Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imekubali ombi la mabalozi wa nchi mbalimbali la kuandaa kikao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wawekezaji kutoka nchi zao.
Mabalozi walioomba kikao hicho ni pamoja na wale wa Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden na Ujerumani.
Akijibu ombi hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alisema serikali iko tayari kujadiliana na mabalozi hao kama walivyoomba, wakiamini kikao hicho kitakuwa na tija na kushughulikia changamoto zilizojitokeza.
“Nimekubali maombi yenu ya kikao kujadili changamoto mlizoziorodhesha na nitaandaa uwepo wa maafisa wa serikali kutoka taasisi husika kama mlivyoomba. Ili kikao kiwe na tija, tunaomba wawekezaji mnaowazungumzia waje na vielelezo vya kina vya changamoto zinazowakabili,” alisema Waziri Makamba.
Waziri Makamba aliwahakikishia mabalozi dhamira na nia dhabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuboresha mazingira ya kibiashara nchini, ili kuvutia uwekezaji kutoka nje (FDI). Alieleza kuwa serikali imefanikiwa kuongeza uwekezaji kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 3 mwaka 2022 mpaka Bilioni 5.5 mwaka 2023.
Kikao hicho kinatarajiwa kuleta mwanga mpya katika juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuondoa vikwazo vinavyowakabili wawekezaji kutoka nje.