kuwaaga atakuta ubalozi hana, yeye aendelee kuaga tu,” alisema Rais Magufuli.

MKURUGENZI TAKUKURU

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani, alisema kwa mwaka 2017/2018 taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Sh bilioni 70.3 ikilinganishwa na Sh bilioni 14.6 za mwaka 2016/2017.

Alisema pia wameongeza idadi ya ufunguaji wa kesi mahakamani ambapo 2017/2018 ilifanikiwa kufungua kesi 495 ikilinganishwa na 435 za 2016/2017.

Diwani alisema kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 14.69, kutaifisha nyumba saba na magari manne.

Alisema wameweka zuio la mali zikiwamo akaunti za fedha zenye zaidi ya Sh bilioni 20, nyumba 26, viwanja 47, magari 61 na mashamba 13.

Alifafanua kuwa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za kuanzia Julai 2015 hadi Juni 2018 zimefanyiwa kazi na hadi sasa mashauri 16 yamefunguliwa mahakamani.

Hata hivyo alisema majalada 64 yako katika hatua mbalimbali za uchunguzi.

“Bado uchunguzi unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa nyaraka halisi kwa wakati au kutopatikana kabisa na kusababisha kuchelewa kukamilika,” alisema Athuman.

Mkurugenzi huyo alisema Kurugenzi ya Uchunguzi imefanikiwa kuchunguza na kukamilisha majalada 906 na kati ya hayo 699 yalihusu hongo na 208 vifungu vingine vya sheria ya Takukuru.

Alifafanua kuwa majalada mapya 465 yaliwasilishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuombewa kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani na kati ya hayo 265 yalipata kibali.

Alisema kesi 495 zilifunguliwa mahakamani na kati ya hizo 208 zilihusu hongo na 287 makosa mengine.

“Kwa ujumla kesi za rushwa 624 ziliendelea katika mahakama zote Tanzania, kesi 296 zilitolewa uamuzi na mahakama na kati ya hizo 178 washtakiwa walitiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali na kesi 118 washtakiwa waliachiwa huru.

“Idadi ya kesi zilizoshinda zimeongezeka na kufikia asilimia 60.1 ikilinganishwa na asilimia 41 iliyofikiwa 2016/2017,” alisema.

Alisema pia kuanzia 2016 hadi 2018 Sh bilioni 13.11 zimerejeshwa serikalini na watuhumiwa waliokiri kukwepa kulipa kodi baada ya kuhojiwa na Takukuru na kukubali kwa ridhaa yao wenyewe kulipa madeni husika.

Mkurugenzi huyo alisema wamefungua kesi kubwa tatu zinazohusu wafanyabiashara waliokwepa kodi zenye thamani ya Sh bilioni 27.78.

“Kwa mwaka 2019 kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tumeshasajili kesi tano katika Mahakama ya Mafisadi ambazo ziko katika hatua mbalimbali,” alisema.

Kuhusu miradi ya maendeleo, alisema miradi 661 yenye thamani ya Sh trilioni 1.49 ilifuatiliwa katika sekta za kipaumbele ambazo ni maji, ujenzi, afya na elimu.

Hata hivyo, alisema wamebaini ufujaji wa fedha za umma katika miradi 63 yenye thamani ya Sh bilioni 32.75.

“Ufujaji uliobainika unatokana na matumizi ya vifaa vilivyo chini ya kiwango vilivyonunuliwa kwa thamani ya bei ya vifaa vyenye viwango vinavyotakiwa,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema miradi 408 yenye thamani ya Sh bilioni 346.26 ilibainika kuchelewa kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mikataba.

Alisema kati ya hiyo, miradi minane yenye thamani ya Sh bilioni 969.88 ilikuwa ni miradi ya maji ya kitaifa na kwamba wameanzisha uchunguzi kwenye miradi 81 yenye thamani ya Sh bilioni 44.97 baada ya kubainika kuwa na kasoro.

HALI YA RUSHWA

Mkurugenzi huyo alisema utafiti uliofanywa na Transparency International Corruption Perception Index umeiweka Tanzania kwenye nafasi ya 99 kati ya nchi 180 kwa kiwango cha rushwa na kupata asilimia 36 ikilinganishwa na nafasi ya 103 ya mwaka 2017.

Alisema tathmini nyingine ya Mo Ibrahim ilionesha kuwa Tanzania imefanya vizuri katika eneo la utawala bora na kupata asilimia 58.5 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 57.5 za mwaka 2016.

Mkurugenzi huyo alisema pia utafiti wa Afro Barometa wa 2018 ulionesha kuwa asilimia 72 ya Watanzania waliohojiwa walisema kiwango cha rushwa nchini kimepungua ikilinganishwa na asilimia 66 waliohojiwa mwaka 2014 ambao walisema kimeongezeka.

Alisema pia utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza mwaka 2017 ulionesha kuwa asilimia 85 ya Watanzania waliohojiwa walisema kiwango cha rushwa nchini kimepungua ikilinganishwa na asilimia 11 waliohojiwa mwaka 2014.

“Kwa mwaka 2019 Takukuru itafanya utafiti wa kitaifa wa kupima hali ya rushwa katika sekta mbalimbali na juhudi zinazofanyika kupambana na rushwa nchini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles